Mkutano wa Wajumbe walioshiriki mazungumzo ya nyuklia mjini Geneva
Hatimaye
Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani wamefikia makubaliano kuhusu
mpango wa nyuklia wa Tehran, Kiongozi Mkuu wa mjadala huo Bi, Catherine
Ashton amethibitisha hilo baada ya takribani siku tano za majadiliano
makali ya mjini Geneva nchini Uswisi.
Mataifa
yenye nguvu duniani ambayo ni Uingereza, Marekani, Urusi, China,
Ufaransa na Ujerumani wamekuwa na madai ya kutaka Tehran isitishe
urutubishaji wa uranium ili iondolewe vikwazo inavyokabiliwa navyo.
Waziri wa
mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema wamefikia muafaka wa
mzungumzo hayo na miongoni mwa mambo muhimu kwao ni kutumia nyuklia
katika uzalishaji wa nishati sambamba na kupunguzwa vikwazo vya
kiuchumi.
Baada ya
kutamatika kwa majadiliano hayo, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John
Kerry amesema kuwa makubaliano hayo yatahakikisha usalama wa Israel
pamoja na eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa
upande wake Rais wa Marekani Barack Obama amepongeza hatua hiyo ya
kihistoria na kusema ni hatua kubwa ya kwanza kuelekea mpango wa
kuimarisha usalama wa dunia kutokana na makubaliano hayo kuizuia Iran
kutengeneza silaha za nyuklia.
Hata
hivyo Obama ameonya kuwa endapo Iran haitatekeleza vipengele vya
makubaliano hayo, basi vikwazo vya takribani dola za Marekani bilioni 7
vitarejeshwa na shinikizo kuongezwa.
No comments:
Post a Comment