Ni kutokana na viongozi wake kusema hadharani bila ya kutumia vikao vya chama
Dar es
Salaam. Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais
Benjamin Mkapa na katika Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, Dk Juma
Ngasongwa amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinababaika katika
kutekeleza majukumu yake.
Vilevile, chama hicho kimekumbwa mgawanyiko kati ya watendaji wake na Serikali na kwamba taifa lina ombwe la uongozi.
Kutokana
na hali hiyo, Dk Ngasongwa ambaye pia ni kada wa CCM amemshauri Rais
Kikwete kuwa mkali katika kusimamia watendaji wake anaowateua ndani ya
chama na Serikali yake na kufuatilia na kupima utekelezaji wa
yanayokubaliwa .
Alikuwa
akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake
mkoani Morogoro anakoendesha maisha yake kwa kilimo cha mpunga baada ya
kustaafu.
Dk
Ngasongwa alisema kuwa mgawanyiko huo kati ya watendaji wa Serikali na
CCM, umeondoa umoja siyo tu katika vyombo hivyo, bali pia miongoni mwa
wabunge wa chama hicho tawala.
Alisema
kuwa hali hiyo inasababisha kutokea mambo mengi ikiwamo matukio ya
mawaziri kushinikizwa kujiuzulu kama ilivyotokea hivi karibuni na kwamba
kwa Serikali ya Awamu ya Nne hali hiyo imekuwa ikijirudia.
"Chama
tawala kinababaika sana, tena hata watendaji wa CCM, wanawasema vibaya
mawaziri hadharani, wakati wote ni wateuliwa wa Rais (Jakaya Kikwete) na
ndiye mwenyekiti wetu wa CCM. Hii inakigawa chama. CCM ina utaratibu
wake, kwa nini wasiitwe wakahojiwa ndani ya chama, badala ya kutajana
hadharani:
"Sielewi
kwa nini CCM inababaika. Inachotakiwa ni kuwa na mshikamano kwa wabunge
wake kukutana mara kwa mara na kujenga msimamo. Hii ni kazi ya mawaziri
na wabunge pia," alisema Dk Ngasongwa na kuongeza:
"...Tatizo
uongozi haufanyi kazi vizuri, ndani ya chama chetu kuna mgawanyiko
mkubwa hata katika Serikali, mfano Mwanasheria Mkuu (AG) anaposema
baadhi ya mawaziri hawamsikilizi, hii 'No' (hapana), lazima kanuni za
uendeshaji wa Serikali zifuatwe, hii ni muhimu."
Alisema hali hiyo inaonekana hata kwenye Baraza la Mawaziri na kwamba mgawanyiko pia upo ndani ya Bunge kwa wapinzani.
"Lakini
kugawanyika kwa upinzani ni afadhali kuliko CCM, kwani matokeo yake ni
kupunguza imani ya watu kwa Serikali yao na chama tawala," alisema.
Akinukuu
maneno ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dk
Ngasongwa alisema: "Nyerere alisema, bila CCM madhubuti nchi itayumba na
ndiyo yanayotokea sasa.
"Msingi
wa yote yanayotokea ni ubinafsi, ubepari...; turudi kwenye Ilani ya
chama, tuzungumze, tufikie mwafaka, siyo kutukanana hadharani. CCM itoe
mwongozo siyo kugawa wananchi."
Ngasongwa
aliyeshika nyadhifa mbalimbali za kisiasa katika CCM na Serikali
ikiwamo ujumbe wa Kamati Kuu (CC), ubunge wa Ulanga Magharibi, Waziri wa
Maliasili na Utalii na baadaye Waziri wa Mipango, Viwanda na
Uwezeshaji, alifafanua kwamba kuna ombwe la uongozi katika chama tawala,
upinzani, Serikali hata bungeni.
"Kuna
ombwe la uongozi siyo tu kwa wapinzani, hata sisi chama tawala CCM,
Serikali, hata bungeni pia kuna mchanganyiko na yanaonekana waziwazi.
Tunaona Spika anavyodharauliwa na wabunge. Bunge linaonyesha picha ya
hali halisi ya nchi yetu ilivyo,"alisema Dk Ngasongwa.
Alipotakiwa kuzungumzia zaidi
tukio la
hivi karibuni la Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wanne
walioshinikizwa kujiuzulu kutokana na Ripoti ya Kamati ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, alieleza
kuwa hajaisoma kwa undani ripoti hiyo, lakini inaonyesha kuwa
utekelezaji wake ulikuwa mbaya.
Hata
hivyo, alisema kuwa kamati hiyo ilitakiwa kuainisha makosa ya watendaji
wa operesheni hiyo na kuwaacha mawaziri wajipime na kujiuzulu wenyewe.
Alisema
kwamba hatua ya wabunge na kamati kushinikiza mawaziri hao wajiuzulu
iliwachongea kwa Rais Kikwete aliyeamua kuwafukuza kazi kwa lugha ya
kistaarabu, hali ambayo alielezea kuwa inaweza kujenga uhasama baina ya
wabunge, kamati na mawaziri walioondolewa.
Hivi
karibuni Rais Kikwete alitengua uteuzi wa Waziri wa Maliasili na Utalii,
Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,
Shamshi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi pia
Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo baada
ya wizara zao kutajwa kushindwa kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili,
iliyopoteza maisha ya watu, mifugo na vitendo vya ukatili kwa binadamu.
Kuhusu
kubadilika kwa mawaziri, Dk Ngasongwa alieleza kuwa jambo hilo siyo
baya, lakini akasema kwamba likifanyika mara kwa mara linadumaza wizara
kwa kukosekana mwendelezo wa utendaji.
"...Ikitokea
mara kwa mara inadumaza utendaji, hupati 'continuity' (mwendelezo
mzuri), kwani mawaziri huhitaji kujifunza na utekelezaji huhitaji muda.
Continuity ni muhimu kwa mawaziri, hata watendaji wengine," alisema.
Hii ni
mara ya tatu kufanyika kwa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri tangu
kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete,
likiwamo lililotokea baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa
kujiuzulu. Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment