WAKATI
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ikiendelea na
kikao chake jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe,
amekacha. Zitto ambaye katika siku za hivi karibuni aliibua mjadala
kwenye vyombo vya habari, hasa alipoingia kwenye malumbano na Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema, amekacha kikao hicho na badala yake ametoa
taarifa ya kusafiri nje ya nchi.Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa
iliyotolewa kwa wajumbe wa mkutano huo na Mwenyekiti wa CHADEMA taifa,
Freeman Mbowe, ilisema kuwa Zitto yuko safarini nchini Sudan, lakini
anatarajia kuhudhuria mkutano huo wakati wowote.Habari kutoka ndani ya
kikao hicho kinachofanyika kwenye Hoteli ya Blue Pearl, jijini Dar es
Salaam zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe wameonyesha dhahiri kukerwa na
hatua ya naibu katibu mkuu huyo kutoshiriki.
Waliolalamikia
hatua hiyo walisema kuwa limekuwa jambo la kawaida kwa Zitto
kutohudhuria vikao muhimu vya chama huku akijua fika kwamba yeye ndiye
msaidizi mkuu wa katibu mkuu wa chama taifa.
Mmoja wa
wajumbe wa kikao hicho aliliambia gazeti hili kuwa moja ya ajenda
zilizowasilishwa jana na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi ni kuhusu mapato
na matumizi ya chama ambayo alidai ingefaa Zitto awepo kuisikiliza.
Mjumbe
huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema ajenda hiyo ilikuwa
muhimu kwa Zitto kuwepo kwani akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), amekuwa akidai kwamba CHADEMA na vyama vingine hawana
hesabu za mapato na matumizi ya fedha za ruzuku wanazopata kila mwezi.
Mkutano huo unaendelea leo.
No comments:
Post a Comment