HATIMAYE binti anayedaiwa kubakwa na Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), amefungua jalada Polisi dhidi ya mbunge huyo.
Habari za kipolisi ambazo Tanzania Dama limezipata, zinasema kuwa binti
huyo ambaye anadai kubakwa na kisha kutishiwa kuuawa na Profesa Kapuya,
amefungua jalada namba OB/RB/21124/13 katika Kituo cha Polisi
Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Harakati za kufungua jalada hilo zilianza juzi jioni na kuendelea
hadi jana ambapo polisi walitumia zaidi ya saa 12 kumhoji binti huyo
anayedaiwa kubakwa ili kupata ukweli wa sakata hilo.
Akiwa kituoni hapo, binti huyo alikutana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya
Kipolisi ya Oysterbay (OCD) na OC-CID wake na kutoa maelezo ya awali
kabla ya viongozi hao kumruhusu ayaweke malalamiko yake katika maandishi
kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alikiri
polisi kufungua jalada hilo na kuongeza kwamba hivi sasa wanafanya
uchunguzi kubaini kama ujumbe ulio katika simu ya binti anayedai kubakwa
na kutishiwa maisha unatoka katika simu ya mbunge huyo.
“Tumefungua jalada, lipo kwa ajili ya uchunguzi na tukibaini kuwa ni
nani anahusika na tuhuma hizo tutamsaka na kumkamata popote alipo,”
alisema Wambura.
Habari zaidi zinasema polisi wamechukua namba ya Kapuya inayodaiwa
kutumika mara kwa mara kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa binti huyo,
akitishiwa kuuawa.
Simu hiyo namba 0784993930 inayodaiwa kumilikiwa na Profesa Kapuya,
mbali ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno ya kutishia kuua, pia ndiyo
inayodaiwa kutumika kutuma pesa kwa njia ya mtandao kwenda kwa binti
huyo.
Moja ya ujumbe wa vitisho unaodaiwa kutumwa na Kapuya kupitia simu
hiyo unasomeka hivi; “Mkiuawa itakuwa vizuri…itawapunguzia gharama za
kuishi, usitake kugombana na serikali mtoto mdogo kama wewe, sisi ndiyo
wenye nchi yetu, mwenye hilo gazeti ni Mbowe sasa mwambieni nyumba ya
kuishi si mmemuingizia hela leo? Mnatumika tu bure watu wanaingiza hela
nyingi, ila mmenitibua lazima niwaue wiki hii haitaisha, nitapiga kambi
kote, jana si wamekuficha tuone utalindwa milele maana washatengeneza
hela, lazima mvae sanda tu hilo sio ombi ni wajibu wenu, mnajitia na
nyie mafia watoto siyo, watoto wetu wanauza unga nani anawakamata? Nani
atapingana nasi.”
Pia simu hiyo iliwahi kutuma ujumbe mfupi wa maneno unaosomeka hivi;
“Ni lazima nitakuua wewe na ndugu yako na atakaetaka kuwasaidia, huyo
Sitta asijiingize kwenu, yaani nitakuua tena sijui leo mtalala wapi? We
unadhani nani atakaenifunga, ndo nishakupa ukimwi, sasa nakutaka uache
mara moja kuongea na mtu, nitakuwinda popote tuone.”
Mbali na kutishia kumuua binti huyo na ndugu yake na mtu mwingine
yeyote atakayejitokeza kumsaidia, Tanzania Daima limenasa baadhi ya
mawasilino ya simu za ujumbe mfupi wa kuhamisha fedha kutoka kwa Profesa
Kapuya kwenda kwa binti huyo ambaye mbunge huyo alikana kumfahamu na
kwamba hajawahi kukutana naye.
Tanzania Daima pia lilinasa mawasiliano ya kutumiana fedha kutoka kwa Kapuya kwenda kwa binti huyo.
Baadhi ya mawasiliano hayo ni pamoja na yale yaliyofanyika Agosti 31
mwaka huu kupitia simu ya Kapuya ambapo alituma sh 300,000 kwenda kwa
binti huyo kama sehemu ya makubaliano ya kutuma pesa kila mwezi kwa
ajili ya matunzo.
Mawasiliano hayo ni kama ifuatavyo: U26UG365 Imethibitishwa Umepokea
Tsh 300,000 kutoka kwa JUMA KAPUYA Tarehe 31/8/13 saa 3:28 PM Salio lako
la M-PESA ni Tsh 300,000
V04EU470 Imethibitishwa Umepokea Tsh 400,000 kutoka kwa JUMA KAPUYA
Tarehe 24/9/13 saa 2:38 PM Salio lako la M-PESA ni Tsh 400,040.
R93NY448 Imethibitishwa Umepokea Tsh 505,000 kutoka kwa JUMA KAPUYA
Tarehe 21/6/13 saa 11:07 AM Salio lako la M-PESA ni Tsh 505,000.
Kutokana na mfululizo wa habari hiyo, Profesa Kapuya kupitia kwa wakili wake Yasin Memba,
ametishia kuliburuza mahakamani Tanzania Daima endapo halitamwomba msamaha ndani ya
siku saba.
Source: Tanzania Daima
Source: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment