Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, November 25, 2013

NGUGI WA THIONG'O NA MATEKA WA LUGHA

Prof_Ngugi_18768.jpg
Ni saanne kamili asubuhi siku ya ijumaa tarehe 22 , November 2013 katika ukumbi wa Nkrumah Chuo Kikuu cha Dar es asslaam ,makamo mkuu wa chuo, Profesa Rwekaza Mkandala anaingia katika ukumbi huu uliosheheni mpaka pomoni .Wanajumuia wa chuo kikuu pamoja na wageni na wanazuoni wengine wakiwemo raia wa kigeni wakiwa hawaamini macho yao kumuona mgeni waliyekuwa wakimsubiri kwa muda mrefu.Mgeni huyu akiwa ameambatana na profesa Mkandala hakuwa mwingine bali mwanaharakati na mwandishi mashuhuri wa vitabu,nguli wa fasihi katika Afika na dunia kwa ujumla ,Ngugi wa Thiong'o. Alizaliwa miaka 75 iliyopita kule Kimiriithu wilayani Kiambu nchini Kenya .Alikuwa amewasili siku moja kabla akitokea California nchini marekanai anakofanyia shughuli zake kuja kutunikiwa shahada yake ya heshima ya udaktari katika fasihi,siku ya jumamosi tarehe 23 ,Novemba 2013.Ngugi pia amewahi kutunikiwa shahada za heshima za udaktari zipatazo saba toka katika vyuo vikuu mbali mbali duniani.
Ngugi wa Thiongo ameandika kazi nyingi za fasihi lakini zilizo maarufu zaidi ni kama vile Petals of Blood;The River Between;Weep,not my child;a grain of wheat,ngaahaika ndeenda na Devil on the Cross,kazi zake nyingi zinatumika katika mitaala ya shule za sekondari na vyuo vikuu katika nchi mbali mbali duniani ikiwemo Tanzania na baadhi ya kazi zake zimetafsiriwa katika lugha zaidi ya 30
Bara la afrika lina utajiri wa waandishi lukuki na mahiri katika fasihi lakini majina ya Ngungi wa Thiongo na hayati Chinua Achebe yamekuwa yakionekana kuwa juu ya wengine ,wengine ambao pia ambao kazi zao zinatambulika ulimwenguni kote ni kama vile marehemu Okop p Bitek,Camara Laye,Wole Soyinka ,Sembene Osmane,ferhat abbas kwa uchache .orodha hii inaungana na waandishi na wanafasihi wa nchini kwetu kama; marehemu shaaban robert,shafi adam shafi,chachage seith chachage,penina mlama ,amadina lyiamba,hayati Agoro anduru,Ben Mtobwa .Fred Macha Euphrase Kazilahabi,marehemu Elvis Musiba na wengineo
Akitoa neno la utangulizi makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Profesa Mkandala alisema haingekuwa busara kumtunuku shahada hiyo na kisha akapaa zake marekani bila kumpatia fursa ya kutupatia mawaidha kutokana na uzoefu wake katika fasihi
Punde muda uliwadia kwa nguli huyo kusimama juu ya mambari kutoa mhadhara ambapo mada kuu katika ilikuwa wanazuoni;lugha za ulaya na za Afika baina ya utumwa na uwezeshwaji. Kwa mujibu wa maelezo yake ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutoa mhadhara kwa lugha ya Kiswahili hali iliyoamsha shangwe kwa wahudhuriaji ukiacha baadhi ya raia wa kigeni
Profesa Ngugi alianza kwa kueleza kuwa ukifanya jambo lolote au kitu chochote kwa lugha yako utakuwa umewezeshwa lakini ukikifanya katika lugha ya kigeni utakuwa umewezwa ,aliifananisha lugha na silaha ,kama ijulikanavyo silaha hutumika vitani na kwenye vita lazima kuwe na majemedari kwa maana ya viongozi ,wanazuoni na wasomi ,lakini majemedari hao wemekuwa mateka ,mateka wa lugha ,alibainisha pia kuwa ukijua lugha yako na ukapata fursa ya kujifunza lugha za kigeni ni kitu kizuri kwani utahamisha maarifa ya kigeni katika jamii yako. Akimtolea mfano Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa mahiri katika lugha ya Kingereza na ambaye alitafsiri kitabu cha Julius Caesar,pamoja na Mabepari wa Venice katika lugha ya Kiswahili ,hata Ngugi mwenyewe pamoja na umahiri wake katika lugha ya Kingereza amekuwa akiandika vitabu vyake katika lugha yake ya asili ya Kikuyu.aliendelea kueleza kuwa hakuna chuo kikuu hata kimoja barani afika ambacho kinafundisha kwa kutumia lugha ya asili ya afrika,alionyesha pia kushangazwa na baadhi ya wanafunzi wa shule kuadhibiwa wanapokutwa wakizungumza lugha zao za asili katika maeneo ya shule ,nikakumbuka kipindi kile tulipokuwa sekondari ilikuwa ukikutwa unaongea Kiswahili unavalishwa gunia kama koti ungevizia mtu mwingine anayeongea Kiswahili umvalihse la sivyo ungekaa nalo mapaka muda wa kulala huku adhabu kali ikikusubiri.Pia katika shule nyingi si ajabu kukuta vibao vimeandikwa speak English katika viambaza vya shule. Kwa ujumla alitetea matumizi ya lugha zetu za asili kulinganisha na zile za kigeni
Ilikuwa ni mada iliyovutia adhirana lilikuwa ni darasa tosha kwa wahudhuriaji.baada ya mhadhara ule aliniacha na changamoto ambazo sikuweza kupata bahati adhimu ya kumuuliza .
Changamoto mojawapo ilikuwa ni matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya Taifa,Profesa Ngungi ,kama nilivyoeleza hapo awali aliwafananisha viongozi na wazuoni na mateka mimi kwa upande wangu niliona heri ya hawa aliowaita mateka kuliko kundi lingine ambalo kuliita mateka ni kama kulipendelea, maana tukiangalia filami za kule Hollywood huwa tunaona mateka wakikombolewa kumbe basi kuna nafasi ya hawa aliowaita mateka kukombolewa ,kundi hili amabalo mimi pia naangukia humo,sijui tulipatie jina gani?nitatoa mfano,baba yangu ni mwenyeji wa pwani ya Tanzania wakati mama yangu ni mwenyeji wa kanda ya ziwa nimezaliwa na kukulia llala jijini Dar es salaam,nyumbani lugha ya mawasilano ni Kiswahili,nimesomea shule za serikali na elimu ya juu nimesomea hapa nchini,sina umahiri wa lugha yoyote, ndio sina umahiri wa lugha yoyote, sifahamu lugha ya asili ya baba wala mama, Kiswahili changu ni kile kinachoniwezesha kuwasiliana tu lakini nani hajui Kiswahili cha watoto waliokulia maeneo ya mijini huwezi kukitumia kwenye mikutano ya umoja wa mataifa au umoja wa afrika wala kwenye redio za kimataifa zinazotumia lugha ya Kiswahili kama BBC na nyinginezo.kwenye kiingereza nani hajui tatizo linalokabili taifa letu juu ya lugha hiyo,vijana wengi wanahitimu elimu ya chuo kikuu lakini hawana umahiri wa lugha ya Kingereza tofauti na zamani.sasa mimi utaniweka kundi gani na nikipita mtaani naitwa msomi,ndio ni msomi endapo wahitimu wa chuo kikuu wote ni wasomi nami pia ni msomi,sasa utaniweka kundi gani,na sipo peke yangu tupo wengisana tunaoangukia kwenye kundi hili ambalo miaka michache ijayo ndio litakuja kutoa viongozi wa nchi,kuna uwezekano wa kupata viongozi ambao watatutia aibu katika anga la kimataifa kwani watashindwa kuwasiliana na wenzao hii imeshaanza kujitokeza kuna kiongozi alidai ulimi uliteleza (slip of tongue)
Kuna baadhi ya watu wanadhani Kiswahili kilianzishwa na mwalimu Nyerere, la hasha, lugha hii adhimu ilikuwepo hata kabla ya uhuru na ilikuwa ikiongelewa eneo kubwa la afrika mashariki na kati,alichofanya mwalimu ni kuirasimisha lugha hii kuwa ya Taifa baada ya kuona ina wazungumzaji wengi,Ni jambo lisilopingika kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa na maono ya kukifanya Kiswahili kijulikane na kieleweke kwa kila mtanzania bila kuyavunja makabili kama ilivyo nchi ya Rwanda ambapo kuna makabila matatu ya watwa,watusi na wahutu lakini wote wakiongea lugha moja ya Kinyarwanda.
Tatizo lililotokeani kuwa hakukuwekwa uwekezaji mkubwa katika Kiswahili ,pamoja na sera iliyowekwa bado ilitakiwa ili tuweze kuongea Kiswahili fasaha na sanifu kuwe na uwekezaji mkubwa wa hali na mali,mpaka leo kuna watu wanadai Kiswahili hakifai kufundishia elimu ya juu kwa kuwa eti hakina misamiati ya kutosha na itakuwa gharama kutafsiri vitabu hususani vya kisayanzi katika Kiswahili,madai haya mawili yanaitaji uwekezaji ili kufanya tafiti za lugha na kutafsiri vitabu inginevyo umateka utaendelea kutusumbua.
Leo hii ukienda kwenye usajili wa ajira kwa kiwango kikubwa lugha inayotumika huwa ni Kingereza, ukiwa na bahati utaulizwa na wana jopo kuwa ungependa kufanyiwa usaili kwa lugha gani,tatizo ni pale utakapochagua Kiswahili wajumbe wa jopo (wengi wao mateka )huanza kukuweka katika kundi la wasiofaa kupewa ajira kwa kudhani hujui Kingereza,ambacho kwao ndio kipimo cha akili.ukichagua lugha ya Kingereza na ukakwama katikati wakati wa kujieleza ujue kazi umeishakosa.
Kuwekwe uwekezaji wakutosha kwa lugha yetu kiswahili na kingereza pia.kwani lugha zote ni mihimu kwa zama hizi nitatoa mfano wa marafiki zangu watatu toka nchi jirani,mmoja anatoka msumbiji,yeye anaongea kireno fasaha na pia lugha yake ya kimakonde ,mwingine anatokea Burundi yeye anaongea Kirundi na kifaransa kwa ufasaha,mwingine anatokea Uganda yeye anaongea kingereza na kiganda kwa ufasaha hawa wote ni wanafunzi wa chuo kikuuu cha Dar es salaam baada ya miaka miatatu ya elimu yao hapa watakuwa wanajua Kiswahili pia na kingereza kwa Yule rafiki yangu toka msumbiji ,hali kwa mwanafunzi mtanzania wa aliyekulia mkini ndio kama nilivyoeleza hapo awali,nafuuu ipo kwa wale waliosoma hizi shule zenye mlemgo wa kimataifa sijui tuziiite English medium au international school wao kwa kiasi kikubwa wana uelewa wa lugha ya kingereza ila lazima itambulike lugha ni kitu tofauti na uelewa wa masomo kwa maana ya maarifa ,katika masomo mengine hupata ufaulu hafifu kuliko wale waliosomea shule za kata .kama Profesa Ngungi alivyobainisha kuwa ukiijua lugha yako kwa umahiri na ukajifunza na kujua lugha za kigeni ni jambo jema lakini ukijua lugha ya kigeni kwa umahiri na kuitukuza kuliko lugha yako wewe ni mateka.
Baada ya mhadhara ule nilibakiwa na swali ambalo sikupata muda wa kumuuliza profesa Ngugi,swali lenyewe ni hili;Mwalimu Nyerere kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa alifanikiwa kutokomeza au kupunguza ukabila kwa kiasi kikubwa lakini Profesa Ngugi alisisitiza matumizi ya lugha za asili bila mipaka, lakini unapoambiwa kutaja nchi ambazo zimeathirika na ukabila Kenya haiwezi kukosa katika orodha ,je si kwa sababu ya kuendekeza hizi lugha za asili kutumika kwenye mikutano ya kisiasa pamoja na maeneo mengine ya umma?
Togo Singano
Tel 0773123400


 

No comments:

Post a Comment