Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, November 17, 2013

HATARI: WATU WAUZA DAMU ZAO MITAANI



 Damu salama ikiwa imehifadhiwa kwenye mfuko maalumu wa kutunzi damu. Picha na Maktaba  

Dar es Salaam na mikoani. Wakati Serikali ikisisitiza kuwa huduma ya kumwongezea mgonjwa damu hospitalini ni bure, imebainika kwamba baadhi ya watu mitaani wakiwamo wabeba mizigo sokoni wanauza damu zao kwa watu wanaohitaji.
Mbali ya watu kuuza damu zao, majimaji hayo mekundu muhimu mwilini yamegeuka bidhaa adimu baada ya baadhi ya wauguzi na madaktari nao kugeuza huduma hiyo kuwa kitegauchumi chao.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ni kosa kwa mtumishi yeyote wa afya nchini kumuuzia mgonjwa damu na wala hakuna biashara ya kuuza damu kwa kuwa hutolewa bure na watu wanachangia kwa hiari.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili katika hospitali mbalimbali nchini, umebaini hospitali nyingi hazina damu za kutosha na hivyo kusababisha baadhi ya wagonjwa kuwalipa watu mitaani, ili kuwatolea damu au kuinunua kwa wauguzi na madakari.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema kuwa wahudumu wa afya wanaoendesha vitendo hivyo ni watu wanaojaribu kuizidi maarifa Serikali na kwamba wananchi wamepewa taarifa za kutosha kuwa damu haiuzwi.
“Kuna watu wanajaribu kutuzidi maarifa, hiyo ni tabia inayopaswa kupigwa vita. Mtu yeyote atakayetakiwa kununua damu, atoe taarifa kwa mganga mkuu au kituo chochote cha polisi,” alisema.

Mkoani Dodoma
Wabeba mizigo wa soko la Majengo Mjini Dodoma, wamekuwa mkombozi kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali ya mkoa huo baada ya kugeuza miili yao kuwa sehemu ya kuvuna damu na kuiuza kwa ndugu wa wagonjwa hao.
Gharama za kuuza damu hiyo ni kati ya Sh10,000 hadi Sh30,000 kwa chupa moja, kutegemea na uwezo wa ndugu wa mgonjwa huyo, lakini baadhi wamekuwa wakitoa zaidi kama sehemu ya shukurani.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuthibitishwa na baadhi ya wabeba mizigo hao, imebainika kuwa kitendo cha kutoa damu kwa wabeba mizigo ni cha kawaida na kwamba utaratibu huo ulianza muda mrefu.
Enock Ayub ambaye ni mmoja wa watu ambao wamechangia damu zaidi ya mara tatu kwa nyakati tofauti, alilimbia gazeti hili kuwa biashara ya kutoa damu anaipenda na kwamba inampa matumaini ya kuishi kwa kuamini kuwa bado ni mzima.
“Mimi nimechangia damu zaidi ya mara tatu, lakini tukifika kule tunabadilisha majina maana madaktari wanataka mtu ukae muda za miezi sita bila ya kutoa, sisi tunataka fedha ‘mkwanja’, hatuna jinsi,” alisema Ayubu na kuongeza:

“Hata hivyo, napenda kutoa damu kwani ukiona wanakutoa ujue afya yako ni nzuri na huna Ukimwi na magonjwa mengine.”
Alipoelezwa hatari za kutoa damu mara kwa mara bila kuzingatia ushauri wa daktari alisema, “Sioni tatizo maana fedha tunazolipwa tunazitumia kunywa bia na matunda, hivyo afya zetu hurejea kama kawaida, tena baada ya muda mfupi.”
Baadhi ya wodi ambazo gazeti hili lilitembelea na kuzungumza na baadhi ya wagonjwa, lilibaini kuwa tatizo la damu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma limekuwa sugu, huku ndugu wa wagonjwa wakilalamika kuwa wanauziwa damu kwa bei ya kati ya Sh40,000 hadi 60,000 kwa chupa moja.
“Mimi sitaki uniandike jina langu gazetini, lakini ukweli ni kuwa madaktari walimpokea mgonjwa vizuri na damu aliwekewa haraka sana tatizo likaja kwenye kuirudisha niliambiwa nitoe Sh60,000 au mimi nitolewe damu, nilipogoma nikaonyeshwa Soko la Majengo kwa wabeba mizigo,” anasema ndugu huyo.
Anasema kuwa alipofika kwa wabeba mizigo walimuuliza daraja la damu aliyotoa na alipowatajia walijitokeza wawili wenye daraja hilo wakaanza kupatana bei kabla ya kukubaliana na mmojawao kwa kiasi cha Sh 25,000.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Dk Nasoro Mzee, alikiri tatizo la damu ni kubwa katika hospitali hiyo na kwamba linatokana na mwitikio mdogo wa wananchi katika kuchangia katika benki ya damu.
Dk Mzee alisema hadi sasa kitengo hicho kina upungufu wa damu na kwamba ni wanafunzi na askari tu ndio wanaochangia damu kwa kiwango kikubwa.
“Wakifika watu ambao wana mahitaji ya haraka tunachukua damu na kuwawekea, wengine ni kweli tunawaambia wachangiwe na ndugu zao, na kwa wale waoga kutoa huwa wanakwenda kutafuta kwa wanaojitolea kutoa damu,” alisema Mzee.
Alifafanua kuwa siyo kila damu inayotoka kwa mtu inakuwa salama kutumika, ni lazima ipimwe.

Songea wanauza damu Sh 50,000
Wabeba mizigo katika Manispaa ya Songea wamekuwa wakichangia damu kwa wagonjwa wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji au kuongezewa damu, bei yao ni Sh50,000 kwa chupa ya ujazo wa lita moja. Baadhi ya wauguzi pia wanadaiwa kujihusisha na biashara hiyo kwa bei ya maelewano kati yao na mgonjwa au muuguzaji.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wabeba mizigo wa manispaa hiyo, Adrian Mbawala amesema biashara hiyo ameifanya kuanzia mwaka 2006.


Anasema wamekuwa wakipata wateja mbalimbali, wengi wakiwa ni wajawazito pamoja na wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji na waliopata ajali.
“Wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji au waliopata ajali tunawatoza kati ya Sh20,000 hadi 50,000 kwa lita moja, ila bei hiyo inategemea na mahitaji ya mteja na uwezo wake kifedha” alisema.
Anasema licha ya kuwa biashara hiyo kuwa ya siri, wao sio wanaotafuta wateja bali wateja ndio wanaowatafuta kwa lengo la kutaka kuuziwa damu ili waweze kuwasaidia ndugu zao, “Ndugu wengi ni waoga wa kutoa damu ndiyo maana wanatutafuta sisi.”
Mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo ya mkoa (jina linahifadhiwa) amesema yeye binafisi hajawahi kufanya biashara hiyo ya kuwauzia wagonjwa damu, ila amewahi kusikia baadhi ya wagonjwa wakilalamikia kuuziwa damu na wauguzi na alipowahoji zaidi walidai kuuziwa damu hiyo kwa Sh10,000kwa lita moja.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedicto Ngaiza amesema taarifa hizo siyo sahihi na hazina ukweli wowote huku akisisitiza kuwa zinaenezwa na watu aliowaita wazushi.
“Hakuna mgonjwa anayeuziwa damu, wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu huwa tunawaeleza ndugu zao kwa ajili ya kuwachangia,” alisema Dk Ngaiza na kuongeza;
“Wanatakiwa kuchangia damu katika Kitengo cha Damu Salama, cha kushangaza baadhi yao wanatafuta watu wa kuwapatia damu na kuwalipa fedha. Wanapokuja nao hapa hospitali wanawatambulisha kama ndugu zao, hivyo hospitali sidhani kama inahusika katika hili.”

Mkoani Morogoro
Mkazi mmoja wa Morogoro aliyejitambulisha kwa jina moja la Msuya alisema kuwa baada ya kuelezwa na uongozi wa hospitali ya mkoa huo kwamba ndugu yake anatakiwa kuongezewa damu chupa mbili, aliishiwa nguvu na kujiuliza ataipata wapi damu.
“Ndugu yangu amelazwa wodi namba tisa, wamesema ana upungufu wa damu, hospitali imesema itatoa chupa moja na sisi ndugu tuchangie chupa moja, nilielezwa na mtu mmoja kuwa kama ndugu hawatakuwa tayari wapo vijana wanaouza damu kwa Sh25,000 hadi 30,000” alisema Msuya.

Mkoa wa Arusha
Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, imefanikiwa kupunguza tatizo la kuuzwa damu kwa wagonjwa kutokana na kuwashirikisha wadau mbalimbali kutoa elimu ya kupinga biashara hiyo, ikiwepo Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Dk Josia Mlay akizungumza na gazeti hili alisema kwa sasa hospitali hiyo, licha ya kupata damu asilimia 35 ya mahitaji kutoka benki ya damu, imeweka matangazo katika wodi zote kuwa damu ni bure.
“Watu wengi hawapendi kutoa damu ila pale wanapoombwa kusaidia wagonjwa wao wanaomba kuuziwa jambo ambalo ni vigumu kulibaini na hata kama ukiwa na taarifa, waliouziwa hawasemi” alisema Dk Mlay.
Dk Mlay alisema kama watu wakiwa na tabia ya kujitolea damu ni wazi tatizo la damu kuuzwa litakwisha, kwani hata wafanyakazi wengi wanajua wakibainika kuwa wanauza damu watachukuliwa hatua.
Baadhi ya wagonjwa katika hospitali hiyo walisema, “Ndugu hawatoi damu na hospitali wanasema hakuna damu ya kutosha sasa unadhani utafanya nini, usipopata damu unakufa.”

Jijini Dar es Salaam
Jane Lyimo ni mkazi wa Jiji la Dar es Salaam na siku za hivi karibuni alikuwa akimuuguza dada yake aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke, “Dada yangu ana tatizo la kupungukiwa damu, awali sikufahamu kama damu inauzwa hadi pale nilipotakiwa kutoa fedha kwa ajili ya kulipia huduma hiyo.”
Anasema Septemba mwaka huu, dada yake aliwekewa chupa mbili za damu lakini siku tatu baadaye wakati wakijiandaa kutoka katika hospitali hiyo, muuguzi aliyekuwa akimhudumia dada yake alimtaka kulipia Sh25,000 ili kununua damu nyingine, kufidia ile aliyowekewa dada yake.
“Muuguzi alisema tunatakiwa kununua damu aina yoyote (group lolote) ili ikawekwe kama akiba. Alitueleza kuwa kuna mtu yupo katika hospitali hiyo kazi yake kubwa ni kujitolea damu na kama tukitoa kiasi hicho cha fedha anaweza kutusaidia,” alifafanua.
Alisema baada ya kutoa Sh20,000 muuguzi huyo aliondoka na aliporejea aliwaeleza kuwa tayari damu hiyo imepatikana.
Katika Hospitali ya Mwananyamala Wilaya ya Kinondoni mwandishi alikutana na Rachel Mhagama, kueleza kuwa amewahi kununua damu mara kadhaa wakati akiwauguza ndugu zake.
Akisimulia zaidi Mhagama, alisema kwamba kaka yake, ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa akihitaji kuongezewa damu, na walipomweleza mhudumu alionekana kutokuwa na habari na mgonjwa wao, kuongeza kuwa baadaye mtu mmoja aliwaeleza kuwa wanatakiwa kutoa fedha ili mgonjwa wao aweze kuongezewa damu.
“Shemeji yangu alimwita muuguzi pembeni na kumwingizia Sh13,000 mfukoni, tena ndiyo fedha pekee aliyokuwa amebakiwa nayo. Baada ya hapo huduma zilianza kutolewa mbio mbio,” alisema.

Naye Hamida Yusufu, mkazi wa Mwananyamala, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na upungufu wa damu alisema kuwa siku moja aliambiwa atoe fedha za kununulia damu baada ya kuelezwa kuwa damu iliyokuwapo ilikuwa kundi tofauti na lake.
“Tuliambiwa tutoe fedha ili apatikane mtu mwenye damu kundi moja na mimi. Ndugu zangu walitoa Sh10,000. Kitu ambacho kilitushangaza, baada ya muda mfupi nililetewa damu na nikawekewa,” alisema.
Katika hali isiyo ya kawaida mgonjwa mmoja katika Hospitali ya Temeke, Hamida Hussein alisimulia namna mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo alivyotaka kumwekea damu kundi tofauti na lake.
Alisema aliandikiwa chupa tatu za damu, kwamba wakati wakati muuguzi akimwekea chupa ya pili, alikosea badala ya kumwekea damu kundi O alimtundikia kundi B.
“Wakati alikuwa akijiandaa kunitundikia chupa ya pili, nilishangaa kuona juu ya chupa hiyo imeandikwa ‘group B’, nikamuuliza kwa nini wameamua kunibadilishia damu. Aliniangalia kisha akasoma kwenye faili langu, halafu akaiondoa na kunitundikia nyingine,” alisema.
Kwa mujibu wa Hamida, muuguzi huyo alimjibu: “Hata kama usingeona ungeshtuka wakati damu inaingia mwilini, ungehisi hali ya tofauti.”
Ofisa Uhusiano na Masoko wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Rajabu Mwenda alisema vitendo vya uuzaji damu vinavyofanywa na wahudumu wa afya wasio waaminifu, vinarudisha nyuma jitihada za taifa za kukusanya damu ya kutosha.
“Vitendo hivyo vinatuharibia taswira yetu, hebu fikiria unamwomba mtu aje kujitolea damu bure halafu kesho ndugu yake akiumwa anaambiwa anunue damu,” alisema.
Mwenda alisema watumishi hao wanatumia uhaba wa damu uliopo nchini kufanya biashara na kuwataka wanaowafahamu wanaoendesha vitendo hivyo kuwataja ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa mwaka unakusanya asimilia 34 pekee ya damu inaohitajika nchi nzima.

Muuguzi atoa ushuhuda
Muuguzi mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama, alilisimulia Mwananchi Jumapili namna wahudumu wa afya kwenye hospitali wanavyowauzia damu wagonjwa.


Muuguzi huyo, ambaye kwa sasa anafanya kazi katika zahanati moja wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, alisema kuwa ili kupata damu kwa urahisi kutoka kwenye benki za damu hospitalini ni pamoja na kusema kuna mgonjwa ameokotwa na wasamaria wema na anahitaji damu haraka.
“Tulikuwa tukipewa ile damu tunawauzia watu wenye fedha wanaotaka wagonjwa wao wahudumiwe haraka,” alibainisha na kuongeza kuwa ingawa kila mhudumu wa afya anajua kufanya hivyo ni kosa. Hiyo ilikuwa njia ya kupata fedha za ziada nje ya mshahara kirahisi.

MAT wazungumza
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia alisema kuwa biashara ya kuuza damu inachochewa na tabia ya baadhi ya watu wanaoogopa kupima damu ili wawaongezee damu ndugu zao, ambao badala yake hutumia fedha kuwashawishi madaktari na wauguzi wawauzie damu hiyo.
“Inafahamika kuwa benki ya damu ya taifa haina damu ya kutosha, lakini pamoja na hivyo watu wanaotakiwa kupima ili wawatolee damu ndugu zao wanaogopa. Badala yake wanatumia fedha kuwahonga madaktari ili waipate kwa njia nyingine,” alisema.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment