Mzee Steven
Francis (50) kulia, mke wake Yustina Kasian (40) aliyembeba mtoto
James James Peter na Eliza Steven (19) wakizuru kaburi la
marehemu Hellan Petri Mahunzila (75) aliyeuawawa kisha mwili wake
kuchunwa ngozi hivi karibuni halmashauri ya wilaya ya Morogoro.PICHA NA MTANDA BLOG
Diwani wa kata ya Bwakilajuu, Emili Kidevu kulia akifafanua jambo mbele ya viongozi wa serikali ya kijiji cha Mgata na kitongji cha Gongo katika eneo la Mondo ambalo ndipo marehemu, Hellan Petri Mahunzila (75) ulitupwa mwili wake baada ya kuuawawa kisha kuchunwa ngozi katika mauaji ya kutatanisha hivi karibuni halmashauri ya wilaya ya Morogoro.
Eneo hili ndilo linalodaiwa mwili ulitupwa.
Mtanda Blog.
TUKIO
la kifo cha kikongwe, Hellan Petri Mahunzila (75) ambaye alipotea
katika mazingira ya kutatanisha kwa siku 12 kisha siku ya 13 mwili wake
kuonekana kando ya shamba lake huku maiti yake ikiwa imechunwa ngozi
mwili mzima, imezua hofu kubwa na kukubikwa na usiri wa mauaji hayo huku
wakazi wa kitongoji cha Gongo kijiji cha Mgata kata ya Bwakilajuu
mkoani Morogoro wakiishi kama mnyama digidigi ambaye amekuwa akiwindwa
na binadamu kwa ajili ya kitoweo.
Wakazi
hao wamekubwa na hofu hiyo wakihofia maisha yao na kulazimika haja
ndogo na kubwa kujisaidia katika makopo hasa nyakati za usiku ndani ya
nyumba zao na asubuhi kumwaga kinyeshi na mkojo na kubadilisha kabisa
mfumo wa kutembea, kulala na kulazimu kila kaya kuingia ndani ya nyumba
kuanzia majira ya saa 12 hadi saa 12:30 jioni kuepuka mtego wa kutekwa.
Ni
majira ya saa 7 usiku, siku ya jumatano kuamkia alhamisi ya oktoba 2
mwaka huu, Eliza Steven (19) anaamka na kumnyonyesha kichanga chake,
James Peter (miezi mitatu) baada ya kilio cha kichanga hicho kilichokuwa
kinahitaji huduma ya kunyonya kutoka kwa mama yake ndicho chanzo cha
kubainika kwa kupotea kwa marehemu Hellan Petri Mahunzila.
Baada
ya James kunyonya na kushiba kichanga hicho kilinyamaza kulia na kumpa
fursa ya mama yake kutoka ndani ili aende nje kwa ajili ya kujisaidia
haja ndogo, anafungua mlango wa chumba chake na kutoka nje kujisaidia
huku akipiga jicho na kuangalia mlango wa chumba anacholala bibi yake
anaona mlango upo wazi.
Jambo
hilo la kukuta mlango wa bibi yake kukuta ukiwa upo wazi hakulitilia
mashaka kwani alikuwa na imani angeweza kukutana naye nje ama chooni
lakini haikuwa hivyo bali akawa na imani tena pakuwa hakuweza hakuonana
naye nje wala chooni aliingia ndani na kwenda moja kwa moja hadi katika
chumba anacholala bibi yake na kuingia ndani.
Alipoingia
katika chumbani chake aliangalia kitandani ili kuweza kujijibu maswali
yake yasiyojaa kichwani likiwemo la kwanini bibi yake ameshindwa kufunga
mlango kama alitoka nje ? anaanza kusema alisema Eliza.
Eliza
aliendelea kueleza kuwa baada ya kuchunguza katika chumba kile
kinachotumiwa na bibi yake, Hellen ambaye alikuwa na kawaida ya kufunga
pindi aiingiapo kulala hakumwona na kuchukua jukumu la kumwamsha mama
yake mzazi, Yustina Kasian (40) ili aweze kusaidiana naye kumtafuta.
“Niligonga
mlango wa chumba alicholala mama na baba na nilimwita mama na alipotoka
ukumbini usiku ule nilimweleza kuwa mlango wa chumba cha bibi upo wazi
lakini hata na ule mlango mkubwa nao pia nimeukuta umeegeshwa tu na
nimeenda chooni pengine yupo kule lakini hayupo”. Alisema Eliza ambaye
ni mjuu wa bibi huyo.
Yustina
Kasian ambaye ni mtoto wa pili kwa kuzaliwa kwa bibi, Hellen Petri
Mahunzila alisema kuwa baada ya kuelezwa maneno yale na mtoto wake,
Eliza Steven ambaye ni bibi yake alienda katika kile chumba anacholala
mama yake na kuangali huku na huku lakini naye hakuweza kuona dalili ya
uwepo wa mtu katika kitanda, uvungu na eneo la chumba kwa ujumla na
kwenda moja kwa moja chooni ili akamwangalie huko pengine alikuwa huko.
“Nilienda
chooni na kuangalia ndani ya chooni lakini sikumwona na badala yake
nilirudi ndani na kumwamsha mume wangu, Steven Francis (50) ili naye
aweze kutusaidia kumfuata kwani tayari hofu ilianza kutanda moyoni mwetu
na kujiuliza maswali ambayo hatuweza kupata majibu kwa usiku ule”.
Alisema Yustina.
Mimi
baada ya kuelezwa jambo hilo na mke wangu nilitoka nje na tochi hadi
chooni na kumulika ndani na kuzunguka kile choo sikuweza kumwona na
kuhamishia kufanya zoezi hilo kwa kuzunguka nyumba, banda la kupikia
chakula na eneo zima la migomba lakini mama mkwe wangu hakuweza
kuonekana akiwa hai ama amekufa. Alisema Steven Francis ambaye ndiye
mwenye kaya hiyo yenye familia ya watu sita.
Francis
alisema kuwa zoezi hilo la kumsaka lilifanya kwa umbali wa mita 100
kutoka eneo la nyumba kwa usiku huo huku mvua kubwa ikinyesha na giza
nene limetanda akishirikiana na familia yake lakini hakukuwa na
mafanikio na kuchukua jukumu la kuomba msaada wa jirani ambapo alienda
kwa Selis Silili na Calist Stephano ili wasaidie mchango wa kimawazo na
kusamkasa mama mkwe wake.
Jirani
zake hao walitoa wazo la kwenda kutoa taarifa la tukio hilo kwa
Mwenyekiti wa kitongoji cha Gongo kijiji cha Mgata kata ya Bwakilajuu,
Festo Mfaume usiku ule wa majira ya saa 7:45 ambapo mwenyekiti huyo
aliwaeleza kuwa kutokana na giza nene na mvua zoezi hilo litafaa
kufanywa asubuhi yake siku ya alhamisi. Alisema Francis.
Mwenyekiti
huyo wa kitongoji cha Gongo, Festo Mfaume alisema kuwa ilikuwa siku wa
jumatano ya oktoba 2 majira ya saa 7:45 kuamkia alhamisi oktoba 3 mwaka
huu aliamshwa na Steven Francis, Selis Silili na Calist Stephano na
kuelezwa juu ya tukio la kupotea kwa bibi Hellen Petri Mahunzila kupotea
katika mazingira ya kutatanisha.
“Ni
kweli usiku wa oktoba 2 siku ya jumatano kuamkia alhamisi ya oktba 3
majira ya saa 7:45 niligongewa mlango na nilipotoka nje niliwaona mama
mkwe wa bibi Hellena (Steven Francis), Selis Silili na Calist Stephano
na kunieleza juu ya kupotea kwa bibi Hellen Petri Mahunzila (sasa ni
marehemu) nami niliwajibu kuwa pakuwa nanyi mmefanya juhudi za kumtafuta
bila mafanikio tuaghalishe zoezi hilo ili asubuhi mapema tuanze kazi ya
kuongeza nguvu ya kumsaka”. Alisema Mfaume.
Mfaume
alisema kuwa siku hiyo ya alhamisi oktoba 3 majira ya saa 11 alfajiri
alienda sehemu maalum ya mlima ambayo hutumika kutoa taarifa kwa kupaza
sauti yake na wakazi wa kitongozi hicho cha Gongo walikusanyika kwa
haraka katika nyumba ya, Steven Francis na muda mfupi wananchi hao
walijigawanya katika makundi na kuanza kazi ya kumsaka huku akifanya
jitihada za kuwajulisha viongozi wa kijiji cha Mgata akiwemo Mwenyekiti
na Mtendaji wake ambao nao waliungana na wananchi hao katika zoezi hilo
asabuhi ile.
“Kitongoji
changu kina zaidi ya wananchi 325 na tukio hili limekuwa la kwanza
kutokea na nilichofanya ni kuwatawanya watu katika makundi kuanza
kumtafuta bibi yetu Hellen sehemu za misitu, vichanga, shambani kwake,
mapango na kutoa taarifa vitongoji vya jirani ili nao watusaidie
kumtafuta, lakini tulifanya kazi hiyo kwa siku sita bila mafanikio na
kukata tamaa”. Alisema Mfaume.
Mfaume
alisema vitongoji vilivyoshiriki kumtafuta katika maeneo yao ni pamoja
na Dinila, Mituna na shuleni vilivyopo ndani ya kijiji cha Mgata, kazi
ya kumfuta kuanzia siku ya alhamisi oktoba 3 hadi 8 mwaka na ile usiku
ule aliotoweka nyumbani kwake lakini mwenyezi mungu ndiye aliyejua kiume
wake amepotelea.
Katika
ardhi ya kitongoji hicho hakuna sehemu ambayo wananchi wameshindwa
kufika lakini cha ajabu baada ya wao kukata tamaa kwa kumtafuta kwa siku
sita, mwili wake ulionwa na mjukuu wake, Eliza Steven siku ya tarehe 15
mwaka huu ikiwa ni siku saba mbele yake siku ya ijumaa saa 7 mchana
kando ya shamba lake ukiwa umechunwa ngozi na kutelekezwa baada ya
kutupwa na kuvingika umbali wa mita zaidi ya 50 tangu utupwe katika
mtelemko wa mlima. Alisema Mwenyekiti huyo wa kitongoji cha Gongo.
Siku
ya oktoba 15 majira ya saa 7 mchana mwaka huu, Eliza Steven aliondoka
nyumbani na chombo kwenda shambani kuchuma mbaazi kwa ajili ya mboga
katika shamba la bibi yake, mita chache kabla ya njia walioizowea
kuingilia shambani anaona nyasi zimelala na mburuzo kwa kitu jambo hilo
lilimstua kwa eneo hilo lilikuwa na kichanga vyenye mchanganyiko wa
miba.
“kabla
ya njia ya kuingilia shambani hatua chache tu niliona nyasi zimelala na
kama kuna kitu kilikuwa kimeburuzwa, nilistuka kidogo kwa sababu eneo
hilo la mburuzo kuna nyasi lakini na mibamiba hivi nami nikaona ngoja
nipite katika njia hiyo ya mburuzo huo nione mwisho wake”. Alisema
Eliza.
Katika
maelezo yake kwa mwandishi katika kitongoji hicho, Eliza alisema kuwa
alipita njia hiyo ili kuweza kujua mwisho wa mburuzo huo ambao alitembea
zaidi ya umbali wa hatua 18 za miguu akaanza kuona khanga na hatua
mbili mbele yake akaona tena kitenge vipo chini na aliponyanyua macho
mbele yake aliona mwili wa mtu.
“Nilitambua
zile nguo kuwa ni za bibi yangu Hellen aliyepotea siku 13 zilizopita na
niliposogelea zaidi ule mwili nilitambua kwa kuona ngua nyingine ambazo
alivalishwa likiwemo gauni, bangili, heleni na shanga shingoni lakini
mwili wake nilishangaa kuuona umekuwa mweupe hauna ngozi”. Alisema
Eliza.
Eliza
alisema kuwa baada ya kuona vile alipatapwa na mshtuko mkubwa huku moyo
ukimdunda kwa hofu kwa kuona tukio hilo ambalo kwake ni la ajabu na
kuamua kurudi kinyumenyume huku akimwita mama yake ambaye naye alienda
shambani huko akimpelekea mtoto wake ambaye alikuwa analia ili aweze
kumnyonyesha kwani sio mbali na shamba.
“Bibi
amekufa, kifo cha kikatili sana, ni tukio la ajabu na kusikitisha
sitaweza kusahau katika maisha yangu ya hapa duniani kwani kila aliyeona
ile maiti alishikwa na butwaa na kuangua kilio, nimewahi kuona maiti
wakati wa kuaga katika misiba ya majirani zetu na nimeona tofauti kubwa,
bibi ameuawawa kisha amechunwa ngozi mwili mzima”. Alisema Eliza kwa
huzuni.
Alienda
kwa mama yake aliyekuwa shambani ameanza kuchuma mbaazi huku
akimbembeleza James aliyekuwa analia na kumchukua mtoto wake na
kumnyonyesha kisha kumweleza kila kitu alichoona na baadaye mama yake
alifuata ule mburuzo hadi kwenye mwili wa marehemu yake naye
alipojiridhisha kuwa ndiye aliyekuwa akisakwa kwa udi na mavumba
aliangua kilio huku akielekea njiani. Anasema Yustin Casian.
Kilio
cha Yustin kilikusanya wakazi wa eneo hilo na kuanza kumiminika umati
wa watu kutoka katika kitongoji kile katika eneo la tukio na taarifa
kusambaa kila kona ya kijiji huku wengine wakijulishana jambo hilo kwa
njia ya simu za viganjani.
Mwenyekiti
wa kitongoji cha Gongo, Festo Mfaume anaeleza kuwa baada ya kuonekana
kwa mwili huo alifuatwa nyumbani kwake na kijana aliyefahamika kwa jina
la, Anthony Kalist na kumweleza kuwa bibi aliyepotea ameonakana kando ya
shamba lake lakini tayari amekufa.
Nilienda
eneo la tukio na nilipouna tu ule mwili nilibaini kuwa amechunwa ngozi
tena kwa utalaam wa hali ya juu kwani hakuna sehemu ya mwili wake ambayo
ngozi ilibakia si katika nywele wala katika vidole vya kucha hakukuwa
ngozi iliyobakia katika mwili wake. Alisema Mfaume.
Nilipiga
simu huku na kule kujulisha viongozi wenzangu kuanzia ngazi ya kijiji,
kata na wengine waliendelea hivyo hivyo lakini baada ya kumpigia Diwani
wa kata ya Bwakilajuu, Emili Kidevu majira ya saa 8 siku ile ya oktoba
15 yeye alinieleza kuwa watu wote wa kitongoji na kijiji cha Mgata
wasiondoke eneo la tukio hadi kesho yake ya oktoba 16 mwaka huu.
“Baada
ya mimi kujulishwa juu ya tukio lile na kuona mwili namna ulivyochunwa
ngozi mwili mzima nilienda ofisi ya Mtendaji na Mwenyekiti wa kijiji cha
Mgata kutoa taarifa pia nilimjulisha Diwani kwa njia ya simu naye
akatoa agizo la kuulinda mwili ule hadi siku ya pili wakati yeye
akifanya utaratibu wa kuwaleta askari polisi na daktari ili wachunguze
tukio hilo”. Alisema Mfaume.
Mfaume
alisema kuwa tukio hilo limekubikwa na utata mpaka wakati huu kutokana
na mazingira yake ya kupotea kisha kifo chake kimekuwa na usiri mkubwa,
na hata baada ya mwili wake kuonekana kando ya shamba lake bado kuna
jambo limejificha kwa raia wa kawaida inamuumiza kichwa zaidi ya
wahusika kufahamu nini wamekifanya na malengo yao.
“Mimi
baada ya kumjulisha Kidevu (Diwani kata ya Bwakilajuu) tukio la
kuonekana kwa marehemu huku mwili mzima ukiwa umechunwa ngozi yeye
alitoa amri kwangu kwa kunitaka nitoe taarifa kwa wakazi wote kuulinda
ule mwili kuanzani muda ule wa saa 7 mchana mpaka asubuhi siku ya pili
yake”. Alisema Mfaume.
Msafara wa
Daktari kituo cha afya Duthumi na askari wa kituo kidogo cha
Kisaki-Gomero na Mtendaji wa kata ya Bwakilajuu ukiongozwa na Diwani wa
kata ya Bwakilajuu, Emili Kidevu uliwasiri eneo la tukio majira ya saa
8:30 mchana siku ya jumatano oktoba 16 mwaka huu kwa ajili ya uchunguzi
mwili na kuchukua maelezo kwa upande wa familia ya karibu ya marehemu.
Msichana Yusta Ostach (15) mkazi
wa kitongoji hicho cha Gongo anasema kuwa yeye tukio hilo wakati
linatokea hakuwepo katika kitongoji hicho bali alikuwa safarini na
aliporejea siku tangu tukio kutokea alielezwa juu ya tukio hilo likiwemo
la watu wa kitongoji hicho kujisaidia haja ndogo na kubwa katika makopo
nyakati za usiku na muda wa kuingia ndani ni saa 12 ama 12:30 jioni.
Ostach
alisema kuwa hali hiyo imekuwa kero kwake kwa hasa kitendo cha
kujisaidia haja kubwa na ndogo katika chombo na suala la kuingia ndani
saa 12 au umezidisha kukaa nje basi iwe saa 12:30 jioni kuwa maisha hayo
yamekuwa hanaya tofauti na mnyama digidigi ama mtu aliye katika
kifunguni japo kunakuwa na tofauti ndogo.
“Nilipoelezwa
tukio la bibi Hellen kufariki dunia tena amechunwa ngozi niliingiwa na
uoga lakini nilikubaliana na ushauri wa wenzangu wa kutotoka nje nyakati
za usiku na kama nitakuwa nimebanwa na haja kubwa ama ndogo basi sina
budi kujisaidie katika mkopo na asubuhi nitamwaga sasa hali hiyo kwangu
imekuwa kero kwangu kwani sijazoea”. Alisema Yusta huku akiwa
ameinamisha kichwa chini.
Aliendelea
kusema msichana huyu kuwa licha ya kupewa onyo la kutotoka nje nyakati
za usiku, jambo lingine aliloelezwa na ndugu zake ni pamoja na
kuzingatia muda wa matembezi ukiwemo wa kurudi nyumbani kuwa ni lazima
uwe saa 11:30 ama saa 12:30 jioni awe tayari katika mazingira ya
nyumbani kwao.
Marehemu
Hellen Petri Mahunzila (75) ameacha watoto watatu wakiwemo wa kiume
wawili, Kassim Athmani Lingila (58), Banzi Mazangwa (55) na mwanamke
pekee, Yustina Kasian (40) na aliachana na mumwe wake miaka 10 iliyopita
huku historia yake ikielezwa kuwa maisha yake yote alijighulisha na
suala la kilimo.
Akieleza mkasa uliokumkuta mama yake kupotea hadi kifo chake cha mateso, Banzi Mazangwaalisema
kuwa mama yake alikuwa mpole na mkimya huku akieleza kuwa hakuwahi
kusikia kama amewahi kugombana na mtu yoyote siku za hivi karibuni na
alikuwa anafanya kazi ndogo ndogo za nyumbani kutokana na uzee wake.
Mazangwa
anasema kuwa mama yao siku za hivi karibuni nyakati za usiku alikuwa
anatoka sana nje kwa ajili ya kusaidia haja ndogo, lakini miaka mitatu
nyumba aliwahi kumweleza mama kwa kuwa yeye sasa umri aliokuwa nao ni
mkubwa inafaa awe anajisaidia haja ndogo na kubwa katika kopo hasa
nyakati za usiku wajuu zake watafanya kazi ya kumwaga asubuhi lakini
jambo hilo alikataa.
“Miaka
mitatu nyumba niliwahi kumweleza mama awe anajisaidia haja ndogo katika
kopo nyakati za usiku lakini alikataa na kunieleza kuwa bado ana nguvu
za kutembea mwenyewe hivyo haoni haja ya kufanya hivyo”. Alisema
Mazangwa.
Akielezea
kwa masikitiko tukio hilo la mauaji ya mama yake, Mazangwa alisema kuwa
ameshangwa na mauji hayo pamoja na ukatili uliofanywa huku mwili wake
ukiwa umechunwa ngozi na kutupwa shambani kwake baada ya kupotea kwa
siku 13 kabla maiti yake kuonekana kandao ya shamba lake.
“Eneo
ambalo mwili wake ulitupwa kando ya shamba lake, sisi familia tumefika
zaidi mara tatu ama nne na watu wengine walifanya hivyo lakini baadaye
wananchi katika zoezi la kumsaka kwa siku nane bila mafanikio, wananchi,
ndugu, jamaa na marafiki tumeshangazwa eti eneo hilo hilo ambalo watu
wamefika na hawajaona kitu, ndipo mwili wake umeonekana ?”. Alihoji
Mazangwa.
Kuna
siri kubwa imefichika katika tukio hilo na bila shaka baadhi ya wakazi
wa kijiji cha Mgata watakuwa wanahusika na hawawezi kukwepa kuhusika
kwao kwa namna moja ama nyingine katika mauaji hayo ya mama yake kwanini
tangu amepotea alikuwa wapi katika siku 13 zote ? kabla ya kifo chake
kama si kuhifadhiwa ndani ya nyumba za mmoja wa wakazi wa Mgata ?.
Aliendelea
kusema kuwa wauaji hao ni watu wanaowafahamu vizuri tu familia yao
kwani baada ya yeye kuona mwili wa mama yake ulionyesha kuwa amekufa
siku moja ama mbili zilizopita kabla ya kuchunwa ngozi na ilionekana ni
watu ambao wametumia utalaam wa hali ya juu kuweza kufanikiwa zoezi hilo
kupata ngozi ya mama yao.
Siku
ya jumatano oktoba 15 mwaka huu majira ya saa 8 mchana ndiyo mwili
ulionekana lakini ndugu, jamaa na wananchi wa kitongoji na kijiji Mgata
walilala eneo hilo usiku kucha wakiulinda wakati wakisubiri ujio wa
daktari, askari polisi na diwani kwa ajili ya uchunguzi lakini cha
kushangaza eneo hilo halikuwa na harufu yoyote kama binadamu aliyekufa
siku 13 zilizopita. Alisema Mazangwa.
Mazangwa
ametoa wito kwa jeshi la polisi kuchunguza tukio hilo kwa kina kwani
ana imani endapo watafanya hivyo watafanikiwa kuwabaini wahalifu ndani
ya kijiji hicho na wale ambao wameshirikiana nao katika mauaji hayo ili
hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa mkondo wake kwani wananchi
sasa hivi wanaishi kama wanyama wanaowindwa na binadamu kwa ajili ya
kitoweo.
Diwani wa kata ya Bwakilajuu, Emili Kidevu anasema
kuwa tangu kutokea tukio hilo hakuna uchunguzi wowote umefanyika kutoka
ndani ya jeshi la polisi zaidi ya kufika siku ya tukio.
Kidevu
alisema kuwa kijiji cha Mgata kimekuwa kikipokea wageni wengi ambao
wengi wao ni wafanyabiashara wanaoenda kijijini hapo kwa ajili ya
kununua zao la iriki hasa katika kipindi cha kuanzia mwezi tano hadi
wa nane na tukio hilo limetoka mwezi wa 10 jambo ambalo kwa upande wake
anatilia shaka na kujiuliza maswali yasiyo na majibu.
“Jambo
hili linavyoonekana halikufanywa na mtu mmoja na kama jeshi la polisi
lingefikilia kuweka mitengo katika barabara ya Dakawa-Bwakilajuu,
Mgata-Bwakilajuu kutumia askari wa polisi jamii wa vijiji husika nina
imani lazima wangeweza kunasa mfuko ya plastiki ama chombo chochote
ambacho wamehifadhi ngozi hiyo na kukamata wahalifu”. Alisema Kidevu.
Kidevu
aliendelea kutoa ufafanuzi kuwa mitego kama ingetegwa katika kijiji cha
Dakawa, Bwakilajuu na Mgata katika barabara ambazo ndizo zinazotumika
kuingia na kutoka baada ya kutokea.
Shaka
nyingine inayumkumba diwani huyu na jamii ya kitongoji cha Gongo,
kijiji cha Mgata na vijiji jirani ni namna tukio hilo lilivyotekelezwa
kiutalaamu bila kukosea, kwanza anaweza kusema kuwa marehemu alitekwa,
kisha akahifadhiwa ndani ya nyumba kwa siku 1o kabla ya kifo chake.
“Nina
imani kama jeshi la polisi likichunguza mauaji hayo wataweza kuwatia
nguvuni wahusika hasa kwa kuanzia katika kile kitongoji cha Gongo na
kijiji cha Mgata inanipa imani kabisa kulingana na mtirirko wa tukio
lenyewe, kwani haiwezekani apotee kwa siku 11 na siku ya 12 ndio mwili
wake uwe umeonekana tena umechunwa ngozi kilataalam ?. alihoji Diwani
huyu.
Naye
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile
akitolea ufafanuzi na kuthibitisha kutokea kwa tukio la marehemu, Hellen Petro (75) kufariki
dunia baada ya kupotea kwa siku 11 kisha mwili wake kukutwa umechunwa
ngozi siku ya 12 amelihusisha tukio hilo na masuala ya ushirikina.
Shilogile
alisema kuwa jeshi la polisi lipo katika uchunguzi wa kuwabaini wauaji
na watakapobainika sheria itafuata mkondo wa sheria ikiwemo kufikishwa
mahakamani.
“Hili
tukio jeshi la polisi mpaka sasa bado lipo katika uchunguzi, uchunguzi
upo wa aina nyingine hilo siwezi kulibainisha kwani itaharibu mitego
yetu ila ninachoweza kusema kuwa tunafanya uchunguzi si lazima pale
katika kitingiji aonekane askari la hasha”. Alisema Shilogile.
Akifafanua
zaidi juu ya uchunguzi wa tukio hilo Kamanda Shilogile aliongeza kwa
kusema mpaka sasa bado wanaendelea kukusanya taarifa mbalimbali na
nyingine kuzichuja ili kuweza kuwabaini wauaji na wakati mungine
uchunguzi unaweza kuchukua zaidi ya mwezi mmoja kabla ya wahusika
kunaswa.
Bado mpaka sasa hakuna
mtu aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo na kwamba baada ya kutokea
tukio aliagiza polisi kuanza kazi ya kuchunguza kwani hatuwezi kukamata
wananchi ovyo bila kuwa na vyanzo vya uhakika.
Mwili wa kikongwe Hellan
Petri Mahunzila (75) aliyefariki dunia kati ya oktoba 14 na 15 mwaka
huu ulizikwa majira ya saa 2 usiku ya eneo la Mondo mita chache kutoka
eneo alilotupwa kando ya shamba lake baada ya uchunguzi wa daktari wa
kituo cha afya Duthumi chini ya askari polisi wa kituo cha Kisaki-Gomero
katika wilaya ya hamashauri ya wilaya ya Morogoro.
Kitongoji
cha Gongo kijiji cha Mgata kipo umali wa kilimeta 14 ukitokea
Bwakilajuu ili kuweza kufika katika kitongoji hicho itakulazimu
kutembelea kwa miguu masaa matano kutokana na kutokuwepo kwa barabara
inayokuwezesha kutumia usafiri wa gari ama pikipuki huku kijiji cha
Bwakilajuu nacho kikiwa na umbali wa kilometa 16 kutoka kijiji cha
Dakawa kilichopo barabara kuu ya Mvuha-Kisaki chenyewe kikipitika kwa
nyakati zote za masika na kiangazi kwa usafiri wa gari ama pikipiki.
No comments:
Post a Comment