KATIBU
Mkuu mpya wa TFF, Selestine Mwesigwa ameingia ofisini na mkakati ambao
hakuna tajiri yeyote wa Simba wala Yanga atataka kuusikia.
Kama
mkakati huo utafanya kazi hakuna fedha zozote za mashabiki au wanachama
matajiri zitatumika kufanya vurugu za usajili, jambo ambalo huenda
likashitua wengi.
Yanga na
Simba zimekuwa zikifanyiana vurugu kwa kupokonyana wachezaji wakati wa
usajili huku wanachama matajiri ambao wengine si viongozi wakitaka
kutunishiana ubabe na kuonyeshana nani mwenye fungu.
Lakini
Mwesigwa ameingia TFF na mfumo ambao utazizuia klabu kutumia fedha
yoyote ambayo haitokani na soka kama zilivyozowea kufanya Simba na Yanga
ambazo hazina vyanzo maalum vya mapato.
Kwa
mujibu wa Mwesigwa klabu zote za Ligi Kuu Bara zitatakiwa kujihadhari na
matumizi ya fedha ambazo hazitokani na soka katika matumizi yake
mbalimbali
ikiwemo usajili.
Mwesigwa
aliliambia Mwanaspoti kwamba, moja ya mambo ambayo atayasimamia ni
utekelezaji wa azimio la Bagamoyo ambalo lilielekeza mambo kadhaa ya
kufuatwa ili kuendeleza soka nchini miongoni mwa mambo hayo ni klabu
kuwa na watumishi wenye sifa, viwanja vya mazoezi na uwazi katika
taarifa za mapato na matumizi.
Katika
mapato na matumizi ndipo inapoingia hoja ya kuwepo kwa matumizi ya haki
ya fedha za soka yaani 'Football Financial Fairplay', mfumo ambao
unasimamiwa na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa).
"Football
Financial Fairplay ndiyo itakayoongoza klabu kutumia fedha zinazotokana
na soka tu na si vinginevyo, unajua hapa ndipo mambo yanapoharibika
kwani unaweza kuona klabu moja inaidhamini klabu nyingine na kupunguza
ushindani katika ligi," alisema Mwesigwa ambaye ni mtaalam wa uongozi wa
biashara.
Mwesigwa
aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, alisema hata kama klabu zinasaidiwa
na watu wenye fedha misaada hiyo inatakiwa kuwepo katika mikataba
maalum na si mtu au kundi la watu binafsi kuingiza fedha kienyeji kwenye
timu.
Klabu za
Simba na Yanga mara nyingi zimekuwa zikifanya usajili wa wachezaji wake
kwa kutumia mamilioni ya fedha ambazo hutoka kwa wapenzi na wanachama
wake.
"Unajua
hata Uefa baada ya kuona baadhi ya timu zinakuwa juu na nyingine
zinaelekea kufa wakaanzisha hii 'Football Financial Fairplay' ili kuzipa
nguvu na klabu nyingine, hivyo na mimi nitaisimamia ili kuona tunapiga
hatua katika soka," alisema Mwesigwa mwenye umri wa miaka 43.
Hiyo
inamaanisha kwamba kama klabu itataka kusajili itapaswa kutumia fedha
zake yenyewe au ambazo zimetokana na udhamini ambao upo kwenye
makubaliano maalum na si mwanachama au shabiki kutoa fungu ghafla.
Chanzo: mwanaspoti
No comments:
Post a Comment