Waziri
wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amepiga marufuku magari ya serikali
kutengenezwa kwenye gereji binafsi na badala yake Wakala wa Ufundi na
Umeme (Temesa) afanye kazi hiyo.
Kadhalika, Waziri Magufuli amesema ipo harufu ya rushwa kwa mameneja wa
Temesa mkoa kwa kutoa vibali kwa magari ya serikali kutegenezwa gereji
za watu binafsi na hivyo kuikosesha serikali mapato.
Aliyasema hayo jana wakati wa kukabidhi vitendea kazi vya karakana za mikoa na vituo kwa mikoa kumi ya Tanzania Bara.
Alisema ipo tabia iliyoota mizizi kwa
mameneja kutoa vibali magari ya serikali yatengenezwe gereji za watu
binafsi ambazo nyingine ni bubu huku wataalamu walioajiriwa na serikali
wakishindwa kuwajibika.
Alisema
kwa mujibu wa sheria namba 30 ya mwaka 1997, hairuhusiwi gari yoyote ya
serikali kutengenezwa nje ya karakana zake, lakini kwa maslahi binafsi
imekuwa kawaida kwa magari hayo kutengenezwa hadi gereji bubu.
Alisema
Wizara itaendelea kutoa vifaa zaidi ili kuboresha karakana hizo kwa kuwa
kumekuwa na malalamiko ya ukosefu wa vifaa hali iliyotumika kama fursa
kwa mameneja kupeleka magari kwenye gereji binafsi.
Alisema
lipo tatizo sugu la taasisi za serikali kutengenezewa magari na kugoma
kulipa hali ambayo imekuwa kikwazo kwa ukuaji wa Temesa kwani inadai
mamilioni ya fedha.
Bila
kuzitaja taasisi hizo, alisema zinafanya makusudi kwa kutengenezewa
magari na wanapokumbushwa kulipa huyakana madeni na ufuatiliaji huwa
mgumu kutokana na kukosekana kwa nyaraka muhimu.
Pia, wanapokuja kutengeneza kwa awamu ya pili huomba kibali cha kwenda gereji za nje na mameneja huvitoa hali inayozua utata
“Gari ya
serikali ikitengenezwa Temesa haitaki kulipa ila ikipelekwa gereji
binafsi wanalipa kwa wakati…kuanzia sasa hakuna kutengeneza gari pasipo
makubaliano rasmi kwa kuchukua taarifa za aliyepeleka gari ili fedha
hizo zikatwe moja kwa moja kwenye fungu la matumizi ya ziada kutoka
Wizarani,” alisisitiza Magufuli.
Aidha,
alizitaka karakana hizo kuongeza ufanisi wa kazi ikiwa ni pamoja na
kumaliza kazi kwa haraka kwani kumekuwa na malalamiko ya ucheleweshwaji
wa kazi ikiwa ni pamoja na kukosa lugha ya biashara.
“Ifike
mahali Meneja wa karakana ya Vingunguti na Mt mjiulize kwanini magari ya
serikali Dar es Salaam, yanatengenezewa Kibaha, inaonyesha karakana
hiyo imejiaminisha inafanyakazi kwa ufanisi,” alibainisha.
Aidha,
aliagiza magari ya miradi ya barabara yaliyo chini ya Wakala wa Barabara
Nchini (Tanroads), yasajiliwe na kuuza kwa Temesa na Wakala wa majengo
Tanzania (TBA), ambako kuna upungufu mkubwa na maeneo mengine hakuna
magari.
Awali,
Mtendaji Mkuu wa Temesa, Mercelline Magesa, alisema utoaji wa vifaa
hivyo ni endelevu na ni awamu ya pili baada ya mikoa kumi ya awali
vilivyogharimu zaidi ya Sh. milioni 823.8.
No comments:
Post a Comment