Hivi karibuni, Mwenyekiti wa CCM alikemea vitendo vya rushwa ndani ya chama na kuonya kuwa vinaweza kukiangusha.
Dodoma. Wahenga walinena, ‘mficha maradhi kifo kitamuumbua’.
Ni hivi karibuni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Rais Jakaya Kikwete aliweka bayana mbele ya hadhara jinsi chama
hicho kinavyotafunwa na mdudu rushwa.
Watendaji wa CCM na viongozi wao walikukuwa
wamekusanyika mjini Dodoma katika mafunzo ya kuandaa ‘jeshi imara’
litakalokivusha chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 na
Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Katika mazungumzo yake, mwenyekiti aliwatwisha mzigo mzito kuwa ‘chama chao kikianguka kutokana na rushwa, wa kulaumiwa ni wao’.
Mbali na hilo, kiongozi huyo alianza kwa
kuwashushua viongozi hao kuwa wengi hawajui wajibu wao, badala yake
wamekuwa na kazi ya kuimba ‘iyena iyena, wembe ni ule ule ushindi’
wakati wembe unageuka na kuwakata wao.
Katika mkutano huo uliojumuisha wajumbe 426 kutoka
makundi ya wenyeviti na makatibu wa wilaya na mikoa, Rais Kikwete
alitumia saa 2:04 kuzungumzia hatari anayoiona kwenye chama hicho.
Sehemu kubwa ya hotuba Kikwete ilijaa hadhari,
huku akisimamia ukweli wa hali halisi ilivyo ndani ya chama na wajumbe
walio wengi walionekana kukubaliana na mawazo yake.
Usugu wa rushwa
Rais Kikwete ametumia muda mrefu kuzungumzia suala
la rushwa ambayo anasema limekuwa ni donda ndugu lisilotibika na
linaelekea kuigharimu CCM kwa siku za usoni.
“Tatizo la rushwa ndani ya chama lipo na lazima
tukubali kwamba lipo. Hili nalisema, kwamba tusipokubali ukweli huu
chama chetu hakitadumu kwa muda mrefu madarakani, wenzetu watachukua
nchi,” anasema.
Inaonekana rais ana taarifa zote, kama
anavyothibitisha: “Rushwa imejichimbia mizizi kuanzia ngazi za chini,
mimi najua kuwa watu wanapewa Airtime (muda wa maongezi) hadi ya
shilingi laki mbili na zinatembea kwenye mitandao na iko siku nitakuja
kuwasoma wengine hapa, maana najua.”
Nini madhara yake? Anawakumbusha watendaji hao wasibweteke akisema kipo chama mbadala ambacho wananchi wanaweza kujiunga nacho.
Kuwatosa wenye madoa
Katika mkutano huo Kikwete pia anazungumzia
wagombea ‘wenye madoa’ ndani ya chama akisema hawafai na kwamba lazima
watoswe kwa ngazi zote kabla ya kuanza kwa safari ya mwaka 2014 na 2015.
Anabainisha kuwa kuna wanachama ambao wamekuwa na
madoa kwa chama na jamii, lakini baadhi ya viongozi wameendelea
kuwakumbatia. Wanashindwa kuwaacha kwa sababu wanaendelea kuneemeka
kutoka kwao.
Anaagiza watu wa namna hiyo waachwe mara moja na
nafasi zao zichukuliwe na vijana wasomi kutoka vyuo vikuu ambao
wanaiunga mkono CCM.
Wakuu wa wilaya, mikoa
Kwa upande mwingine anaonyesha namna ambavyo wakuu
wa wilaya wanashindwa kukisaidia chama wakati wakiwa makada wa CCM na
hivyo kusababisha kilaumiwe. Mmoja wa washiriki, Katibu wa CCM Wilaya ya
Makete, Njombe, Miraji Mtaturu anakiri kuwa jambo lililozungumzwa na
kiongozi huyo ni la kweli, kweli rushwa ipo ndani ya chama.
Mtaturu anasema wapo viongozi wengi ambao wamekuwa wakitafuta mafanikio ya haraka na kusahau maadili ya chama.
Ndejembi apongeza
Kada wa siku nyingi wa CCM, Pankras Ndejembi anapongeza kauli ya Rais Kikwete kuwa imekuja kwa wakati wake.
Ndejembi aliwahi kuwa mwenyekiti wa CCM na
mwenyekiti wa wenyeviti wa mikoa, anaungana na Rais Kikwete kuhusu
kukithiri kwa rushwa ndani ya CCM, lakini anapingana na kumkabidhi
jukumu hilo Mangula hadharani. Anasema rushwa ndani ya CCM ‘imeingia
hadi katika milango ya dhahabu’ ambayo kuitoa kwake inakuwa ni ngumu
sana, hivyo inahitaji nguvu ya ziada na ya pamoja.
Anasema kuwa uongozi wa CCM ulitoa nafasi kubwa
kwa ‘watu wa rushwa’ na kuwafanya kuchimbia mizizi yao chini, kitu
ambacho ni tofauti na enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere ambaye
alikuwa akiagiza jambo analifuatilia na kuona mwisho wa utekelezaji
wake.
CHANZO MWANANCHI
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment