Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, October 10, 2013

Viongozi watoa wito kwa Wakenya kuondoa uchochezi wa mapigano ya kidini


Viongozi wa kisiasa na kidini nchini Kenya wanatoa wito kwa pande zote kuondoa hasira za kidini ambazo ni za ukatili mkubwa kufuatia shambulio la al-Shabaab kwenye kituo cha biashara cha Westgate huko Nairobi mwezi uliopita na kuuawa kwa maulamaa wanne wa Kiislamu huko Mombasa wiki iliyopita.
  • Askari polisi akijibu moto kwenye kanisa la Jeshi la Wokovu huko  Mombasa, lililopangwa na kutekelezwa na wapingaji Ijumaa (tarehe 4 Oktoba). [Rajab Ramah/Sabahi] Askari polisi akijibu moto kwenye kanisa la Jeshi la Wokovu huko Mombasa, lililopangwa na kutekelezwa na wapingaji Ijumaa (tarehe 4 Oktoba). [Rajab Ramah/Sabahi]
  • Polisi wakiwatawanya wapingaji huko Mombasa huku magurudumu yakichomwa na kutoa moshi mweusi. [Rajab Ramah/Sabahi] Polisi wakiwatawanya wapingaji huko Mombasa huku magurudumu yakichomwa na kutoa moshi mweusi. [Rajab Ramah/Sabahi]
  • Polisi waliwakamata baadhi ya wapingaji, wengi wao wakiwa ni vijana, katika kuchukua hatua kali za kinidhamu katika jiji lote. Vijana wanne walifariki dunia katika mapambano na polisi. [Rajab Ramah/Sabahi] Polisi waliwakamata baadhi ya wapingaji, wengi wao wakiwa ni vijana, katika kuchukua hatua kali za kinidhamu katika jiji lote. Vijana wanne walifariki dunia katika mapambano na polisi. [Rajab Ramah/Sabahi]
Ghasia zilianza Ijumaa iliyopita (tarehe 4 Oktoba) huko Mombasa baada ya watu wenye silaha ambao hawajajulikana kumuua Sheikh Ibrahim Ismail na watu watatu aliokuwa nao kwa kupigwa risasi wakati akiendesha gari Alhamisi jioni.
Ismail alionekana kwa sehemu kubwa kama mrithi wa muhubiri matata Aboud Rogo Mohammed. Watu wote wawili walikuwa na mfungamano wa karibu na Msikiti wa jiji hilo wa Masjid Musa.
Wapingaji walianza machafuko katika kanisa la Jeshi la Wokovu la jiji hilo, na vijana wanne waliuawa katika kukabiliana na polisi.
Mratibu Mkuu wa Jukwaa la Haki za Binadamu la Kiislamu al-Amin Kimathi aliwalaumu polisi kwa mauaji ya Ismail na kwa kushindwa kuhimili vurugu zilizofuatia baadaye.
"Polisi wanatumia faida ya mihemko ya wananchi iliyopo iliyochochewa na shambulio la kigaidi la Westgate," Kimathi aliiambia Sabahi, akitahadharisha kwamba kama "mauaji nje ya mahakama " hayatakomeshwa yatarudisha nyuma vita dhidi ya ugaidi.
"Shambulio hilo ni kinyume na aina zote za sheria katika ardhi hii na kinyume na kanuni zote za haki za binadamu," alisema. "Bila kujali kiasi cha uhalifu kilichofanywa na mtu, tuna taasisi zinazofanya kazi. Waache watuhumiwa wa jambo lolote kupelekwa mbele ya sheria."
Mkuu wa Polisi wa kaunti ya Mombasa Robert Kitur alikana kwamba polisi walihusika na chochote katika kufyatua risasi.
"Hatukuhusika kabisa na mauaji hayo. Hivyo sivyo tunavyofanya kazi. [sheria ya polisi] ni kuwakamata washukiwa wowote na kuwafikisha mbele ya mahakama zetu, sio kuwaua," Kitur aliiambia Sabahi.
Kitur alisema polisi walikuwa wanachunguza mauaji na wameimarisha ulinzi ili kuzuia kutokea tena kwa fujo siku zijazo, na kwamba hali ya kawaida imerejea Mombasa.

Viongozi wa Kiislamu walaani vurugu, kuchomwa kwa kanisa

Wawakilishi kutoka Baraza Kuu la Waislamu la Kenya (SUPKEM), Kamati ya Msikiti wa Jamia, Majlis Ulamaa Kenya, Baraza la Maimamu la Kenya na Ulamaa, na Jukwaa la Waislamu la Haki za Binadamu wameshutumu mauaji ya muhubiri wa dini, pamoja na uchomaji wa kanisa.
Katibu Mkuu wa SUPKEM Adan Wachu aliiambia Sabahi kwamba mauaji yalilenga kutisha na kudhoofisha hali ya usalama nchini Kenya ambayo inahitaji kushughulikiwa haraka ili kuhakikisha kwamba sheria na utulivu vinatawala.
"Ingawa tunarudia kutoa shutuma zetu za mauaji ya watu wengi ya Westgate, pia tunashtushwa na vurugu ambazo zilijitokeza katika matokeo ya mauaji yasiyoidhinishwa ya wahubiri wanne wa kiislamu siku ya Alhamisi, mashambulizi yasiyo na sababu katika kanisa na mali binafsi huko Mombasa baada ya swala ya Ijumaa," Wachu alisema.
Shambulizi la Westgate na mauaji huko Mombasa yanalenga kuchochea uhasama baina ya dini nchini, alisema.
"Tunatoa wito kwa wapenda amani wote wa Kenya kutokubali kuangukia katika mitego ya mambo hayo ya wahalifu wanaolenga katika kuchochea chuki baina ya Wakenya," Wachu alisema.
"Wale wanaohusika na uchomaji wa kanisa la Jeshi la Wokovu ni wahalifu ambao hawaiheshimu dini," alisema." Uislamu hauruhusu tabia kama hiyo ya kuchukiza na hata katika nyakati za migogoro, maadili ya Kiislamu yako wazi kwamba nyumba za ibada na wanaozitumia hazipaswi kushambuliwa au kuharibiwa kwa namna yoyote."
Seneta wa chama cha National Alliance Emma Mbura, anayewakilisha Kaunti ya Mombasa, alitoa wito kwa mashirika ya ulinzi kuboresha mbinu za kipolisi kutotegemea mauaji ya nje ya mahakama, ambayo alisema yanaweza kuongeza mvutano baina ya dini.
"Kila mmoja anapaswa kuchukuliwa hana makosa hadi hapo atakapothibitika kuwa na kosa, kwa kuwa kuua hakuwapi watuhumiwa siku zao katika mahakama," aliiambia Sabahi. "Kinachofuata ni kwamba watu wasio na hatia wanaweza kuwa waathirika, na wale wanaoachiwa wakawa na hasira na wanaweza wakaingia katika kulipiza kisasi."
Mbura alionya kwamba mauaji kama hayo yanaweza kusababisha vijana kuwaunga mkono al-Shabaab na hata kuwashawishi kujiunga na wanamgambo, lakini kuwapeleka watuhumiwa wa ugaidi mahakamani kunauruhusu umma kutambua makosa ya wanaotuhumiwa.

Kubatilisha agizo la polisi la 'kupiga risasi na kuua'

Wakati huo, baadhi ya waangalizi wanamuomba Inspekta Jenerali wa Polisi David Kimaiyo kubatilisha maagizo ya upigaji risasi na kuua aliyoyatoa mwezi Septemba, akisema kwamba mashirika ya usalama yamesikiliza maelekezo kwa kutumia nguvu ya ziada.
"Inapotokea maisha ya ofisa au mtu mwingine yanakuwa hatarini, polisi lazima watumie risasi za moto kwa ufanisi. Na hili ni agizo kwa maofisa polisi wote nchini Kenya," Kimaiyo alisema tarehe 13 Septemba wakati wa uzinduzi wa ushirikiano kati ya huduma za polisi na serikali ya Kaunti ya Mombasa.
Alisema hilo agizo lilikusudia "kushughulikia kikamilifu wahalifu ambao pia wanahatarisha maisha ya wengine".
Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar Hassan alisema mauaji ya maulamaa hao yaliyotokea wiki iliyopita huko Mombasa yalikuwa ni matokeo ya maelekezo ya Kimaiyo.
"Agizo hilo, ambalo bado linafuatwa hata baada ya tukio la Westgate linahatarisha usalama wa pamoja wa baadhi ya jamii," alisema, akiongeza kwamba Kimaiyo anapaswa kuzingatia tena agizo hilo katika kipindi hiki kibaya.
"Kama polisi wanaweza kusikiliza agizo la kiongozi wao la 'kupiga risasi na kuua', kimsingi wanaweza kusikiliza agizo la kiongozi wao la kukamata na kushtaki. Wana uwezo huo," aliiambia Sabahi.
Maagizo ya Kimaiyo yanakwenda kinyume na katiba ya nchi, kwa sababu sheria inawaruhusu maofisa polisi tu kupiga risasi kwa kujilinda, kwa mujibu wa Mratibu Mtendaji wa Kituo cha Kuhamasisha na Kulinda Haki Odhiambo Oyoko.
Hata hapo, polisi wanatarajiwa kupiga risasi na kulemaza, alisema, akiongeza kwamba agizo lililorekebishwa litafungua ukurasa mpya wa "mauaji rasmi ya kutumia nguvu".
Agizo linaonyesha kutokuwa na msimamo kwa jeshi la polisi kufanya mauaji, alisema Simiyu Werunga, kapteni mstaafu wa Jeshi la Kenya ambaye pia ni mkurugenzi wa Kituo cha Afrika cha Usalama na Mafunzo ya Kimkakati huko Nairobi.
"Kuna mengi katika ufanisi wa sera kuliko kuwaua tu washukiwa," alisema. "Serikali inapaswa kufanya utekelezaji sasa wa mabadiliko mengi ya polisi, ambalo pia linahitaji mabadiliko ya mtaala wa mafunzo katika vyuo vya mafunzo ya polisi."
Serikali inapaswa kuimarisha mikusanyiko ya kiintelijensia na mafunzo ya polisi, alisema, na maofisa wanapaswa kupewa motisha kwa malipo mazuri, vifaa vinavyofaa na kutambua mafanikio yao.
Maelekezo ya Kimaiyo yalizuia kushindwa kwa polisi kuandaa kesi ambazo zinaweza kushtakiwa, kwa mujibu wa Moses Omusula, mtaalamu wa usalama anayeishi Nairobi.
"Polisi wanaficha aibu zao kwa kushindwa kutoa ushahidi wa kuwatia hatiani kuwezesha mashtaka ya mahakama," Omusula aliiambia Sabahi. "Kuficah kuonekana kutokuwa na ufanisi kwao, wanaamua kuwaua washukiwa."
"Maagizo kama hayo kabla yameshindwa katika kushughulikia vurugu," Omusula alisema. "Maofisa polisi wazembe watakuwa wakitekeleza agizo na badala yake watapiga risasi badala ya kuwakamata na kutoa ushahidi kwa washtakiwa."

Kimaiyo: 'Wahalifu hawakutuachia chaguzi nyengine'

Lakini Katibu wa Baraza la Mawaziri Joseph ole Lenku aliunga mkono maelekezo ya Kimaiyo na kusema kwamba polisi watafuata sheria.
"Hakuna kitu kama mauaji nje ya mahakama," alisema mwezi Septemba wakati inspekta wa polisi alipotangazo agizo hilo. "Tuna wajibu wa kuilinda nchi. Polisi hawatakamata maguruneti kwa mikono yao na kuwapeleka gerezani kwa kisingizio cha kuzuia mauaji nje ya mahakama. Tutahakikisha kuwa wahalifu wenye silaha wanashughulikiwa kama wahalifu wenye silaha."
Kimaiyo pia alitetea maelekezo yake kwa kuonesha ongezeko la vurugu taifa zima kutoka kwa magengi ya wahalifu waliojipanga, wanamgambo wa kikabila na vikundi vya kigaidi.
"Amr hiyo haina uhusiano hata kidogo na mashtaka kwa sababu tunaheshimu mahakama, kwa sababu inatoa haki pale inapohitajika," aliiambia Sabahi.
"Tumekuwa tukiwashughulikia wahalifu kwa glavu za kitoto kwa muda mrefu," Kimaiyo alisema. "Tumefikiria chaguo za aina zote, ikiwa ni pamoja na kutoa msamaha kwa wahalifu, magaidi na wanamgambo wa kikabila ili waachane na vurugu, lakini ni machache sana yametiliwa maanani."
"NI uchaguzi mgumu lakini wahalifu hawakutuachia chaguzi nyengine," alisema.chanzo Sabahi online.

No comments:

Post a Comment