THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kwa mijadala isiyoisha na vikao
vya kulipana posho bali kwa viongozi kufanya maamuzi na kuyatekeleza
haraka.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania inachelewa kupata maendeleo ya
haraka kwa sababu kila mtu anayepewa kazi anataka kwanza kujadili badala
ya kuchukua maamuzi na kuyatekeleza.
Rais
Kikwete ametoa tahadhari hiyo ya kuchelewesha maendeleo wakati
alipozindua Kambi ya Vijana ya Kilimo na Maarifa ya Mkongo, Wilaya ya
Rufiji, Mkoa wa Pwani kwenye siku yake ya tatu ya ziara ya kikazi katika
Mkoa huo leo, Jumamosi, Oktoba 5, 2013.
Akizungumza
na wananchi kabla ya kuzindua kambi hiyo na kukagua shughuli
zinazofanywa na vijana 50 kutoka vijiji vya Wilaya ya Rufiji ambao
wanajifunza mbinu na maarifa ya kilimo bora katika kambi hiyo, alitaka
kujua kama makampuni mawili yaliyoomba ardhi ya kulima kisasa katika
bonde la Mto Rufiji, yamepewa ardhi ya kuanza kulima.
Awali
katika maelezo yaliyosomwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo
ya Bonde la Rufiji (RUBADA), Bwana Aloyce Masanja yaliashiria kuonyesha
kuwa makampuni hayo, Frontline Development Partners na Lukurilo Holdings
Company Limited yalikuwa yamepewa ardhi na Mamlaka hiyo kama
yalivyokuwa yameomba.
Lakini
Rais Kikwete alipotaka maelezo ya ziara kutaka ukweli kama makampuni
hayo yamepewa ardhi na ni kiasi gani, Bwana Masanja alithibitisha kuwa
Frontline Development Partners walioomba hekta 20,000 walikuwa
hawajapewa hata hekta moja na kuwa Lukurilo Holdings walioomba hekta
12,000 walikuwa wamepewa 4,000 tu.
Rais Kikwete alishangazwa na hali hiyo na kusema: “Kwa
miaka minne sasa tumekuwa tunazungumza jambo hili bila kufikia uamuzi
wake. Tumewahi kujadili suala hili pale Ikulu, Dar Es Salaam, na
kukubaliana. Imetokea nini? Tulikubaliana kutekeleza jambo hilo sasa
tunaendelea kujadili nini?”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nchi
yetu itachelewa sana kupata maendeleo kwa sababu kila mtu anayepewa
kazi anataka kuanza kujadili. Tanzania haiwezi kuendelea kwa mijadala na
kwa vikao vya kulipana posho visivyoisha. Hatuwezi kuendeleza nchi kwa
mwenendo huu – Frontline Company imeanza kuomba ardhi ya kulima kiasi
cha miaka mitano iliyopita…”
Rais Kikwete ambaye amewaamuru viongozi wote wanaohusika na suala hilo kukutana wiki ijayo amesema: “Nchi
inakwamishwa na watu wa namna hii, kila siku kuzungumza na
kujadiliana…hadithi haiishi. Maendeleo yetu yanachelewa kwa sababu
mizunguko – kila siku mnazunguka, hamumalizi.”
Mapema
Rais Kikwete amewaambia viongozi wa kambi hiyo ambayo inamilikiwa na
RUBADA kuwa kazi ya kambi hiyo iwe ni kuandaa vijana wa kujiajiri kwa
kilimo cha kisasa na siyo kuandaa watu wa kutafuta kazi ya kuajiriwa
katika kilimo.
“Tunaandaa
wakulima wazuri, vijana, na siyo tunaandaa kundi la watu wa kutafuta
ajira ya kilimo. Hatuwezi kuwa na kambi ya namna hii ikiandaa kundi la
watu wa kutafuta ajira…kijijini utaajiriwa na nani kama siyo kushiriki
kilimo?”
Rais
Kikwete, hata hivyo, amesema kuwa amefurahishwa na uamuzi wa kuandaa
vijana hao kushiriki katika kilimo kwa sababu mageuzi ya kilimo
yataletwa na vijana.
“Tukiingiza
vijana katika shughuli za kilimo basi mageuzi ya kilimo katika nchi
yetu yanawezekana kwa sababu ni dhahiri kuwa mageuzi ya kilimo yatakuwa
magumu kuletwa na baba zao, na magumu zaidi kuletwa na babu zao.”
Rais
ambaye alikuwa kwenye ziara ya Wilaya ya Rufiji pia amezindua mradi
mkubwa wa maji mjini Kibiti na amekabidhiwa boti ambazo zitafanya
shughuli za kubeba wagonjwa katika maeneo ya Nyamisati na visiwa vya
jirani.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
5 Oktoba, 2013
No comments:
Post a Comment