Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, December 28, 2013

FOLENI KUENDELEA KUTESA JIJINI DAR


Kuna kila dalili kuwa jinamizi la foleni litaendelea kuwatesa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa muda mrefu zaidi kutokana na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara za pembezoni (ring roads) na usanifu wa barabara za juu (flyig overs) ambayo kwa ujumla inahitaji walau Sh. bilioni 170.
Kero hiyo itapungua kwa kiasi kikubwa ikiwa fedha hizo zitapatikana ili kutekeleza miradi mbalimbali iliyopewa kipaumbele katika kukabili tatizo hilo.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE hadi kufikia mwisho wa wiki iliyopita, umebaini kuwa ujenzi wa barabara za pembezoni unaendelea kwa kasi ya kinyonga huku ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara kuu ukiwa ndiyo kwanza uko katika hatua ya usanifu.

Aidha, jumla ya Sh. bilioni 171.2, ambazo ni sawa na asilimia 14 ya bajeti yote ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/2014, ni sehemu tu ya mikakati iliyopewa kipaumbele katika utekelezaji ili kupunguza foleni jijini Dar es Salaam ikihusisha usanifu wa barabara za juu (Sh. bilioni 100), ujenzi barabara ya Kigogo – Jangwani (Sh. bilioni 7.6), fidia kwa majengo ya kandoni mwa barabara ya Kigogo-Jangwani (Sh. bilioni 15.8) na kipande cha kilomita tatu cha barabara ya Kimara Korogwe- Kilungule kinachogharimu Sh. bilioni 3.5.

Fedha nyingine ni Sh. bilioni 13 kwa ajili ya kilomita saba za Mbezi Mwisho-Goba, Sh. bilioni 16 za Tangi Bovu-Goba, Baruti-Msewe (Sh. bilioni 4.6) na Kigogo- Tabata Dampo (Sh. bilioni 5.7).

HALI ILIVYO
Hakika, katika jiji la Dar es Salaam kunahitaji uvumilivu wa hali ya juu, hasa kuhusiana na usafiri wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine nyakati za asubuhi na jioni.

Kiukweli, unaweza kujikuta usingizi wako ukiathiriwa na jinamizi la foleni. Unalala ukiwaza foleni itakavyokutesa asubuhi wakati ukienda au kurejea kutoka katikati ya jiji kusaka mkate wa kila siku.

Tatizo huwa kubwa zaidi kwa wakazi wa pembezoni mwa jiji. Kwa mfano, wanaoishi maeneo ya nje ya katikati ya jiji kama Tabata Segerea, Kinyerezi, Kibamba, Bunju na Kivule, hali huwa mbaya zaidi. Ni zaidi ya kero. Ni adhabu kubwa!
Mbaya zaidi, wakati mwingine adha hii huwa haichagui nyakati. Ni kawaida pia kukuta foleni kubwa ya magari mchana na hata usiku wa hadi saa 5:00.

Matokeo yake, siyo jambo geni kujikuta ukitumia jumla ya saa tatu hadi sita kwa safari ya kwenda maeneo ya katikati ya mji na kurudi.

Wananchi wa kawaida ambao wengi hutegemea usafiri wa daladala hujikuta wakikumbana na adha nyingine ya kupata usafiri huo kwani magari huwa haba kwa vile hutumia muda mwingi yakiwa yamesimama tu barabarani kutokana na foleni. Na gari linapofika kituoni, ni wenye nguvu tu ndiyo hujihakikishia siti huku wengine wakihaha walau kupata upenyo wa kuingia garini.

Wagonjwa, wajawazito, watoto na wazee huwa ni waathirika wakubwa kwani huwa hawawezi kupigania daladala hizi.

Wakati mwingine, unalazimika kutumia gharama maradufu kufika maeneo ya kati ya mji kwani mahali pa nauli ya Sh.400, unaweza kutumia Sh. 2,000 kwa kuwa madereva na makondakta wamegeuza mtaji kwa kupakiza abiria vituo vya mwanzo na kwenda nao hadi mwisho na kugeuka nao hata kama gari limejaa.

Mbali na kuwa kero kwa watumiaji wa barabara, foleni za magari pia husababisha athari za uchafuzi wa mazingira kwani magari hutumia muda mwingi barabarani na kutoa moshi (ulio na gesi ukaa) kwa wingi.

Zipo pia athari kubwa za kiuchumi kutokana na foleni ndefu za mara kwa mara katika barabara za jiji la Dar es Salaam kama Morogoro, New Bagamoyo, Kilwa, Kawawa, Mandela na Nyerere.

Kwa mfano, utafiti uliofanywa na kitengo cha takwimu cha Kampuni ya The Guardian Limited chini ya usimamizi wa Edward Ntwale, ulibaini kuwa msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam unaipotezea serikali mapato ya Sh. bilioni 411 kila mwaka, huku wafanyakazi wanaotumia usafiri wa daladala wakipoteza saa mbili barabarani kila uchao.

Aidha, kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 120.4 zinapotezwa na waajiri kila mwaka kwa kuwalipa wafanyakazi kwa saa ambazo hawafanyi kazi huku wamiliki wa daladala wakipoteza Sh. bilioni 265.6 na gharama za mafuta ya ziada kwa wamiliki wa magari zikiwa ni Sh. bilioni 25.6 kwa kipindi hicho.

Kulingana na utafiti huo, kiasi hicho cha fedha kinachopotea kwenye foleni ya magari kila mwaka kingeweza kugharimia ruzuku ya mbolea kwa mwaka wa fedha 2013/14 na chenji ikabaki, kwa kuwa serikali katika bajeti ya mwaka 2013/14 imetenga Sh. bilioni 349.2 pekee kwa ajili ya ruzuku ya mbolea.

Aidha, fedha hizo pia ni zaidi ya makisio ya serikali ya kukusanya Sh. bilioni 383.5 kutoka halmashauri kwa mwaka huu wa fedha.

Katika barabara ya Morogoro ambako hivi sasa kuna ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi (Dart), hali ni mbaya kwa kupita kiasi. Kwa sasa hakuna nafuu kwa nyakati za asubuhi, mchana wala usiku. Muda wote huwa kuna foleni na kila dereva hujitahidi kuhakikisha kuwa anaingia kwenye barabara hizi finyu ili kuwahi anakotaka kwenda.

Inapotokea ajali, hata kama ni ndogo kiasi gani, mateso ya foleni huongezeka maradufu.

Kupunguza au kumaliza kabisa foleni jijini Dar es Salaam kunahitaji mipango thabiti na utekelezaji kivitendo wa kila kinachoelezwa.

Hata hivyo, kinachoonekana ni kuwa kasi ya kukabiliana na adha ya foleni jijini Dar es Salaam haiendani na ongezeko la magari barabarani. Na ofisi nyingi muhimu za serikali na binafsi zinaendelea kuelekezwa katika maeneo ya katikati ya jiji, hasa Posta, Upanga na maeneo ya jirani.

“Imekuwa ni kawaida kuamka saa 10:00 alfajiri na kurudi nyumbani kwangu saa 5:00 usiku. Foleni inanifanya siku zote kuwa mgeni kwa familia yangu. Nashindwa kuonana na wanangu kwa wakati, nikitoka wamelala, nikirudi wamelala,” ndivyo anavyoeleza Nassari Kitoi, mkazi wa Mbezi Madale, eneo lililopo katika Manispaa ya Kinondoni, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Kitoi anasema kuwa kwa uzoefu wake, anajua kuwa siku za Jumanne hali ya foleni huwa ni mbaya zaidi kwani ni siku mojawapo ambayo magari yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam huondoshwa kwa wingi zaidi.

Kitoi anasema kuwa ili aweze kufika kazini kwake saa 2:00 asubuhi, hulazimika kutoka nyumbani kwake saa 11:00 alfajiri kwani nyakati hizo huwa kuna nafuu kubwa.

KINACHOENDELEA
Kwa kutambua kuwa foleni ni kero na pia zina madhara makubwa kwa uchumi wa nchi, Wizara ya Ujenzi imekuwa ikitangaza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo hilo, baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kujenga barabara za juu (fly overs) katika makutano ya barabara kubwa na pia kuboresha barabara za pembezoni mwa jiji (ring roads).

Katika Bunge la Bajeti lililokakaa kati ya Aprili na Juni mwaka huu, Waziri wa Ujenzi alisema kasma 4138, fedha zilikuwa ni pamoja na zile za matengenezo ya barabara za pembezoni ili kukabiliana na foleni kwenye barabara kuu jijini Dar es Salaam.

Barabara hizo ni Kimara Korogwe-Kilungule, Mbezi-Malamba Mawili-Kinyerezi- Banana, Tabata Dampo-Vingunguti, Tangibovu-Samaki Wabichi –Goba, Tegeta-Kibaoni-Wazo –Goba-Mbezi, Kimara- Baruti –Msewe na Kimara Baruti Tangibovu-Goba na Makongo Juu –Goba.

Solomoni Sungo na Peter Mikaeli ni madereva wanaotumia mara kwa mara barabara ya kutoka Tangibovu hadi Goba. Wanasema kuwa kwa ujumla, barabara hazina hali nzuri kwani matengenezo yake si ya kuridhisha. “Zinakwanguliwa bila kuwekewa changarawe.

Udongo unaokwanguliwa ndiyo huohuo unashindiliwa na wanasubiri hadi ziwe kwenye hali mbaya … hivi unavyoona ndiyo zimeshatengenezwa na sasa hata miezi mitatu haijapita lakini zimeshaharibika,” anasema Sungo.

Wanasema kipindi cha mvua, udongo huondolewa na barabara inaharibika tena. Baada ya muda inakwanguliwa na kushindiliwa upya bila kuwekwa changarawe ili kuifanya idumu kwa muda mrefu.

"Wengi hatuoni thamani ya fedha inayotengwa. Barabara inatengenezwa bila mitaro ya kupitisha maji. Zimenyanyaliwa kidogo na kuna maeneo ambayo mvua ikinyesha hazipitiki kabisa, mfano eneo lenye mwinuko mkali karibu na Goba,” anaeleza.

Mikaeli anasema imekuwa kawaida kwa magari kukaka ‘spring’ na bodi kuchakaa mapema kutokana na ubovu wa barabara hiyo ambayo kijiografia, ina nafasi kubwa ya kuwasaidia wakazi waotoka Mbezi Beach barabara ya New Bagamoyo kwenda kuunga kwenye barabara ya Morogoro kuanzia Mbezi Luis kuelekea Kibaha.

Anasema ni vyema serikali ikawasimamia kwa karibu makandarasi wanaopewa kazi ya kutengeneza barabara hizo ili kuhakikisha kuwa fedha inayotolewa inafanya kazi inayotarajiwa; na siyo kuzitengea fedha kidogo kidogo katika kila mwaka wa bajeti ya serikali huku kazi ikifanywa kwa mtindo wa zimamoto.

KIMARA KOROGWE - KILUNGULE EXTERNAL
Barabara ya Kimara -Korogwe - Kilungule External (Mandela) inatajwa kuwa na umbali wa kilomita tisa na uboreshaji wake utahusisha pia uwekaji lami kwa awamu.

Evord Urassa, mkazi wa Kimara, anasema sehemu kubwa ya barabara hiyo kwa sasa imeshindiliwa udongo tu unaotifuliwa na wala si changarawe, hali inayoifanya isiwe imara na kupitika kwa kipindi chote cha mwaka.

"Hivi karibuni niliona wakiweka kifusi cha changarawe katika eneo la Kilungule A na B hadi njiapanda ya Makoka kutokea River Side, Ubungo. Eneo hilo lilikuwa korofi na nyakati za mvua halipitiki kutokana na utelezi... tulitarajia wataimarisha barabara yote, lakini hawakufanya hivyo,” anasema.

Anasema utengenezaji unafanyika kwa vipande vipande na kuweka viraka huku katika makutano ya barabara hiyo na ile ya Mawenzi barabara ikiwa ni nyembamba sana, yenye mchanga mwingi na nyakati za mvua huwa haipitiki.

"Haihitajiki elimu ya chuo kikuu kujua barabara inayotengenezwa vizuri. Ninachoshangaa ni kuwa udongo unaotifuliwa na greda unashindiliwa tena na hatuoni changarawe zikiwekwa,” anasema.

KIGOGO - JANGWANI (YANGA)
Hii ni barabara nzuri pia miongoni mwa zile za pembezoni mwa mji kwa ajili ya kupunguza foleni. Inatajwa kuwa na urefu wa kilomita 2.7 na fedha zilizokadiriwa kukamilisha ujenzi wake ni Sh. bilioni 7.6.

Baadhi ya wananchi wamekubali kubomoa nyumba zao baada ya kukubali kupokea fidia waliyopewa.

Wengine wamegomea fidia kwa sababu mbalimbali ikiwamo ile ya kupinga kulipwa eneo walau nusu la nyumba iliyobomolewa na sehemu iliyobaki kutolipwa.
Hadi sasa kuna kesi zinaendelea kunguruma mahakamani.

Kwa ujumla, matengenezo yanaendelea kwa uwekaji wa kifusi cha changarawe huku kazi ya ujenzi wa kiwango cha lami ikiishia Jangwani hadi njiapanda ya daraja la kuelekea Kigogo.

“Kama unavyoona wapo waliobomoa, sisi mwenye nyumba wetu kabomoa nusu baada ya kulipwa kiasi cha fedha na sehemu ndiyo hii imebaki tumepangishwa, wengine wamevunja ndiyo maana unaona maeneo ya wazi na wengine wamefungua kesi kwa madai ya kutoridhishwa na fidia,” anasema Anastanzia Adrian, mkazi wa Mchikichini Bondeni.

Kwa kiasi kikubwa, barabara hiyo imekamilika licha ya wengine kutobomoa nyumba zao, ujenzi unaendelea na upanuzi wake umefanyika.

Mwaka 2010, serikali ilitangaza kutumia Sh. bilioni 15 kuwalipa fidia wananchi watakaoathiriwa na ujenzi huo wa barabara ya Jangwani-Kigogo hadi Ubungo Maziwa, ikiwa ni jitihada za serikali katika kupunguza foleni.

Julai mwaka huu, Waziri Dk. John Magufuli, alitembelea barabara hizo na kukaririwa na vyombo vya habari akisema ujenzi utaendelea licha ya wakazi sita kufungua kesi mahakamani.
Dk. Magufuli alisema ujenzi huo ulitakiwa kukamilika miaka mwili iliyopita, lakini licha ya kulipwa fidia ya awali wakazi hao walifungua kesi nyingine kudai kuwa fidia ni ndogo na kumuagiza mkandarasi kuendelea pasipo kubomoa nyumba ya mtu.

Mhandisi mshauri wa mradi, Mussa Ally, alisema ni mwaka wa tatu eneo hilo halijatengenezwa kwani kuna nyumba 13 zilizopimwa na kufanyiwa tathmini ya Sh. billioni 3.8, lakini wamiliki sita walidai fedha ni kidogo na kwenda mahakamani.

YOMBO VITUKA - DAVIS CORNER
Mkandarasi anaendelea vema na kazi kwenye barabara hiyo ya urefu wa kilomita 10.3 licha ya baadhi ya wakazi kugoma kubomoa nyumba zao. Waliotahiminiwa majengo yao walilipwa fidia ya Sh. billioni 15.8 na wengine wamegomea na kwenda kushtaki mahakamani.

KAULI YA TANROADS MKOA
Meneja miradi wa Wakala wa Barabara mkoa wa Dar es Salaam (Tanroads), Mhandisi Humphrey Kanyenye, anasema mchakato wa manunuzi na uteuzi wa makandarasi upo kwenye hatua za mwisho na kwamba, wakati wowote watepewa barua (letter of acceptance).

Anasema barabara ya Kimara Korogwe - Kilungule itajengwa kwa kiwango cha lami kwa kilomita tatu kuanzia External hadi eneo la Majichumvi na kazi ilitarajiwa kuanza mwezi huu.

Ujenzi wa kilomita tatu ni Sh. bilioni 3.5, mradi ni wa miezi 12 na mradi wote ni wa miaka zaidi ya mitatu kutegemeana na upatikanaji wa fedha.

FEDHA ZAKWAMISHA KIMARA – KINYEREZI
Anaongeza kuwa barabara ya Kimara - Kinyerezi yenye urefu wa kilomita 6.8, usanifu wake umekamilika, lakini hivi sasa hakuna fedha za kutekeleza mradi huo ambao serikali imepania kuukamilisha kwa kiwango cha lami.

Anasema barabara ya Mbezi Malamba Mawili – Kinyerezi –Banana yenye urefu wa kilomita 14, usanifu wake umekamilika lakini ujenzi wa kiwango cha lami utafanyika kwenye umbali wa kilomita nne, eneo la Kinyerezi hadi Kifuru.

Anasema barabara hiyo na ile ya External – Dampo –Vingunguti na Kimara Korogwe-Kilungule hadi External, zabuni zake zilishatangazwa na makandarasi wakajitokeza kuomba, lakini wote walipeleka makadirio ya juu sana na kuilazimu Tanroads kurudia upya zoezi hilo.

Anasema tararibu za manunuzi zinachukua siku 70 tangu kutangazwa hadi kumpa mkandarasi kazi.

Anasema zabuni za barabara za Tegeta Kibaoni - Wazo, Kimara Baruti - Msewe na Tangibovu - Goba zilitangazwa pia Julai mwaka huu.

Anaongeza kuwa barabara ya Mbezi - Malambamawili - Kinyerezi - Banana iko kwenye hatua za mwisho na mkandarasi amepatikana isipokuwa bado hajapewa barua rasmi na matarajio ni kuanza ujenzi mwishoni mwa mwezi huu.

Mhandisi Kanyenye anasema barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill, Goba - Mbezi Mwisho yenye urefu wa kilomita 20, ujenzi utaanza kwenye umbali wa kilomita saba, ukianzia Mbezi Mwisho kuelekea Goba.

Anasema mkandarasi ameshapatikana na ujenzi utagharimu Sh. bilioni 13. Itakamilika ndani ya miezi 16 na ujenzi wake unatarajiwa kuanza mwezi huu.

Barabara ya Tangibovu au Samaki Wabichi - Goba yenye urefu wa kilomita tisa, usanifu wake ulifanyika na mkandarasi kupatikana.

Itajengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh. bilioni 16 kwa miezi 18.
Barabara ya Kimara Baruti - Msewe yenye urefu wa kilomita 2.6 itajengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 4.6 na muda wa kukamilika kwake ni miezi nane.

"Ujenzi wa barabara hii una changamoto nyingi kutokana na wananchi kujenga makazi hadi kwenye hifadhi ya barabara. Kilichofanyika ni mkandarasi kutakiwa kufanya upembuzi yakinifu ili kuona ni watu wangapi watalipwa fidia kwani siyo wote watakaolipwa,” anasema.

Anasema mkandarasi ndiye atakayewasilisha michoro ya barabara na ndipo itajulikana nani anastahili kulipwa fidia ili kupisha ujenzi huo.
Anasema barabara ya Tabata Dampo yenye urefu wa kilomita 1.6 itajengwa kwa miezi minane kwa gharama ya Sh. bilion 5.7.

Anaongeza kuwa kinachoendelea sasa ni matengenezo ya kawaida na kwamba barabara hiyo ina changamoto nyingi kutokana na kujengwa juu ya uso wa ardhi uliojaa rundo la uchafu na mkandarasi atapaswa kuiongezea uimara kwa kuijaza kwa mita mbili zaidi. “Hivi sasa tuko kwenye hatua za mwisho za manunuzi,” anasema.

Kuhusiana na Barabara ya Kigogo - Jangwani (Yanga), baada ya kuona baadhi ya wakazi wamegoma kubomoa nyumba zao kwa madai ya fidia kuwa ndogo, mkandarasi aliambiwa ajenge barabara kulingana na eneo lililopo na baada ya kupima ilionekana kuwa upana unatosha ikiwa ni pamoja na kuweka mitaro.

Barabara ya Jet Corner-Yombo, mkandarasi yupo kazini licha ya kuwapo watu waliofungua kesi mahakamani wakitaka kulipwa zaidi kwa madai kwamba fidia iliyokadiriwa awali ni ndogo.

CHANGAMOTO ZA FIDIA, MANUNUZI
Kanyenye anasema sheria inasema huwezi kulipa fidia nusu bali kwa nyumba yote na yapo maeneo ambako fidia hulipwa kwa mita za mraba na wapo ambao huomba kulipwa nusu kwa kuwa eneo linalobaki linaweza kutumika kwa shughuli nyingine kama kufungua maduka.

“Wapo wanaolipwa nusu kulingana na mahitaji yake, wengine huwataka Tanroads kuchukua eneo la kutosha ujenzi wa barabara tu na jingine wamuachie kwa biashara zake, na wanaolalamika ni wale walio nyuma ya nyumba zilizobomolewa nusu kwa kudai wanazibwa kwani walipaswa kuwa barabarani baada ya wenzao wa mbele kuondolewa,” anasema. Kanyenye anaongeza kuwa matengenezo yanayofanyika sasa kwenye barabara hizo ni ya kawaida kwani Tanroads haiwezi kusubiri mkandarasi bali ni wajibu wao kuhakikisha kuwa barabara hizo zinapitika kwa wakati.

BARABARA ZA JUU (FLY OVERS)
Barabara za juu zilizoahidiwa kujengwa ni pamoja na kwenye makutano ya Mandela na Morogoro eneo la Ubungo na Mandela na Nyerere, eneo la Tazara.

Kanyenye anasema mhandisi mshauri amepatikana kwa ajili ya kufanya usanifu.
Hata hivyo, michoro haijaandaliwa lakini mhandisi mshauri anatakiwa kuangalia ni ipi inafaa.

Anasema kwa hali ya barabara za jiji la Dar es Salaam hivi sasa kulinganisha na magari yaliyopo, zinatakiwa barabara za juu katika makutano ya barabara za Mwenge, Chang’ombe, Tabata, Morocco, Kamata na Magomeni.

Anasema wajibu wa Tanroads mkoa ni kuondoa miundombinu ya umeme na maji kwenye maeneo hayo hadi kufikia Mei 2014 kabla ya kuendelea kwa hatua nyingine.

TANROADS WAKIRI FOLENI BALAA
Mhandisi Kanyenye anathibitisha kuwa hali ya foleni katika jiji la Dar es Salaam ni mbaya na kwamba naye anaathiriwa sana na foleni kwani makazi yake yapo Kibamba.

Anasema kuwa hutumia usafiri wake, akiondoka nyumbani kwake saa 12:00 na kufika ofsini saa 1:40 asubuhi huku akikadiria kuwa mtu anayetumia usafiri wa umma (daladala) hufika kazini kwake katika maeneo ya katikati ya jiji saa 2:00 asubuhi ikiwa ataondoka Kibamba saa 11:00 alfajiri.

“Unafika ofisini wakati akili ikiwa imeshaanza kuchoka, unafanya kazi hadi saa 6 mchana, unajikuta tayari unaanza kusinzia, unafika nyumbani usiku wakati watoto wakiwa wamelala, mahusiano ya kifamilia nayo yanatetereka... na unapokosa amani nyumbani huwezi kufanya kazi vizuri,” anasema.

Anasema kwa wanaotumia barabara za pembezoni magari yanaharibika haraka kwa vile barabara zake bado hazijawa katika hali nzuri.

“Kwenye janga la foleni hakuna anayepona. Uwe na gari na usiwe nalo, wote mko sawa tu. Ni vyema serikali ikaharakisha mpango wa ujenzi wa barabara za juu kwani tunaamini kuwa utasaidia sana kupunguza matatizo haya,” anasema.

DANADANA TANROADS MAKAO MAKUU
Oktoba 23 mwaka huu, NIPASHE ilipeleka maswali kadhaa kwenye ofisi za Tanroads makao makuu kwa nia ya kupata ufafanuzi kuhusiana na maendeleo ya mradi wa barabara za pembezoni jijini Dar es Salaam (ring roads) kwa nia ya kupunguza tatizo la foleni. Cha kushangaza, kukawa na danadana kubwa katika utoaji wa majibu, hali inayoonekana kutolingana na hadhi ya ofisi hiyo inayotarajiwa kuwa kinara wa kuendesha mambo yake kwa weledi.

Kwa mfano, Novemba 4 mwaka huu, mwandishi alikwenda ofisini kwao kuulizia majibu ya maswali yaliyotumwa kwao kwa kufuata utaratibu walizoelekeza wenyewe hapo kabla. Msemaji akamtaka mwandishi aende kwa katibu muhtasi wa Mtendaji Mkuu.

Kufika huko, katibu muhtasi naye alimtaka mwandishi kwenda kwa katibu muhtasi wa meneja miradi.
Mwandishi alikutanishwa na meneja miradi huyo aitwaye Rajabu Manga, aliyewasiliana kwa simu na ofisi ya Mtendaji Mkuu na kuelezwa kuwa majibu yapo, lakini bado hayajasainiwa na (Mtendaji huyo). Rajabu akamtaka mwandishi kuondoka na atajulishwa kwa njia ya simu kuhusiana na majibu hayo.

Wiki moja baadaye (Novemba 11), mwandishi alikwenda kwenye ofisi hizo na kabla ya kuingia alikutana na Rajabu, lakini baada ya kusalimiana, akamuelekeza kwenda kwa katibu muhtasi wa Mtendaji wa Tanroads kwa kuwa majibu yalishakuwa tayari.

Kufika huko, mwandishi akaambiwa arudi tena kwenye ofisi ya Rajabu, ambaye naye alipoambiwa habari hiyo, akasema aulizwe Mtendaji kwani yeye hahusiki. Siku inayofuata ambayo ni Novemba 12, mwandishi aliwasiliana tena na Rajabu kutaka kujua kulikoni wamekuwa wakimpiga danadana kwa masuala yanayoonekana kuwa ndani ya uwezo wao, lakini aliruka na kusisitiza kuwa anayepaswa kuulizwa ni bosi wake, yaani Mtendaji Mkuu wa Tanroads.

“Sikiliza mwandishi. Siwezi kumlazimisha bosi wangu asaini majibu ya maswali... mimi ni Meneja Miradi, yeye ni Mtendaji Mkuu, muulize kwa nini hakupi majibu,” alisisitiza Rajabu kisha akakata simu.

Kurudi tena kwa Mtendaji Mkuu, katibu wake muhtasi aliendelea kuwa kikwazo. Hakutoa fursa hata chembe ya kumuona bosi wake na badala yake akasisitiza kuwa mwandishi arudi kwa Meneja Miradi, Rajabu.

WAZIRI MAGUFULI
Waziri wa ujenzi, Dk. John Magufuli, anasema serikali imedhamiria kumaliza tatizo la foleni na ndiyo maana imetenga fedha za kutosha na kwamba barabara zote (za ring roads) zitaendelea kujengwa mwakani. Anasema katika barabara za juu, usanifu umeshakamilika na zimetengwa Sh. bilioni 100 kwa kazi hiyo huku Serikali ya Japani ikikubali kutoa Sh. bilioni 79 na itahusika katika ujenzi ambao michora yake imeshakuwa tayari.

Anasema serikali pia inatarajia kuleta kivuko kikubwa kitakachofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, na kwamba kutakuwa na vituo saba.

CHANZO NI NIPASHE

No comments:

Post a Comment