Dodoma. Mbunge wa Sikonge, Said Mkumba (CCM), amemshukia Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kuwa amebeza kauli ya Bunge na kukejeli chombo hicho kwa kwenda kuzungumzia Operesheni Tokomeza Majangili nje ya Bunge, wakati uamuzi ulishatolewa bungeni.
Mkumba, jana aliomba mwongozo wa Spika kupitia
kanuni ya 68 na hatua hiyo aliifanya muda mfupi baada ya kumalizika kwa
kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Mbunge huyo alisema juzi wabunge walijadili kwa
kina hoja ya dharura kuhusu maonevu wanayofanyiwa wananchi katika
Operesheni Tokomeza Majangili.
Alisema hata hivyo Balozi Kagasheki, ameonekana na
kunukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba wabunge wanasema sema tu
ndani ya Bunge lakini hawajali rasilimali za taifa.
Alisema waziri huyo pia alisema hatishwi na uamuzi
ya wabunge wa kumtaka ajiuzulu na kwamba hatoki hadi aliyemteua
abatilishe uamuzi wa uteuzi wake.
“Sasa kwa kuwa yeye mwenyewe ndiye aliyetoa kauli
ya kusitisha operesheni hii ya Tokomeza na kitendo cha kuwakamata
Wachina ni zoezi tu la Serikali la kila siku ambalo linaweza kuendelea
bila operesheni,” alisema.
Je, mheshimiwa Spika, mheshimiwa waziri aliyetoa
kauli ndani ya Bunge na anatoka nje na anabeza kauli ya Bunge, anakejeli
Bunge naomba mwongozo wako kama jambo hili linaruhusiwa, “ alisema
mbunge huyo.
Spika Makinda aliwaonya wabunge na mawaziri kutotumia vibaya midomo yao.
“Nadhani matumizi mabaya ya mdomo yasitumike kwa
sababu tukishakubaliana vitu hapa kwenda kusema vitu vingine ni kuwasha
moto pengine uliokuwa unaendelea kuwaka vizuri,”alisema.
Bunge liliazimia kuunda kamati maalumu ya
kuchunguza operesheni hiyo ambapo Spika Makinda aliahidi kutangaza
wabunge watakaounda kamati hiyo jana.
Akizungumza baada kukamata pembe 706 za ndovu
jijini Dar es Salaam, Balozi Kagasheki alisema wabunge wanaomtaka
ajiuzulu kwa madai kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili imesababisha
mauaji ya watu na mifugo wanapoteza muda kwa kuwa mwenye mamlaka ya
kumtoa ni Rais Jakaya Kikwete pekee.
Alisema ipo mikakati inayofanywa na baadhi ya wabunge kutaka kuwang’oa baadhi ya mawaziri kwa masilahi binafsi ya kisiasa.CHANZO MWANAINCHI
No comments:
Post a Comment