I: UTANGULIZI
a) Masuala ya Jumla
Mheshimiwa Spika,
1. Ni
jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa
kutufikisha salama siku ya leo. Tumekuwepo hapa Dodoma kwa takriban siku
15 za kazi ambapo tumeweza kutekeleza majukumu na kazi za Mkutano wa 14
wa Bunge lako Tukufu ambapo tunahitimisha shughuli zilizopangwa hivi
leo.
Mheshimiwa Spika,
2. Nitumie
nafasi hii ya mwanzo kabisa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Asha
Rose Migiro, (Mb.) kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika
Bunge lako Tukufu. Wengi wetu tunafahamu uwezo mkubwa wa Dkt. Asha Rose
Migiro na bila shaka ndiyo sababu Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi wa
kumteua kuwa Mbunge kwa kuzingatia sifa nzuri alizonazo. Pamoja na kumpongeza napenda kumtakia kazi njema ndani na nje ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika,
3. Tangu Mkutano wa 13 wa Bunge baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamepotelewa na Ndugu, Jamaa na Marafiki. Napenda
kutumia fursa hii kuwapa pole wote waliofikwa na misiba hiyo. Lakini
katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili
Azimio la Bunge kuhusu kuungana na Nchi ya Afrika Kusini, katika
kuombeleza kifo cha Muasisi, Mpinga ubaguzi wa rangi, Rais wa Kwanza
Mweusi wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Madiba Mandela kilichotokea
tarehe 5 Desemba 2013. Wote tunakubaliana kwamba huu ni msiba Mkubwa
kwa Dunia nzima na hasa kwa wale wanaomfahamu Mzee Mandela na historia
yake.
4. Aidha,
nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuwakilisha vyema Watanzania wote
katika msiba huu mkubwa wa Afrika na Dunia nzima. Hotuba ya Mheshimiwa
Rais aliyoitoa wakati wa mazishi ya Hayati Nelson Mandela tarehe 15
Desemba, 2013 pale Qunu ilitosha kabisa kuitangaza Tanzania Dunia nzima
katika ushiriki wake kwenye harakati za ukombozi Barani Afrika katika
Karne ya 20. Ninaamini kwamba hiyo ni Historia ambayo haitafutika
vizazi vingi vijavyo. Tutaendelea kumuenzi Mzee Mandela kwa kuiga na
kufuata nyayo zake.
b) Maswali
Mheshimiwa Spika,
5. Katika
Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kuuliza maswali ya msingi 170
na ya nyongeza 458 ambayo yote yalijibiwa na Serikali. Aidha, maswali
17 ya msingi na 15 ya nyongeza yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya
Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa
kuuliza maswali mazuri na Waheshimiwa Mawaziri kutoa majibu ya maswali
hayo kwa umahiri mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
6. Pamoja na shughuli hizo za kawaida, Bunge lako lilikamilisha kazi kubwa zifuatazo:
Kwanza: Bunge lilijadili na kukamilisha Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013. [The Referendum Bill, 2013];
Pili: Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge za Sekta Mtambuka.
Tatu: Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge zinazosimamia Fedha za Umma; na
Nne: Kujadili Taarifa Tisa (9) za Kamati za Bunge za Kisekta.
7. Aidha,
Bunge lako Tukufu lilijadili kwa utaratibu wa Hati ya Dharura Muswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa wa Mwaka 2013 [The Excise (Management and Tariff) (Amendment) Bill, 2013]. Mwisho Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 ulisomwa kwa mara ya kwanza.
8. Nitumie
nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kujadili Taarifa
hizo na kutoa maoni na ushauri kwa uwazi mkubwa na kwa kina. Mapendekezo
na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge umepokelewa na Serikali na
utazingatiwa kwa uzito unaostahili.
II: KILIMO
a) Hali ya chakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
9. Kama
nilivyoeleza katika Mkutano wa Bunge wa 13, hali ya upatikanaji wa
Chakula Nchini kwa ujumla imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo
mengi kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa Kilimo wa 2012/2013 katika
maeneo mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya chakula na lishe iliyofanyika
mwezi Oktoba na Novemba, 2013 katika maeneo yenye matatizo ya usalama
wa chakula na lishe inaonesha kuwa jumla ya Watu 828,063 wanakabiliwa na
upungufu wa chakula na watahitaji msaada wa chakula wa Tani 23,312 hadi
ifikapo mwezi Februari 2014. Aidha, kati ya mwezi Julai na Novemba
2013, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulitenga jumla ya
Tani 16,119 za chakula cha mgao kwa Halmashauri zenye mahitaji ya
chakula cha msaada. Hadi kufikia tarehe 16 Disemba 2013, jumla ya Tani
13,716 zilikwishachukuliwa na Halmashauri husika. Tani 2,402 zilikuwa
hazijachukuliwa na Halmashauri za Mwanga, Babati, Igunga, Mpwapwa na
Manyoni.
10. Ninawaagiza
Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ambazo hazijachukua chakula hicho
kufanya hivyo kabla ya tarehe 15 Januari 2014. Ambao hawatatekeleza
maagizo haya watachukuliwa hatua za kisheria. Nitumie nafasi hii
kuwahakikishia Wananchi kuwa Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji
wa chakula katika Halmashauri zenye hali tete ya chakula kwa lengo la
kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula.
b) Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
11. Kutokana
na miezi hii kuwa katika kipindi cha mwisho wa msimu wa ununuzi wa
mazao, kiasi cha mazao yanayoingia sokoni kimeanza kupungua. Hali hii
imesababisha bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika
soko hapa Nchini kuanza kupanda ingawaje si kwa kiasi kikubwa. Kwa
mfano, bei ya mahindi Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 536.86 kwa kilo
mwezi Oktoba, 2013 hadi kufikia Shilingi 538.26 kwa kilo mwezi Novemba,
2013. Kwa upande wa Mchele, bei ya wastani wa Kitaifa imepanda kutoka
Shilingi 1,188.60 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi Shilingi 1,191.10 kwa
kilo mwezi Novemba, 2013.
12. Pamoja
na kuwepo kwa hali ya kupanda kwa bei, bado bei za sasa kwa baadhi ya
mazao mfano mahindi, mchele, maharage na viazi ziko chini ikilinganishwa
na zile za kipindi kama hiki mwaka jana. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa
yenye mavuno mazuri kuendelea kuwahamasisha wakulima kuhifadhi chakula
cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao na kuuza ziada katika Soko ili
kusaidia kupunguza bei ya vyakula katika miji yetu. Halmashauri
zihakikishe kuwa zinathibiti ununuzi holela wa chakula kutoka mashambani
na majumbani mwa Wakulima kwa lengo la kujihakikishia upatikanaji wa
chakula cha kutosha.
c) Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa
Mheshimiwa Spika,
13. Serikali
kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ilipanga kununua Tani
250,000 za nafaka. Wakala umeendelea na kazi hiyo na hadi kufikia tarehe
11 Desemba, 2013, Wakala ulikuwa umekwishanunua kiasi cha Tani 218,499
za nafaka sawa na Asilimia 87.4 ya kiasi kilichopangwa kununuliwa.
Aidha, hadi kufikia tarehe 16 Desemba, 2013, Maghala ya Wakala wa Taifa
wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na akiba ya jumla ya Tani 233,808 za
nafaka. Kati ya hizo, Tani 233,315 ni za Mahindi na Tani 493 ni za
Mtama.
14. Wakati
huo huo, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unaendelea kuhamisha
chakula kutoka katika maghala yake yaliyoko katika Mikoa iliyozalisha
ziada kwenda kwenye maghala yaliyoko kwenye Mikoa yenye upungufu wa
chakula ili kukabiliana na mahitaji ya chakula cha msaada
kitakachohitajika kusambazwa kwa walengwa. Hadi kufikia tarehe 9
Desemba, 2013, jumla ya Tani 44,129 za Mahindi zimekwishahamishwa.
Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara kununua chakula katika
Mikoa yenye ziada ya chakula na kukipeleka katika Mikoa yenye upungufu
wa chakula.
d) Hali Halisi ya Usambazaji wa Pembejeo
Mheshimiwa Spika,
15. Kama
nilivyoeleza katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali ilichapisha jumla
ya vocha 2,796,300, kwa ajili ya pembejeo za Kilimo kwa msimu wa Kilimo
wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 12 Desemba, 2013, Tani 74,925 sawa na
Asilimia 96 za mbolea ya kupandia na Tani 42,295 sawa na Asilimia 91 ya
mbolea ya kukuzia zilikuwa zimekwishafikishwa katika Mikoa husika
kulingana na aina ya mazao yanayohitaji mbolea hizo. Aidha,
Maghala ya Wakala wa Mbolea Jijini Dar es Salaam yana akiba ya kutosha
ya mbolea hiyo. Nirejee kutoa wito kwa Wakuu wote wa Mikoa kuhakikisha
kuwa vocha zote zinatolewa kwa walengwa kwa wakati sambamba na aina ya
pembejeo inayomlenga Mkulima husika kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.
e) Malipo ya Madeni ya Wakulima ya Mahindi.
Mheshimiwa Spika,
16. Katika
mwaka wa 2013/2014, Serikali ilitenga jumla ya Shilingi Bilioni 109.6
kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya kununua
Tani 250,000 za nafaka. Hadi kufikia tarehe 19 Desemba, 2013 NFRA
ilikuwa imenunua jumla ya Tani 218,499 zenye thamani ya Shilingi
Bilioni 109.25 na kwa ajili hiyo. Kutokana na Serikali kutoa bei nzuri
ya wastani wa Shilingi 500/= kwa kilo ya mahindi, zoezi hilo lilikuwa na
matokeo mazuri katika msimu huu kulinganisha na miaka iliyopita na
liliwavuta Wananchi wengi kupeleka nafaka katika Vituo vya kununulia
nafaka. Hadi sasa Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 100.6 kwa ajili ya
zoezi hilo na imehakikisha kuwa wananchi wote waliouza nafaka zao kwa
NFRA wamelipwa fedha zao. Aidha, natambua kuwa NFRA ilitumia baadhi ya
Wakala kukusanya nafaka hiyo kutoka kwa Wakulima na kama nilivyosema
katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali inatambua kuwa Wakala hao kutoka
Mikoa ya Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga, Ruvuma, Rukwa na Tanga
wanaidai Serikali jumla ya Shilingi Bilioni 8.65 Niwaombe Wakala wote
wanaoidai Serikali kuendelea kuwa na subira wakati Serikali inaendelea
na utaratibu wa kulipa deni hilo kwa vile kiasi cha deni lao lipo ndani
ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ununuzi wa nafaka katika mwaka wa fedha
wa 2013/2014.
III: MPANGO WA HUDUMA JUMUISHI ZA KIFEDHA
Mheshimiwa Spika,
17. Tarehe 12 Desemba, 2013 Serikali ilizindua Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (yaani National Financial Inclusion Framework).
Uzinduzi wa Mpango huu ulifanywa na Malkia wa Uholanzi Mheshimiwa
Máxima Zorreguieta Cerruti ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Mpango wa Huduma Jumuishi za Kifedha na
kushuhudiwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal na
Wawakilishi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa.
Mheshimiwa Spika,
18. Lengo
la Mpango huo ni kusimamia ukuzaji wa huduma za kifedha kwa jamii
Nchini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya Fedha.
Vilevile, Mpango unalenga kusogeza huduma karibu kwa jamii pana zaidi ya
Watanzania kwa kutumia mifumo ya Teknolojia mbalimbali katika kufikisha
huduma za kifedha kwa Wananchi na hasa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi
waliopo Vijijini ambao wengi wao wako nje ya mfumo rasmi wa kifedha.
Teknolojia hizo ni pamoja na:
(a) Huduma za Kibenki za moja kwa moja na kupitia Wakala (Agent Banking);
(b) Huduma za kifedha kupitia Mitandao mbalimbali kama vile M-PESA, TIGO PESA, AIRTEL MONEY na Easy PESA.
(c) Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (Point of Sales – POS).
19. Aidha,
Mpango huu utaweka mazingira linganifu na yaliyo bora kwa kutumia
Sayansi na Teknolojia kutekeleza Sera ya Fedha kwa ufanisi, kuimarisha
Sekta ya Fedha katika Pato la Taifa na Kukuza Uchumi kwa ujumla. Mpango
huu pia utawezesha kuongeza kasi ya upatikanaji wa Chakula, masuala ya
Lishe na Maendeleo Vijijini kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
20. Utafiti
uliofanywa na Benki ya Dunia katika Nchi mbalimbali Barani Afrika
unaonesha kuwa Watu wanaonufaika na Mfumo rasmi wa Taasisi za Kifedha ni
Asilimia 24 tu. Kwa upande wa Tanzania, Wananchi waliopo kwenye Mfumo
rasmi wa Asasi za Kifedha ikijumuisha wale waliojiunga na Vyama vya
Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOs) ni Asilimia 22. Asilimia 78 ya
Watanzania wapo nje ya Mfumo wa Kifedha na wengi wao ni kutoka Vijijini
hasa Wakulima wadogo. Mpango huu wa Huduma Jumuishi za Kifedha unalenga
kufikia Asilimia 50 ya Watu wazima wanaotumia huduma rasmi za kifedha
ifikapo mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika,
21. Kiwango hiki kidogo cha Wananchi walio katika Mfumo rasmi wa huduma za kifedha unatokana na changamoto zifuatazo:
Moja:
Miundombinu ya kuanzisha huduma za Kifedha Vijijini ni hafifu hususan
barabara, mawasiliano, makazi na huduma za kiusalama;
Mbili: Wananchi wengi wa Vijijini bado hawajahamasishwa kutambua umuhimu na faida ya huduma za kifedha. Aidha, utamaduni wa kujiwekea akiba na kukopa ni mdogo; na.
Tatu:
Taasisi nyingi za kifedha zinaogopa kwamba Wananchi wengi wa Vijijini
ambao ni Wakulima hawana fedha za kutosha kuweza kuweka akiba katika
Taasisi hizo na uwezo wao wa kukopa mikopo ni mdogo, hivyo wakipeleka
huduma zao huko hawatapata faida.
Mheshimiwa Spika,
22. Zipo
faida nyingi za kueneza Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Wananchi wengi
wa Vijijini hasa Wakulima. Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na:
Moja:
Kuwezesha Wananchi kujiwekea Akiba na pia kupata mikopo ya kuwawezesha
kuanzisha miradi ya maendeleo na shughuli nyingine za kijamii hivyo
kujiongezea kipato na kuondoa umaskini;
Mbili:
Huduma za Kifedha Vijijini zinawawezesha Wananchi wengi hasa Wakulima
kupata mikopo ya pembejeo na mikopo ya ununuzi wa mazao;
Tatu: Huduma
za Kifedha Vijijini ni Mkombozi wa Makundi maalum kama vile Vijana,
Wanawake, Wazee, na Walemavu. Aidha, zinasaidia Wananchi kujiongezea
kipato, kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya Kilimo na kuongeza
thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na ufugaji nyuki; na
Nne: Kuwepo
kwa Huduma za Kifedha Vijijini kunaongeza Usalama wa Chakula, kulinda
mazingira na kufanya Vijiji kuwa ni sehemu nzuri ya kuishi.
Mheshimiwa Spika,
23. Serikali
imeonesha juhudi kubwa katika kuanzisha Huduma Jumuishi za Kifedha
Nchini kwa mfano tumeweza kuanzisha Benki nyingi Nchini. Tayari tunazo
Benki takriban 52 zenye matawi zaidi ya 609 kote Nchini. Lakini pia
tunazo huduma za Bima kwa Makampuni Binafsi zaidi ya 27 na Mawakala wa
Bima takriban 600. Ipo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Umma 5, Masoko ya
Mitaji na Vikundi na Taasisi ndogondogo za Fedha (SACCOS) takriban
5,600.
24. Aidha
tunazo huduma za Kifedha kwa kutumia Huduma za Kifedha kupitia mtandao
(PESA – MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (POINTS OF SALES
– POS). Inakadiriwa kuna Mawakala na Vituo zaidi ya 55,000 ambapo
Waajiriwa wa moja kwa Moja (Direct Employment) wanakadiriwa kufika takriban 100,000.
Mheshimiwa Spika,
25. Maisha
bora kwa kila Mtanzania ni pamoja na kutumia Teknolojia na kurahisisha
maisha. Kwa mfano, huduma za M-PESA peke yake zinawezesha malipo kwenye
biashara mbalimbali zaidi ya aina 300 ikiwemo manunuzi kwenye
Supermarket na maduka ya kawaida. Huduma hizo ambazo zinatolewa pia kwa
njia ya TIGOPESA, AIRTEL MONEY, EASY PESA zinaweza kulipia Luku, Ada za
shule na Vyuo, Tiketi za ndege, kufanya marejesho Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu, n.k. Aidha, baadhi ya Makampuni haya yameunganisha huduma
zao na Benki zaidi ya 20 ikiwemo CRDB, NMB, Benki ya Posta, Standard
Chartered, Amana Bank na Diamond Trust Bank (DTB). Vilevile, kwa kutumia
huduma za jumuishi za kifedha mteja anaweza kuhamisha fedha kutoka
Akaunti ya Benki kwenda M- PESA, TIGO PESA n.k. halafu akazitoa kupitia
Wakala. Kwa sasa Watumishi walio Vijijini hawana tena sababu ya kufunga
Ofisi kufuata mishahara Benki bali kupitia huduma hizi za Kifedha na wanaweza kutoa pesa kupitia Wakala, na kwa kufanya hivyo ufanisi na tija kwa Watumishi unaongezaka.
Mheshimiwa Spika,
26. Ni
kweli kwamba tunayo kazi kubwa ya kutekeleza Dhana ya Huduma Jumuishi
za Kifedha Nchini. Lakini ni ukweli kuwa Uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa
wa Huduma Jumuishi za Kifedha una manufaa makubwa na mengi ikiwemo
kuongeza kasi ya Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini kwa kupeleka
maendeleo Vijijini, kuongeza Akiba ya Chakula na pia kufikia malengo ya
Milenia. Ni matumaini yangu kwamba uzinduzi wa Mpango huu utatuwezesha
kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi. Natoa wito kwa Mabenki, Taasisi za
Kifedha na Vituo vya Kifedha kupitia mitandao (PESA MTANDAO) na Vituo
vya malipo kwa kutumia Wakala kuongeza jitihada katika kusambaza huduma
za Kifedha Vijijini ambako ndiko kwenye kundi kubwa la Wananchi
wanaohitaji huduma hiyo.
IV: NISHATI NA MADINI
a) Mradi wa Gesi
Mheshimiwa Spika,
27. Kama
ambavyo Wananchi wengi wanafahamu, Serikali kupitia Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea kutekeleza mradi wa
ujenzi wa mitambo ya kusafishia Gesi Asilia katika maeneo ya
Madimba, Mtwara Vijijini na Songo Songo Wilayani Kilwa. Pia ujenzi
wa Bomba la kusafirishia Gesi hiyo kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar
es Salaam unaendelea vizuri. Mradi huu utakapokamilika utaunganisha
maeneo yanayozalisha Gesi Asilia hususan Mnazi Bay-Mtwara, Songo Songo,
Kisiwani, Mkuranga, Ntorya na maeneo yaliyogunduliwa Gesi katika eneo la
bahari ya kina kirefu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Gesi
Asilia mbali na matumizi mengine, inatumika katika kuzalisha umeme ambao
kwa sasa Asilimia kubwa unazalishwa kwa kutumia nishati ya mafuta
yanayoingizwa kutoka Nchi za nje na hivyo kuligharimu Taifa kiasi
kikubwa cha fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika,
28. Katika utekelezaji wa mradi huu, Kazi zifuatazo zimekamilika hadi kufikia tarehe 30 Novemba, 2013:
Moja:
Kukamilika kwa upakuaji wa Shehena ya Sita (6) ya Mabomba ya Mradi
yapatayo 4,444 ya umbali wa Kilomita 51.169 katika Bandari ya Mtwara.
Jumla ya mabomba yaliyowasili Nchini hadi Novemba, 2013 ni 24,935 ya
umbali wa kilomita 295.5;
Pili: Kusafisha Mkuza wa Mabomba, tayari Kilomita 498.5 zimekamilika;
Tatu:
Usafirishaji wa mabomba kutoka kwenye yadi za kuhifadhia na kuyasambaza
kwenye Mkuza tayari kwa kuyaunganisha kwa kuchomelea. Hadi sasa mabomba
ya Kilomita 186.9 yamekwishasafirishwa;
Nne: Uchimbaji wa njia ya kuweka bomba, yenye umbali wa Kilomita 27.0 umekamilika;
Tano: Uwekaji wa mabomba kwenye njia yake sambamba na kuweka Mkongo wa Mawasiliano (Fiber Optic Cable) umekamilika Kilomita 21.1;
Sita:
Kufukia bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano. Tayari Kilomita 7.30
za Bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano zimefukiwa; na
Saba: Utafiti wa njia ya Bomba la Baharini nao umekamilika.
Hayo ni maeneo machache ambayo nimeona niyataje.
Mheshimiwa Spika,
29. Ni
kweli kwamba kazi za mradi huu ni kubwa lakini kwa ujumla zinaendelea
vizuri na kwa kasi. Moja ya faida za mwanzo za mradi huu ambazo
tumeziona ni pamoja na upatikanaji wa ajira kwa Wafanyakazi wa Mradi
ambao sehemu kubwa ya ajira ni ushirikishwaji wa wazawa katika Mradi wa
Gesi na Mafuta. Kwa kuwa kazi za ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi ni
za kitaalamu sana, malengo ya Shirika la Petroli Nchini (TPDC) ni
kuajiri wafanyakazi Wakiwemo Wazawa mapema ili waweze kushiriki na
kujifunza kwa vitendo shughuli zote zinazohusiana na ujenzi wa mitambo
na Bomba la Gesi hatua kwa hatua, tangu mwanzo hadi mwisho wa ujenzi.
Utaratibu huu utasaidia kupata wataalamu wazuri na wazoefu wa Kitanzania
watakaoendesha (operations) na kufanya matengenezo (Maintenance) ya mitambo na Bomba la Gesi kwa kipindi chote cha matumizi.
Mheshimiwa Spika,
30. Vilevile
moja ya makubaliano katika Mkataba wa utekelezaji wa Mradi huu,
Mkandarasi anawajibika kuwapeleka Wafanyakazi kwenye mitambo na mabomba
yanayofanya kazi kwa sasa kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja ili
wajifunze pia kwa vitendo na kwa nadharia shughuli zote za kuendesha
mitambo ya kusafisha Gesi Asilia na Bomba la Gesi. Malengo ya TPDC ni
kuwapeleka wafanyakazi husika kwa awamu tofauti tofauti wakati wa
kipindi cha ujenzi ili ikifika kipindi cha kukabidhi mradi Wafanyakazi
wote wawe wamekwishapata uzoefu wa kutosha.
Mheshimiwa Spika,
31. Kampuni
nyingi zilizopo Mtwara zinazojishughulisha na mambo ya utafiti na
uzalishaji wa Gesi na Viwanda vinavyohusiana na matumizi ya Gesi,
zimekuwa zikisomesha na pia kuajiri wazawa. Kwa mfano, Mpango wa kujenga
mitambo ya kutengeneza Gesi kuwa kimiminika (LNG) wa Kampuni ya British Gas Tanzania utakuwa
na utengenezaji wa ajira nyingi za kiwango kuanzia Kada ya Chini na
Kada ya Kati ambayo itasomesha Watanzania kupitia VETA katika fani
mbalimbali. Wako watakaosomeshwa katika fani ya Vyuma, wengine ujenzi,
uhandisi wa miundombinu na ufundi wa vyuma na umeme.
32. Katika
Kada ya Kati, Kampuni ya Gesi Tanzania wanatarajiwa kusomesha wataalamu
16,756 waliofaulu vizuri masomo ya Kidato cha Nne. Takwimu zinaonesha
kuwa kwa Mtwara tu, kumekuwapo ajira mpya 400, na Watanzania wanaotoa
huduma mbalimbali kwenye Kampuni za Gesi na Mafuta ni sawa na Asilimia
70 ya watoa huduma hiyo Nchini. Asilimia 30 iliyobaki ya watoa huduma
inatolewa na Wageni.
33. Katika
Kada za Juu, Kampuni itasomesha na kuajiri Wataalamu wa Jiolojia,
Uhandisi, Kemia na Sayansi husika kwenye Gesi na Mafuta. Matokeo
yameanza kuonekana ambapo jumla ya Wanafunzi wa VETA 370 wamesomeshwa
kuhusu Gesi na Mafuta kwa kiwango cha cheti cha Kimataifa na Wanafunzi
12 wa Kada za Juu wamepata ufadhili na wanasomea fani za Gesi na Mafuta
ndani na nje ya Nchi.
Mheshimiwa Spika,
34. Napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Kampuni ya British Gas Tanzania
wamegundua gesi kiasi cha Futi za Ujazo Trilioni 13. Katika kuandaa na
kuendesha mradi wa uzalishaji Gesi nyingi kiasi hicho ni dhahiri kwamba
ajira zitapatikana kwa maelfu ya Watanzania. Katika hatua ya ujenzi,
mradi utatoa ajira kwa maelfu; na katika uzalishaji (operations)
ajira nyingine zaidi kwa maelfu zitapatikana hapa Nchini, na katika
mnyororo wa usambazaji ajira nyingi pia zitajitokeza. Nitumie fursa hii
kuwapa Watanzania matumaini, kwamba Mradi wa Gesi Nchini una manufaa
mengi sana, kuanzia upatikanaji wa Gesi na Ajira kwa Wazawa. Nawaomba
Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwaelimisha Wananchi wetu kuhusu manufaa
ya mradi huu katika Nchi yetu. Ni fursa ya kipekee ambayo Wananchi wetu
wanatakiwa wafaidike nayo katika kuwaletea maisha bora.
V: MATUMIZI YA MASHINE ZA KIELEKTRONIKI (EFDs)
Mheshimiwa Spika,
35. Katika
mwaka wa fedha wa 2013/2014, Serikali ililiarifu Bunge lako Tukufu
kuhusu mikakati mbalimbali itakayotekelezwa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Ndani.
Moja ya hatua hizo muhimu ni kuendelea kuimarisha matumizi ya Mashine za
Kielektroniki za kutoa Risiti (Electronic Fiscal Devices- EFDs).
Mashine hizi zimeunganishwa kwa Mtandao wa Kompyuta moja kwa moja na
Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa lengo la kuwezesha Serikali kupata mapato
stahiki bila udanganyifu. Aidha, Mashine hizi zinasimamiwa kupitia
Mtandao wa Kielektroniki ambapo hupeleka taarifa moja kwa moja kwenye
Hifadhi Kuu ya Kumbukumbu za Mamlaka ya Mapato Tanzania kila siku.
Mheshimiwa Spika,
36. Katika
utekelezaji wa zoezi hili kwa mwaka huu, Serikali imelenga kuingiza
Walipa Kodi 200,000 kati ya 1,500,000 ili waweze kutumia Mashine za
Kielektroniki. Walengwa wa utaratibu huu ni Wafanyabiashara wenye
biashara kubwa zenye Mtaji wa kati ya Shilingi Milioni 14 na Shilingi
Milioni 40. Katika zoezi hili, Wafanyabiashara Wadogo wanaoendesha
biashara zisizo rasmi kama vile Wamachinga na wale wanaotembeza bidhaa
barabarani na Mama Lishe hawahusiki na utaratibu huu hata kidogo.
Mheshimiwa Spika,
37. Katika
utekelezaji wa zoezi hili kumejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya
Wafanyabiashara Nchini hususan wa Mikoa ya Mbeya, Morogoro, Lindi na Dar
es Salaam (Kariakoo) kuhusiana na bei na matumizi ya Mashine hizi.
Malalamiko makubwa ya Wafanyabiashara hao ni kuhusu: Bei kubwa ya
ununuzi wa Mashine za Kielektroniki; Bei kubwa ya Karatasi za kutolea
Risiti; Mchakato uliotumika kununua Mashine za Kielektroniki; Walengwa
wa kutumia Mashine hizo; na Gharama za matengenezo.
Mheshimiwa Spika,
38. Kwa
kuzingatia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa
(ICT); Wataalam wanathibitisha kwamba, Mashine za Kielektroniki
zinafanya kazi zifuatazo:
Moja:
Zinatoa Risiti na Ankara za Kodi kwa urahisi na Mfanyabiashara
huondokana na adha ya kuchapisha au kununua vitabu vingi vya kuandikia
risiti ambavyo utunzaji wa nakala zake unaleta usumbufu;
Pili: Zina uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi na mali ya biashara (stock) bila kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano;
Tatu:
Mtumiaji anaweza kutoa kwa urahisi taarifa za mauzo yake kwa siku, kwa
wiki, kwa mwezi, kwa mwaka na kwa wakati wowote kwa kipindi
kisichopungua miaka mitano;
Nne:
Humwezesha Mfanyabiashara kutuma taarifa zake za mauzo moja kwa moja
kwenda Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka nyingine
zenye mahitaji ya taarifa hizo, kama vile Taasisi ya Taifa ya Takwimu,
Benki Kuu, EWURA, na SUMATRA;
Tano: Mashine
zinaweza kupokea maelekezo moja kwa moja kutoka kwenye Mfumo wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania, na kumtaarifu Mfanyabiashara taarifa yoyote ya Kodi
inayomhusu;
Sita: Kutuma na kupokea fedha kwa njia ya “Mobile Money”.
Utaratibu huu unamwezesha Mtumiaji kutumia Mashine hizi kulipia kodi na
huduma nyingine moja kwa moja kama vile, Ankara za Umeme, Maji, Simu,
n.k;
Nane: Mashine za Kielektroniki zinatumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza inayoeleweka kwa Wananchi wengi;
Tisa:
Mashine za Kielektroniki zinaiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania
kutambua mauzo sahihi ya Mfanyabishara na hivyo kuweza kutoza Kodi
halali.
Mheshimiwa Spika,
39. Msingi
wa bei ya kununulia Mashine hizi za Kielektroniki umezingatia pamoja na
mambo mengine, manufaa na faida nyingi nilizozitaja kwa mtumiaji na
ubora wa mashine zenyewe. Aidha, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania katika Nchi mbalimbali Duniani unaonesha kuwa
mashine zenye ubora unaokidhi mahitaji niliyoyataja hapo juu zinauzwa
na wasambazaji kwa kati ya Shilingi 600,000/= (Dola 375) hadi Shilingi
778,377/= (Dola 486) ikilinganishwa na bei za Mashine za Kielektroniki
za Nchi nyingine zinazotumia mfumo unaofanana na wa Tanzania ambazo
zinauzwa bei kubwa za kati ya Dola za Kimarekani 360 hadi 870. Pamoja na
bei hizo, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kujadiliana na
Wasambazaji wa Mashine hizo ili kuona uwezekano wa kushusha bei hizo.
Mheshimiwa Spika,
40. Kuhusu
bei za karatasi za kutolea Risiti uchunguzi unaonesha kuwa karatasi
hizo zinauzwa kati ya Shilingi 2,200/= hadi Shilingi 4,500/= kuzingatia
ubora na ukubwa mbalimbali wa Risiti hizo. Karatasi hizo zina uwezo wa
kutoa wastani wa risiti kati ya Risiti 200 hadi 1,000 kulingana na urefu
wa “Paper Roll”! au Bunda. Bei ya Karatasi hizi zinazojulikana kama “Thermal Paper” umezingatia kwamba ni za kisasa na hazifutiki kwa urahisi na zina Alama za Siri ndani yake kwa ajili ya kuongeza usalama.
Mheshimiwa Spika,
41. Kuhusu
utaratibu uliotumika kuwapata Watengenezaji na Wasambazaji wa Mashine
hizi za Kielektoniki na Wasambazaji wa karatasi, napenda kulihakikishia
Bunge lako Tukufu kuwa ulikuwa wa wazi na wa ushindani wa Kimataifa na
haukuwa na dosari yoyote.
Mheshimiwa Spika,
42. Katika
kutafuta Watengenezaji na Wasambazaji, kwenye Awamu ya Kwanza
Watengenezaji Wanne (4) na Wasambazaji Sita (6) walipatikana kwa kutumia
Zabuni ya wazi ya Kimataifa (International Competitive Tendering)
kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na
Kanuni zake za mwaka 2005. Kuanzia Mwezi Desemba Mwaka 2009 mpaka Mei
2010 makubaliano yaliingiwa kati ya kila Mtengenezaji na Msambazaji
aliyechaguliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya “Memorandum of Understanding (MOU).
43. Kwenye
Awamu ya Pili ya utekelezaji wa utaratibu huohuo wa Zabuni ya
Watengenezaji ilitangazwa kwenye gazeti la Daily News, The African,
Tovuti ya TRA na Tovuti ya PPRA. Jumla ya Wazabuni Kumi na Nne (14)
walituma maombi ambayo yalifunguliwa mara moja baada ya saa Nne asubuhi
tarehe 27 Septemba 2012. Watengenezaji wa Mashine Wanne (4)
walichaguliwa kati ya Kumi na Nne (14) waliokuwa wameomba na Wasambazaji
Watano (5) walipatikana kati ya Tisa waliotuma maombi yao ndani ya
muda. Kwa kifupi, huo ndio utaratibu uliotumika ambao ulikuwa wa wazi na
ushindani.
Mheshimiwa Spika,
44. Ili kuhakikisha ubora wa Mashine hizi za Kielektroniki, Watengenezaji wametoa “Guarantee”
ya muda wa miaka mitatu kwamba Mashine inayoharibika bila kukusudia na
watawajibika kutoa mashine nyingine na pia kutoa elimu ya matumizi ya
mashine hizo. Vilevile, kwa mujibu wa Mkataba ulioingiwa kati ya
Wasambazaji na TRA, Wasambazaji wanawajibika kuzifanyia matengenezo
mashine hizo kila zinapoharibika ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji
kutafuta watengenezaji wao wenyewe. Napenda kuwahakikishia
Wafanyabiashara na Wananchi wote kwamba, utaratibu wa kutumia Mashine za
Kielektroniki haukuwekwa kwa nia mbaya, bali unalenga kumrahisishia
Mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za kila siku za biashara na
kuwawezesha kulipa kodi stahiki Serikalini.
Mheshimiwa Spika,
45. Kwa
kutambua umuhimu wa mashine hizi katika kuongeza Mapato ya Ndani; na
ili kuyashughulikia malalamiko ya baadhi ya Wafanyabiashara
yaliyojitokeza, Serikali imesogeza mbele muda wa mwisho wa kununua
Mashine za Kielektroniki hadi tarehe 31 Desemba, 2013. Lengo ni
kuwawezesha Walengwa kupata nafasi zaidi ya kujiandaa kununua mashine
hizi na kujifunza namna ya kuzitumia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana
na Wadau mbalimbali wa Sekta Binafsi inaendelea kutoa elimu kuhusu
matumizi endelevu na faida za Mashine za Kielektroniki kwa
Wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa na huduma. Natoa wito kwa
Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa ngazi zote kushirikiana na Serikali
kuwaelimisha Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu manufaa ya Mfumo huu wa
Mashine za Kielektroniki ili kwa pamoja tushirikiane kujenga Nchi yetu
na kuleta maendeleo endelevu kwa kulipa Kodi stahiki.
VI: USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika,
46. Tarehe
16 – 25 Oktoba 2013 nilifanya ziara ya kikazi Nchini China kufuatia
mwaliko wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Li
Keqiang. Katika ziara hiyo, nilifuatana na Viongozi wa Serikali wakiwemo
baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Viongozi wa
Asasi za Sekta Binafsi Tanzania na Watendaji Wakuu wa Serikali na
Mashirika ya Umma ambao walishiriki kwenye mazungumzo na Wabia wetu kwa
upande wa Jamhuri ya Watu wa China.
Mheshimiwa Spika,
47. Dhamira
kubwa ya ziara hiyo kimsingi ilihusu; kukuza mashirikiano ya kibiashara
na utalii Nchini, kufanya mazungumzo na vyombo vya fedha ili kupata
mikopo, kuendeleza uhusiano wa Nchi hizi mbili marafiki, kuona Sekta
Binafsi ya Tanzania inavyoweza kushirikiana na wenzetu wa China na
mwisho kutoa shukrani kwa misaada na mikopo ambayo Nchi yetu imepokea
kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Mheshimiwa Spika,
48. Kama
mnavyojua Taifa la Jamhuri ya Watu wa China ni miongoni mwa Nchi zenye
uchumi unaokua kwa kasi kubwa sana na limepiga hatua kubwa sana katika
maendeleo yake. Kutokana na maendeleo makubwa yanayotokea katika Taifa
la China, nilitoa mwaliko wa kuwakaribisha ili kushirikiana na Tanzania
na Bara la Afrika kwa ujumla wake katika Nyanja za kiuchumi, utamaduni
na kisiasa. Yapo maeneo mengi ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na soko
kubwa la bidhaa za China na uwekezaji.
Mheshimiwa Spika,
49. Katika
ziara hiyo nilipata fursa ya kutembelea Miji ya Beijing, Shenzhen,
Chengdu na Guangzhou ambapo nilipata nafasi ya kukutana na Viongozi wa
Makampuni mbalimbali ya China. Kutokana na Mikutano hiyo, baadhi ya
Makampuni na Taasisi za Umma wameanza kuja Nchini kwa ajili ya
kuendeleza mazungumzo na Serikali pamoja na Sekta Binafsi ili kuanzisha
ushirikiano wa kiuchumi.
Mheshimiwa Spika,
50. Kwa
ujumla ziara hii ilikuwa na mafanikio makubwa. Kwa mfano, pamoja na
kuendeleza na kudumisha ushirikiano ambao umeanzishwa na Viongozi
waasisi wa Nchi hizi mbili yaani Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati
Mwenyekiti Mao Zedong wa Jamhuri ya Watu wa China, kwenye ziara hiyo,
niliweza kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa China Bwana Li Keqiang,
pamoja na Viongozi wa Makampuni yapatayo 30 ya China. Ninaamini
tukijipanga vizuri tutaweza kufanya mengi kati ya Tanzania na China.
Mheshimiwa Spika,
51. Ziara
yangu pia ilifanikisha kutiwa saini kwa Mikataba ya ushirikiano wa
Tanzania na China katika eneo la Sayansi na Teknolojia na katika
Utalii. Mikataba mingine iliyotiwa saini ni kuhusu uuzaji wa bidhaa za
baharini za Tanzania Nchini China na kuanzisha Ukanda wa Kisasa wa
Viwanda vya Nguo pamoja na kukuza zao la Pamba Nchini. Aidha, Mikataba
ya Maelewano inayohusu Sekta za Nishati, Nyumba na Makazi baina ya
Makampuni ya China na ya Mashirika yetu ya Umma yakiwepo Kampuni ya
Umeme – TANESCO, Shirika la Taifa la Maendeleo – NDC na Shirika la Taifa
la Nyumba – NHC ilisainiwa.
Mheshimiwa Spika,
52. Mafanikio
mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuyashawishi Makampuni makubwa ya
usafiri wa anga na Mawakala wa safari za kitalii kuwekeza Tanzania.
Katika jitihada hizo nilikutana na Makampuni ya China Hainan, China Southern Air Line Holding Company na China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited.
53. Napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa kwa kiasi kikubwa Makampuni haya ya
Usafiri wa Anga ya Nchini China yameonesha utayari wao wa kuanzisha
safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na China. Aidha,
Kampuni ya China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited
ambayo inafanya biashara ya kusafirisha Watalii katika Nchi mbalimbali
duniani wameonesha nia ya kuja kuwekeza hapa Nchini katika Sekta ya
Hoteli kubwa za Kitalii. Kampuni ya China Merchants Holdings International Limited ambayo
imehusika katika ujenzi wa Bandari kubwa na Mji wa Shenzhen katika
Jimbo la Guangdong, kwa upande wake imekubali kuingia ubia na Serikali
yetu katika ujenzi na kuendeleza Bandari mpya ya Bagamoyo na Mji wa
Bagamoyo unaotarajiwa kuwa “Trade Hub” ya Afrika.
Mheshimiwa Spika,
54. Tanzania
imedhamiria kuendeleza uchumi wake kwa lengo la kufikisha Tanzania kuwa
Nchi ya Uchumi wa Kati kabla au ifikapo mwaka 2025. Viashiria vyote
vinaonesha hivyo, na ndio sababu Makampuni yote niliyozungumza nayo
wakati wa ziara hiyo yameonesha shauku kubwa ya kuja kuwekeza Tanzania
katika Sekta mbalimbali na mengine tayari yapo Nchini kutekeleza miradi
mbalimbali. Napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kuwa Serikali kwa upande
wake tutajitahidi kupokea Uwekezaji huo na hivyo kunufaika na matokeo
tunayotarajia. Aidha, tutaendelea kuondoa vikwazo vya kufanya biashara
na uwekezaji ili kuweza kuvutia Mitaji na Wawekezaji wengi zaidi pamoja
na Watalii kutoka China na maeneo mengine duniani.
VII: JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika,
55. Mtakumbuka
tarehe 7 Novemba, 2013 Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alihutubia Bunge ambapo pamoja na mambo
mengine alizungumzia suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali
wa Tanzania katika Jumuiya hiyo. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu
kwamba katika Mkutano
Mkuu wa 15 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika
tarehe 30 Novemba, 2013 Kampala Nchini Uganda, Wakuu wa Nchi hizo
akiwemo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete walikutana na
waliidhinisha na kuweka Saini Itifaki ya Umoja wa Fedha wa Afrika
Mashariki. Aidha, Viongozi hao walizitaka Nchi Wanachama kukamilisha
taratibu za kuridhia Itifaki hiyo ifikapo mwezi Julai, 2014.
Mheshimiwa Spika,
56. Manufaa
ya Umoja wa Fedha ni pamoja na: kupunguza gharama ya kufanya biashara
katika Nchi Wanachama; kuwezesha Nchi Wanachama kuwa na kiwango kidogo
na tulivu cha Mfumuko wa Bei; kuwa na viwango vidogo vya riba ya kukopa;
na kuepusha athari za ubadilishaji wa fedha ndani ya Jumuiya kwa kuwa
na Sarafu Moja. Matarajio ni kujenga ukanda tulivu wa kifedha (Monetary and Financial Stability Zone) utakaorahisisha na kusaidia ukuaji wa biashara na shughuli za kiuchumi ndani ya Jumuiya.
Mheshimiwa Spika,
57. Katika
Mkutano huo wa Kampala Wakuu wa Nchi pia waliridhia Mfumo wa kuanzisha
Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuagiza kuwa
ifikapo mwezi Januari 2014, Nchi Wanachama ziwe zimeanza utekelezaji
wake na kuukamilisha ifikapo au kabla ya mwezi Juni 2014.
Aidha, Wakuu wa Nchi walipokea Taarifa kuhusu maendeleo ya Mpango Kazi
wa kuelekea kuanzisha Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.
Walitumia muda wa Mkutano huo kujadili hali ya usalama iliyopo katika Nchi hizi na waliona kuna umuhimu wa kuongeza juhudi katika kukabiliana na Ugaidi.
Mheshimiwa Spika,
58. Kwa
ujumla Mkutano huo ulikuwa na mafanikio sana hasa katika kuimarisha
Umoja wa Jumuiya. Aidha Wakuu wa Nchi wote kwa pamoja walitumia muda huo
kubadilishana mawazo kuhusu kuhakikisha kwamba mahusiano yetu kati ya
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanadumu na tunaendelea kuijenga
Jumuiya na kuiimarisha kwa nguvu zetu zote.
X: PROGRAMU YA KUBORESHA MIJI NCHINI (URBAN LOCAL GOVERNMENT STRENGTHENING PROGRAMME-ULGSP)
Mheshimiwa Spika,
59. Wakati wa kuhitimisha Mkutano wa 12 wa Bunge, nilieleza kuhusu Programu ya Kuboresha Miji Nchini (Urban Local Government Strengthening Programme-ULGSP) ya miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2013 hadi 2018. Huu ni mwendelezo wa Programu ya Uendelezaji na Uboreshaji Miji Nchini (Tanzania Strategic Cities Programme-TSCP); ambao kwa sasa unakaribia kumalizika utekelezaji wake. Programu
hii ya ULGSP kwa sasa inahusisha Manispaa 11 na Miji 7. Manispaa
hizo ni Tabora, Morogoro, Shinyanga, Lindi, Sumbawanga, Musoma, Songea,
Singida, Iringa, Bukoba na Moshi. Miji mingine inayohusika ni Kibaha,
Geita, Babati, Korogwe, Mpanda, Njombe na Bariadi. Halmashauri hizi
zinazojumuisha Manispaa na Miji 18 ziko tayari baada ya kukidhi vigezo
vilivyowekwa, ambavyo ni pamoja na:
i. Kuongeza Bajeti ya mapato kila mwaka;
ii. Kutokuwa na Hati Chafu za Hesabu za Halmashauri,
iii. Kuunda Kamati za kushughulikia matatizo yanayotokana na Programu kwenye ngazi ya Halmashauri, ngazi ya Kata na Mitaa;
iv. Kuhakikisha Programu hiyo imetangazwa na kueleweka na wakazi wa Halmashauri za Manispaa na Miji;
v. Kuhakikisha kuna Wakuu wa Idara wa kutosha;
vi. Kuhakikisha Sheria za Manunuzi zinafuatwa;
vii. Kuhakikisha Watu watakaohamishwa na Programu na kulipwa fidia hawazidi nyumba 20;
viii. Kuhakikisha miradi iliyotekelezwa inalingana na thamani ya fedha iliyotumika;
ix. Kutekeleza miradi ya miundombinu iliyoko kwenye menu;
x. Kupeleka taarifa za kila robo mwaka za miradi kwa muda unaotakiwa;
xi. Kuhakikisha kuna Master Plan ya Mji;
xii. Kuhakikisha ukusanyaji wa kodi ya majengo unaongezeka kati ya Asilimia 5 hadi 30; na
xiii. Kuhakikisha taarifa za Mkaguzi wa Ndani zinaenda kwenye vikao vya Halmashauri kila robo mwaka.
Ukikosa hapa fedha hizo hazipatikani.
Mheshimiwa Spika,
60. Nimetaja
baadhi ya Vigezo kwani viko zaidi ya 200 na vinagusa kila Sekta ya
Halmashauri. Upimaji wa vigezo vyote vitafanyika mara 2 kwa mwaka; na
Halmashauri zitakazoshindwa kufikia Alama (Marks) 60 na
kuendelea, watapunguziwa fedha za miradi yao. Hivyo, Mikoa na Mabaraza
ya Madiwani lazima yahakikishe kuwa vigezo vyote vinasimamiwa na
kutekelezwa kikamilifu. Aidha, TAMISEMI wawachukulie hatua za kisheria
wale wote watakaozembea katika kutimiza vigezo hivi na kuathiri
maendeleo ya Wananchi.
Mheshimiwa Spika,
61. Programu
hii ambayo ni ya kwanza Afrika itatumia Dola za Kimarekani 255, fedha
ambazo zilikuwa zitolewe mwezi Julai mwaka huu, lakini kutokana na
matatizo ya ubadhirifu yaliyojitokeza kwa Wasimamiaji wa fedha
zilichelewa kutolewa. Hata hivyo, baada ya kuwapeleka wahusika wa
ubadhirifu kwenye Vyombo vya Sheria, Wafadhili waliridhika na hatua
zilizochukuliwa, hivyo tarehe 27 Novemba, 2013 Wafadhili walitoa fedha
za Awamu ya Kwanza, ambazo zilitumwa kwenye Halmashauri hizo 18. Miradi
iliyopo kwenye Programu ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara na
mifereji ya mvua, uwekaji taa barabarani, ujenzi wa Stendi za Mabasi,
upimaji viwanja, utengenezaji wa madampo, kuweka miundombinu ya majitaka
na uboreshaji wa makazi. Hii ni baadhi ya Miradi ya Miji iliyoibuliwa
na Halmashauri zenyewe kufuatana na matatizo ya Miji hiyo. Hivyo,
ninawaomba TAMISEMI – wasimamie Programu hii vizuri ili Miradi husika
iweze kutatua matatizo ya Wananchi katika maeneo yao na kuhakikisha
Mapato ya Halmashauri yanaongezeka. Lengo ni kuwezesha Halmashauri hizo kujitegemea baada ya Miradi hiyo kukamilika.
XI: USIMAMIZI NA UDHIBITI WA FEDHA KATIKA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA
Mheshimiwa Spika,
62. Kama
ambavyo itakumbukwa, wakati wa majadiliano ya Taarifa ya Kamati ya
Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu zilizokaguliwa za Serikali za
Mitaa, kwa mwaka 2011/2012, Waheshimiwa Wabunge walionesha masikitiko
yao kwa vitendo vya ubadhirifu na ufisadi unaofanywa na baadhi ya
Halmashauri Nchini. Aidha, Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia
mjadala huo walidai kuwa Serikali imekuwa haichukui hatua dhidi ya
Watumishi wanaofanya makosa katika Halmashauri. Napenda kuwafahamisha
Waheshimiwa Wabunge kwamba pamoja na matatizo na changamoto mbalimbali
zilizopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu usimamizi na
udhibiti wa fedha za Umma, Serikali imejitahidi kuimarisha usimamizi na
utendaji katika eneo hili. Jitihada hizi zimedhihirishwa na Matokeo ya
Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo
yanaonesha kuongezeka kwa ubora wa Hati za Ukaguzi zinazotolewa kwa
Mamlaka za Serikali za Mitaa hususan kuanzia mwaka 2000 hadi sasa. Kwa
mfano, mwaka 2000/2001 Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ulifanywa
na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unaonesha kuwa
Halmashauri zilizopata Hati safi zilikuwa 16 sawa na Asilimia 14 ya
Halmashauri zote. Aidha, Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati zenye
Shaka zilikuwa 23, sawa na Asilimia 20 na Halmashauri zilizopata Hati
Chafu zilikuwa 75 sawa na Asilimia 65 ya Halmashauri zote.
Mwaka
2005/2006 Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati Safi iliongezeka hadi
kufikia 53, sawa na Asilimia 43 na Halmashauri zilizopata Hati zenye
Shaka zilikuwa 67, sawa na Asilimia 54 na Halmashauri zenye Hati Chafu
zilikuwa Nne (4), sawa na Asilimia Tatu (3).
Mwaka
2011/2012 taarifa za Ukaguzi ziliimarika zaidi ambapo Halmashauri
zilizopata Hati Safi ziliongezeka maradufu hadi kufikia 104, sawa na
Asilimia 78 na zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 29, sawa na Asilimia
21 na hakukuwa na Halmashauri iliyopata Hati Chafu.
Mheshimiwa Spika,
63. Jitihada
hizi ni kubwa. Hivyo, Serikali itaendelea kuimarisha Usimamizi na
Udhibiti na Mapato na Matumizi ya Serikali katika Sekta zote na Mamlaka
za Serikali za Mitaa ili kuongeza ufanisi na tija katika utendaji na
kudhibiti ubadhirifu wa fedha na mali za Umma. Lengo ni kuongeza kasi ya
kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu na Kukuza Uchumi kwa haraka.
Mheshimiwa Spika,
64. Pamoja
na jitihada hizo za Serikali zinazoonekana, napenda kuwahakikishia
kwamba Watumishi waliohusika na ubadhirifu wa mali na fedha za Umma
wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kusimamishwa
kazi, kushushwa vyeo, na kufikishwa mahakamani. Aidha, kesi za
Watumishi hao ziko katika Mahakamani na katika Vyombo vya nidhamu vya
Halmashauri na Tume ya Utumishi wa Umma kulingana na makosa yao
kuhakikisha kwamba tunajenga nidhamu. Kutokana na hatua hizo kati ya
mwaka 2011/2012 hadi Septemba, 2013 jumla ya Wakurugenzi 52, Wakuu
wa Idara 65 na Watumishi wengine 749 wamechukuliwa hatua za kinidhamu
na kisheria kwa ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri mbalimbali
Nchini. Hatua hizo za kinidhamu ni kama ifuatavyo:
i) Waliofukuzwa kazi ni 232,
ii) Waliosimamishwa kazi ni 186,
iii) Waliovuliwa Madaraka ni 33,
iv) Waliopunguziwa Mshahara ni 1,
v) Walioshushwa Cheo ni 32,
vi) Walipewa ONYO ni 113,
vii) Waliofikishwa Mahakamani ni 233,
viii) Waliofikishwa Polisi na TAKUKURU ni 36.
Serikali itaendelea kusimamie eneo hili kuhakikisha fedha za Umma zinatumika vizuri.
Mheshimiwa Spika,
65. Pamoja
na hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa Watumishi hao mmoja mmoja,
Serikali imeendelea kuchukua hatua nyingine mbalimbali kukabiliana na
tatizo la ubadhirifu wa mali za Umma katika Halmashauri. Juhudi hizo
ni pamoja na kuongeza uwezo kwa kuajiri Wahasibu wa kutosha katika
Halmashauri zetu; kuanzisha Kamati za Mapato na Matumizi katika ngazi
zote za Halmashauri na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Kamati za
Mapato na Matumizi za Halmashauri zote. Mbinu nyingine zinazotumika ni
kufanya Ukaguzi Maalum kubaini ufisadi na ubadhirifu wowote
uliojitokeza. Kwa mfano, Katika mwaka wa fedha 2011/12 kumefanyika
Kaguzi maalumu kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kumi na nne (14),
ambazo ni Kilindi, Kiteto, Muheza, Ruangwa, Musoma, Kilwa, Temeke,
Singida, Arusha, Mvomero, Morogoro, Dodoma, Mbarali na Bunda. Kaguzi
hizo zimesaidia sana katika kujenga nidhamu ya Watumishi katika
Halmashauri hizo.
Mheshimiwa Spika,
66. Serikali
pia imeweza kubadili na kuweka Mfumo wa ‘Lawson’ katika kila
Halmashauri ili kumaliza tatizo la Mishahara kwa Watumishi waliofariki,
walioacha kazi, wastaafu, n.k. Vilevile kuna Mfumo wa Epicor 9.05 ambao
zinasaidia kudhibiti Bajeti za Mapato na Matumizi katika Halmashauri
Nchini. Mafunzo kuhusu matumizi ya Mifumo hii mipya yanaendelea kutolewa
ili kuweza kutumia mifumo hii kwa ufanisi. Vilevile, Wakuu wa Mikoa
walikwishaagizwa kuhudhuria Vikao vya Baraza za Halmashauri; katika
kujadili Hoja za Ukaguzi ili Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali aweze kufuta zile zilizojibiwa kikamilifu. Hoja ambazo
hazikupata majibu kikamilifu, Sheria zifuatwe na wenye kuhusika na
ubadhirifu wowote wachukuliwe hatua zinazostahili. Aidha, Maafisa
Masuuli (Wakurugenzi) wanaohusika na Hoja mbalimbali za Ukaguzi
wanapaswa kuitwa kwenye Halmashauri walizotoka ili kujibu hoja
zinazowahusu bila kujali wamehamishiwa wapi.
XI: HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
67. Tumekuwa
na muda mzuri wa kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Nchi
yetu hapa Bungeni kwa kipindi chetu tulichokuwa katika Mkutano huu.
Napenda niwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee
nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza
vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza Vikao
vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa
michango yao wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu wa Bunge na
Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake
ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma
mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa
Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za
majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi.
Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri waliofanya ya kuwasafirisha kwa
usalama Waheshimiwa Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi
wote walioshiriki katika Mkutano huu.
68. Niwashukuru
Wabunge wote kwa kujadili vizuri hoja za zilizojitokeza hapa Bungeni.
Lakini kipekee niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri Wanne waliokubali kubeba
jukumu ka kuwajibika kwa yote yaliyotokea. Tunawashukuru kwa uzalendo
wao kwa Nchi yetu na tunawatakia kila la kheri katika maisha yao.
Mheshimiwa Spika,
69. Tunahitimisha
shughuli za Bunge hili tukiwa tumebakiza siku chache kabla ya kufika
Mwisho wa Mwaka huu 2013. Tunamuomba Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa
Rehema atujalie katika siku hizi chache tuweze kusherehekea Sikukuu
njema ya Krismas na tuvuke salama mwisho wa mwaka na kuingia Mwaka Mpya
2014 kwa Amani na Furaha!.
Mheshimiwa Spika,
70. Kama
ambavyo Waheshimiwa Wabunge wote tunavyofahamu, tutakuwa na Bunge la
Katiba litakalofanyika mapema mwakani na kwa tarehe itakavyopangwa.
Kutokana na utaratibu huo ni dhahiri kwamba wengi wetu tutakutana wakati
wa Bunge la Katiba. Nitumie fursa hii kuwatakia safari njema
mnaporejea kwenye maeneo yenu na wengi wenu niwatakie mapumziko mema ya
Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya hadi tutakapokutana wakati wa Bunge la
Katiba.
Mheshimiwa Spika,
71. Baada
ya kusema hayo, naomba sasa Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi
litakapokutana kwa Mkutano maalum wa Kumi na Tano wa Bunge la Bajeti
tarehe 06 Mei, 2014 saa 3:00 Asubuhi katika Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
72. Naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment