KWELI
huu ni unyama wa wanaume hata kama si wote! Wanawake wawili wakazi wa
maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, wamepoteza maisha kufuatia madai ya
kuuawa na waume zao. Inauma sana na Uwazi ndilo lenye mkasa mzima!
Matukio
yote mawili yametokea jijini Dar es Salaam na kuacha vilio kwa ndugu na
jamaa wakiwa hawaamini kilichowakumba wapendwa wao.
WALIOTENDWAWanawake
waliojulikana kwa majina ya Mwanahamisi na mwenzake Waisiko Robert
Mtundi ndiyo waliodaiwa kuuawa na waume zao, kisa kikubwa kikidaiwa ni
hofu ya wanaume hao kusalitiwa katika mapenzi.
WANAODAIWA KUTENDA
Juma Shaban, mkazi wa Manzese
Kwamfuga Mbwa na Samuel Gesire Mlimi, mwenye makazi yake Msongola,
maeneo yote hayo yapo Dar ndiyo wanaodaiwa kutekeleza ukatili huo wenye
kutoa machozi mpaka basi.
MWANAHAMISI ALIVYOUAWA
Ilikuwa saa tatu usiku,
Septemba 21, mwaka huu, kila familia ya eneo la Kwamfuga Mbwa ilikuwa
ndani kwa chakula cha usiku au maandalizi ya kulala, ndipo waliposikia
zogo kutoka ndani ya chumba cha kwa wanandoa hao.
ZOGO NA MANENO
Kwa mujibu wa majirani hao
waliozungumza na gazeti hili baada ya tukio, zogo hilo liliambatana na
maneno ya shutuma kutoka kwa Juma kwamba mkewe huyo si mwaminifu ndani
ya uhusiano wao.
Majirani walisema shutuma za Juma ziliambatana na kelele za Mwanahamisi kuomba msaada akisema ‘nauawa jamani! Nauawa mwenzenu!’
Wakasema baada ya kama saa
moja ya mzozo ulipita ukimya, ndipo kila jirani alitoka nje na kuulizana
nini kinaendelea ndani ya chumba cha Mwanahamisi na mumewe!
“Baada ya dakika kumi,
tulimwona Juma akitoka chumbani kwake huku akiwa anabofyabofya simu yake
ya mkononi na kutokomea kusikojulikana,” alisema jirani mmoja huku
macho yakiwa yamevimba kwa sababu ya kumlilia Mwanahamisi ambaye wakati
huo alikuwa chini ameshakata roho.
Akaendelea: “Baada ya Juma
kuondoka tulipatwa na wasiwasi, tukaenda kumwangalia Mwanahamisi
chumbani na kumkuta hajitambui, amelala kifudifudi, ana majeraha sehemu
mbalimbali za mwili huku akiwa ametapakaa damu. Alikuwa akipumua kwa
mbali.
“Alikuwa hawezi kuongea
vizuri, mimi nilimsikia akisema hana uhai tena, tumwombee mtoto wake.
Ndani ya chumba tuliona viroba vya pombe kali na kisu kikiwa kimelowa
damu, nahisi ndicho alichotumia Juma kufanyia ukatili wake.
“Tuliamua kumwahisha hospitali
Mwanahamisi lakini kutokana na hali yake tuliona ni vizuri kuwasiliana
na polisi ambao walifika baada ya muda.
“Lakini siku yake Mwanahamisi ilitimia kwani wakati polisi wakijiandaa kumchukua kumkimbiza hospitali aliaga dunia.”
KUMBE NI MWEZI MMOJA BAADA YA KUHAMIA
Wengine waliozungumza na
gazeti hili siku ya tukio huku wakitoa machozi, walisema Juma ambaye
alitoroka baada ya ukatili huo, alihamia kwenye nyumba hiyo mwezi mmoja
nyuma lakini walipata umaarufu mtaani hapo kutokana na tabia yao ya
kupigana mara kwa mara.
MJUMBE WA MTAA NAYE ANENA
Akizungumza na gazeti hili
katika eneo la tukio, Mjumbe wa Nyumba Kumi, Techla Tesha aliwalaumu
majirani na wapangaji wa nyumba hiyo kwa kushindwa kumpelekea taarifa
mapema huku wakijua mtuhumiwa alikuwa na tabia ya kumpiga mkewe mara kwa
mara.
WAISIKO ALIVYOUAWA
Awali ya yote, inadaiwa Waisiko ni mke mkubwa, mke mdogo jina lake halikupatikana mara moja.
Siku ya tukio, saa tatu usiku
inadaiwa Samuel alikwenda nyumbani kwa Waisiko ambapo si mbali sana na
nyumbani kwa mke mdogo na kuangusha timbwili zito.
“Samuel aliingia ndani na kuanza kumpiga mkewe mkubwa huku akionya majirani kuwa asiwepo mtu wa kwenda kuamua ugomvi wao.
“Sisi kama majirani tuliogopa kwa sababu Samuel alikuwa akitishia kuwa atakayeingia atamchoma kisu.
“Licha ya vitisho hivyo,
tulisimama nje ya chumba chao huku vitisho vikiongezeka lakini namna ya
kutoa msaada tulishindwa. Hatukujua chanzo cha ugomvi wao.
“Kauli za mwanamke kila wakati
ziliashiria alichokuwa akitendwa kwa wakati huo, mfano kuna wakati
tulimsikia akisema anavunjwa mgongo, akasema anang’olewa kucha. Pia kuna
muda alilalamikia kuvunjwa mkono. Jamani, marehemu aliteswa sana kabla
ya kufariki dunia,” alisema shuhuda mmoja.
NI MATESO YA USIKU KUCHA!!
Shuhuda huyo aliongeza:
“Mateso ya mwanamke huyo huenda yalikuwa ya usiku kucha kwani nakumbuka
mpaka alfajiri ndipo tukasikia sauti ya mwisho ya Waisiko akisema Samuel
umeshaniua, nimalizie kabisa basi. Baada ya hapo hatukusikia tena sauti
wala vurugu.
SERIKALI YA MTAA YAZUNGUMZA
Makamu Mwenyekiti wa Serikali
ya Mtaa wa Msongola, Juma Chacha alipohojiwa kuhusiana na mauaji hayo,
alisema ana taarifa lakini mtuhumiwa alikimbia baada ya kutenda unyama
huo na anatafutwa na polisi.
UWAZI LABAINI KISA
Uchunguzi wa gazeti hili
ulibaini kuwa chanzo cha ugomvi huo ni wivu wa mapenzi kwani ilidaiwa
kuwa Samuel alikuwa akimhisi mkewe huyo kutoka nje ya ndoa.
Chanzo chetu kilisema siku ya
tukio, Samuel aliwachukua baadhi ya marafiki zake na kwenda nao baa
ambako aliwaambia kuwa anahisi mkewe huyo ana jambo kwani akimuuliza
kitu anamjibu jeuri.
Mtoa habari wetu alisema Samuel akiwaambia marafiki hao kwamba siku hiyo akirudi nyumbani, mwanamke huyo atamtambua.
POLISI WALIVYOIKUTA MAITI
Polisi walipofika na
kuichunguza maiti waliikuta imevunjwa mkono wa kushoto na kung’olewa
kucha za miguu huku uti wa mgongo nao ukiwa umevunjika.
Habari zinasema mara baada ya
mtuhumiwa kufanya mauaji hayo, alikwenda kwa mkewe mdogo na kumtaka
akamuone mke mwenzie, alipokwenda yeye nyuma akatoroka.
Polisi Mkoa wa Ilala tayari wamemfungulia jalada mtuhumiwa huyo lenye namba STK/RB/10058/2013 MAUAJI.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ACP Marietha Minangi amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment