Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, November 17, 2013

Tido Mhando:Nazomewa uwanjani



Tido Mhando 

Kwenye simulizi zangu hizi za kila Jumapili, hupata wasaa wa kuelezea baadhi tu ya yale mengi niliyokutana nayo kwenye maisha yangu ya muda mrefu kama mtangazaji wa redio wa kitaifa na kimataifa. Jumapili iliyopita, nilisimulia juu ya siku niliyorejea kutoka Mombasa ambako nilikuwa nimekwenda kwa ajili ya fungate, Februari 1974, baada ya kufunga harusi. Nilielezea kwamba, nikiwa bado uwanja wa ndege, nilifahamishwa kuwa kijisanduku changu kilichokuwa kimepotea wakati nilipokuwa safarini New Zealand mwezi uliotangulia kilikuwa kimepatikana. SASA ENDELEA...
Pamoja na kupoteza shauku kuhusu kikijsanduku hicho, taarifa hizi za kupatikana kwake, zilifanya niwaze haraharaka kuhusu yote yaliyotokea kutokana na kupotea kwake.
Nikakumbuka kwamba nilipokuwa New Zealand, mara mbili nilipatiwa fedha za kujikimu na Kampuni ya Ndege ya Qantas ambayo iliwajibika kwa upotevu huo. Fedha hizo ziliniwezesha kununua nguo zangu murua pamoja na vitu vingine kadhaa muhimu.
Na wakati nikiwa njiani kurejea nyumbani, nilipofika Australia, kampuni hiyo ya ndege ikaamua kunilipa fidia ya mwisho ya upoteaji huo ya kiasi cha dola mia nne, fedha ambazo zilinisaidia sana katika kununulia nguo na vifaa vingine vya bibi harusi wangu, nikaonekana mwanamume wa shoka.
Sasa baada ya mambo yote haya kukamilika, nikiwa nimesahau na kukata tamaa juu ya kijisanduku hicho, naambiwa kimepatikana. Ndipo nikaamini kweli kwamba, Mungu ni mkubwa na ana mambo yake.
Basi nikaelekea kwenye chumba ambako masanduku yaliyopotea huhifadhiwa. hakika, kufika tu, nikakiona kijisanduku changu. Kilikuwa cha rangi ya kijivu na kwa kuwa nilikanunua mahsusi kwa safari ile ya New Zealand, kilikuwa bado kwenye hali yake nzuri tu.
Nilikachukua bila hata kukifungua na kwenda nacho nyumbani. Nilipokaangalia baadaye, nikakuta ya kwamba nilikuwa nimeweka humo nguo chache mno ambazo kwa sasa niliziona kamwe hazikuwa na mvuto. Kwa mara nyingine, nikashukuru kwamba ni heri kisanduku hicho kilipotea na kwa jinsi hiyo, nikafarijika.
Siku chache baadaye, nilirejea ofisini RTD. Nilijiona kama mtu mpya, kwa maana nilikuwa nimeshapiga hatua kubwa nyingine maishani. Nimefunga pingu za maisha, naitwa mumewe Mwangaza. Niliamua ya kuwa ingebidi kubadilisha mtindo wa maisha kwa kuacha kabisa yale ya ubarobaro kwa kuchapa kazi tu mtindo mmoja maana punde nitakuwa baba pia.
Kwa hakika, mwaka ule ulikuwa na mambo mengi mno hasa ya kimichezo. Ukiacha ile Michezo ya Commonwealth kule New Zealand, pia yalikuwapo mashindano mengine kadhaa ya kandanda ya hapa nyumbani na hasa yale ya ubingwa wa vilabu yaliyokuwa yamepamba moto.
Wakati huo, mashindano yenyewe yalikuwa yakifanyika kwa mtindo wa kutoana huku vilabu vya Yanga na Simba vikiwa ndivyo vinatambiana ile babu kubwa kwa ushabiki wa kiwango cha juu, labda kuliko wakati mwingine wowote ule.
Kwa jumla, ilikuwa vigumu kwa mtu yeyote kuepuka ushabiki huu wa kufa mtu. Ushabiki uliokuwa umewavaa hata viongozi wa juu wa Serikali. Ushabiki ambao ulikuwa umeingia vilivyo pale RTD wakiwepo jamaa ambao walikuwa hata wamechukua nafasi za uongozi wa juu kwenye vilabu hivi.
Wakati nilipoanza kazi pale, mtangazaji mwenzetu Mshindo Mkeyenge alikuwa Katibu Mwenezi wa Yanga na kwa upande wa Simba wakati huo Katibu Mwenezi alikuwa tena mtangazaji mwingine pale pale RTD, Zuberi Mkali.CHANZO MWANANCHI

No comments:

Post a Comment