Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, October 7, 2013

UCHAGUZI TFF UTAFANYIKA OKTOBA 27- TENGA



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi wa kupata Kamati mpya ya Utendaji ya shirikisho utafanyika Oktoba 27 mwaka huu kama ilivyopangwa.
“Wazungu wanasema ije mvua au jua, uchaguzi utafanyika. Isipokuwa tunachotaka kuhakikisha ni kuwa unakuwa uchaguzi huru na wa haki,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana (Oktoba 7 mwaka huu).
Amesema mchakato unakwenda vizuri kilichobaki ni revision (mapitio) na rufani, masuala ambayo yako mbele ya Kamati ya Rufani ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi.
Rais Tenga amesema lengo la hatua hizo si kuzuia watu wasigombee kwani ni lazima mambo ya msingi ikiwemo sifa za wagombea yaangaliwe, lakini kwenye haki ni lazima kuhakikisha inatendeka hata kama ni kwa mtu mmoja.
Mchakato wa uchaguzi ulivutia waombaji 58 ambapo watatu wamekata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kupinga kuondolewa na Kamati ya Uchaguzi wakati wengine wanane masuala yao yamepelekwa Kamati ya Rufani ya Maadili kwa njia ya mapitio (revision) ili kupata mwongozo wa utekelezaji.
Mwongozo huo umeombwa na Sekretarieti ya TFF kwa Kamati ya Rufani ya Maadili kwa vile Kamati ya Maadili iliwaona waombaji wanane wa uongozi waliofikishwa mbele yake kwa makosa ya kimaadili kutokuwa na hatia, lakini wakati huo huo ikitambua kuondolewa kwao kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kulikofanywa na Kamati ya Uchaguzi.
MRADI WA FOOTBALL FOR HOPE KUFUNGULIWA OKTOBA 13
Mradi wa Football for Hope kusaidia watoto na wasiojiweza kupitia mpira wa miguu uliofadhiliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) mkoani Iringa utafunguliwa rasmi Oktoba 13 mwaka huu.
FIFA hutoa mradi huo kwa baadhi ya nchi kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo utawala bora, lakini kwa kupitia taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) ambapo kwa Tanzania umepatikana kupitia taasisi ya Iringa Development of Youth, Disabled and Child Care (IDYDCC).
Rais wa TFF, Leodegar Tenga ameishukuru FIFA kwa msaada huo, kwani ni mkubwa na kuongeza kuwa ni matumaini yake utatumika kwa lengo lililopangwa.
Amesema mradi huo wa FIFA ambao ni wa kusaidia watoto kielimu na wasiojiweza kwa kupitia mpira wa miguu haukupita moja kwa moja TFF ni mzuri kwani moja ya mambo uliofanikisha ni kuwepo jengo na sehemu ya watoto kucheza.
Ni wastani wa nchi kumi tu duniani kwa mwaka zinapata mradi huo kutoka FIFA, jambo ambalo Rais Tenga amesema linachangiwa pia na uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na shirikisho hilo.
KAMATI YA WANAWAKE, TWFA YAPONGEZWA
Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) wamepongezwa kwa kuhakikisha akina mama wanacheza mashindano mbalimbali.
Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambapo amesema timu za wanawake zimekuwa zikishiriki katika mashindano mbalimbali licha ya ukweli kuwa hadi sasa hakuna udhamini kwenye mchezo huo.
Amesema mpira wa miguu unaendeshwa na udhamini na kuchangia, jambo ambalo linafanikishwa kwa kiasi kikubwa na uwazi katika matumizi ya fedha, jambo ambalo hivi sasa lipo ndani ya TFF.
Rais Tenga amesema baada ya kuanzisha Kamati ya Ligi, hivi sasa TFF inapata asilimia 4.5 tu ya mapato ya mechi za ligi kutoka asilimia 33 iliyokuwa ikipata wakati anaingia madarakani mwaka 2004.
Amesema asilimia hiyo 4.5 haiwezi kuendesha mpira na ndiyo maana nguvu zinaelekezwa katika kutafuta wadhamini na kuchangia. Pia TFF inatoa zaidi ya asilimia 15 ya Fedha za Msaada wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FAP) kutoka FIFA kwenye mpira wa miguu wa wanawake ambapo ni nchi chache zinazofikia kiwango hicho.
Hivyo, ametoa mwito kwa kampuni kujitokeza kudhamini au kuchangia timu za Taifa za mpira wa miguu za wanawake ambazo zinashiriki mashindano mbalimbali mwaka huu, kwani gharama za kuziendesha ni kubwa.
Timu ya wakubwa (Twiga Stars) inacheza mashindano ya mchujo ya Fainali za Afrika (AWC) zitakazofanyika mwakani nchini Namibia wakati ile ya chini ya miaka 20 inacheza mashindano ya Dunia ambayo fainali pia zitachezwa mwakani nchini Canada.

No comments:

Post a Comment