JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika
siku za hivi karibuni, imebainika kuwa, baadhi ya watu waliomilikishwa
silaha kihalali wamekuwa wakitumia silaha hizo kinyume na malengo mazuri
ya umilikishwaji. Baadhi yao wamekuwa wakitoa vitisho kwa wananchi kwa
kutumia silaha hizo bila sababu za msingi wawapo katika maeneo
mbalimbali, kama vile kwenye mabaa, kumbi za starehe na hata kulipizana
visasi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na malengo ya umilikishwaji.
Kufuatia
hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linatoa onyo kali kwa wote wenye
tabia hiyo kuacha mara moja na badala yake wanatakiwa kuzingatia sheria
na masharti waliyopewa wakati wa umilikishwaji.
Aidha,
Jeshi la Polisi linaanza operesheni kali ya kuwabaini wote wanaofanya
vitendo hivyo, ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya silaha hizo wale
watakaobainika kwenda kinyume cha sheria na matumizi ya silaha zao.
Jeshi
la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote wazalendo na wenye mapenzi
mema na nchi yetu, kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini watu hao
wanaojihusisha na vitendo hivyo ili waweze kukamatwa na kufikishwa
kwenye vyombo vya sheria kupitia namba ya simu 0754785557, namba za simu
za makamanda wa mikoa au kwenye kituo chochote cha Polisi.
Imetolewa na:-
Advera Senso – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment