
*Ampa ushauri ule ule uliomkosanisha na JK
*Marekani, Uingereza, SADC wazidisha kibano
WAKATI hatima ya kutiwa saini mkataba wa amani kati ya Serikali ya
DRC na waasi waliosambaratishwa wa M23 ikiwa haijulikana, uhusiano wa
maswahiba wawili wa eneo la Maziwa Makuu, Rais Yoweri Museveni wa Uganda
na Paul Kagame wa Rwanda umetikisika baada ya Museveni kumtaka mwenzake
huyo azungumze na waasi.
Ni ushauri
kama huo aliopewa Kagame Mei mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete ukilenga
kuleta na kuimarisha amani Mashariki mwa Congo ndio ulioyumbisha
uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda, kabla ya Kikwete kuifafanua na
kisha kukutana na Kagame jijini Kampala, Uganda Agosti mwaka huu.
Kwa
mujibu wa mtandao wa AfroAmerica Network, Museveni, baada ya kurejea
kutoka kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za SADC na zile za Maziwa Makuu
(IGGLR) huko Pretoria, Afrika Kusini wiki iliyopita, alimpigia simu
Kagame na kumwambia: "Huenda sasa ni wakati muafaka wa kuzungumza na
wapinzani wako wenye silaha."
Chanzo
cha habari cha mtandao huo kimemnukuu mmoja kati ya viongozi wa juu wa
Jeshi la Rwanda (RDF), akisema Museveni alimwomba Kagame kuzungumza na
waasi hao haraka kabla muda haujapita mara tu Rais huyo wa Uganda
aliporejea Kampala Alhamisi iliyopita.
Mkutano
wa pamoja wa wakuu wa nchi za SADC na ICGLR uliofanyika kuanzia Jumatatu
wiki iliyopita chini ya uenyekiti wa marais watatu, Joyce Banda
(Malawi, SADC), Museveni (Uganda, ICGLR) na wa Afrika Kusini, Jacob
Zuma, ulitoa wito kwa M23 kuweka silaha chini. Siku mbili baadaye waasi
hao wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, walishindwa vita na kutangaza
kuacha uasi.
Kagame hakuhudhuria mkutano huo, badala yake aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Louise Mushikiwabo.
"Ni
ushauri tu. Nimerejea kutoka kwenye mkutano na SADC uliojadili amani
eneo la Maziwa Makuu. Bahati mbaya inaonekana kwamba karibu viongozi
wote wanaamini kikwazo kikubwa cha amani ni kuwapo kwa waasi wa
Kinyarwanda mashariki mwa DRC.
"Hakika
suala hili linapaswa kuzungumzwa kwa njia moja au nyingine. Na viongozi
hao wanaamini kwamba hili halitatatuliwa bila serikali ya Rwanda kukaa
kwenye meza ya usuluhishi na wapinzani wake wenye silaha. Hata mimi
ninaamini hivyo, huenda wakati umefika kwako kuzungumza nao,"
alinukuliwa Museveni akimwambia Kagame katika mazungumzo ya simu
yaliyodumu kwa takriban dakika 15.
Kagame alijibu: "Sitozungumza na FDLR, washiriki wa mauaji ya kimbari. Never, ... , ever. Sitozungumza kamwe na wahalifu."
Hata
hivyo, inadaiwa Museveni alimkumbusha Kagame kuwa si waasi wote wa
Rwanda walioko DRC ni wanachama wa FDLR au wahalifuna kwamba wapo
anaoweza kuzungumza nao kwa kuanzia.
Baada ya
mazungumzo hayo, Kagame aliitisha mkutano wa dharura na washauri wake
wakuu na kuwaeleza walichozungumza na Museveni na kuongeza:
"Nimekuwa
nikiwaambia mara kwa mara kuwa tuko peke yetu. Hata Yoweri,
tuliyemwamini kama rafiki yetu na mwenzetu anatugeuka! Leo anatuambia
hiki, kesho anakwenda kukutana na viongozi wengine na kutubadilikia."
Baadaye
akawataka washauri hao kuja na mpango mkakati wa nini cha kufanya wakati
huu Rwanda ikizidi kutengwa na nchi za Afrika na hata za nje ya Afrika.
Mwanzoni
mwa mwezi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na mwenzake wa
Uingereza walimwonya Kagame kuachana mara moja na ushiriki wake kwenye
machafuko ya mashariki mwa DRC, ikiwa ni mara ya pili ndani ya mwaka
mmoja kwa wakubwa hao kutoa onyo kama hilo.
Wakati
hayo yakiendelea, zipo taarifa kwamba Rais Museveni amepanga kutuma
ujumbe nchini kuja kuzungumzia mustakabali wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaambia Watanzania kwamba
Tanzania haijakiuka chochote katika makubaliano ya msingi, ila wenzetu
hao ndio huenda wana ajenda yao.
Kauli ya
Kikwete ilihitimisha hali ya wasiwasi wa Tanzania kujitoa EAC na iwapo
ujumbe wa Uganda utakuja, itakuwa ni mwendelezo wa kilichofanywa
mwishoni mwa wiki na Kenya waliomtuma Waziri wa Mambo ya Nje kuja Dar es
Salaam kuweka mambo sawa.
>>>Hali nchini Kenya
Mapema
wiki hii, aliyekuwa Mwanasheria wa Serikali ya Kenya, Amos Wako ambaye
pia ni Seneta wa Bisia alitoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha
kuwa EAC haisambaratiki, akidai kuwa watakaoumia zaidi ni Wakenya.
Wako
aliyekuwa kwenye mkutano wa hadhara pamoja na Mbunge wa Budalangi, Ababu
Namwumba, alisema wakati jumuiya ya awali ilipovunjika mwaka 1977,
Wakenya wengi waliokuwa wakifanyakazi nje ya nchi ndio walioathirika
zaidi.
"Wapo
watu mashuhuri kama Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wanaokubalika ndani
na nje ya nchi ambao kama Uhuru anataka wanaweza kumsaidia kuzungumza na
Rais Kikwete wa Tanzania. Hatutaki jumuiya hii ivunjike, si busara hata
kidogo," alisema Wako. Chanzo: mtanzania

No comments:
Post a Comment