Mwanza.Wakati
maziko ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani hapa na Diwani wa Kata ya
Kisesa, Clement Mabina yakifanyika kesho katika kilima cha Kanyama,
ikiwa ni eneo ambalo alilouawa na kundi la watu Jumapili iliyopita,Rais
Jakaya Kikwete ametuma salaam za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
kutokana na msiba huo.
Mabina, aliyekuwa Mwenyekiti CCM
Mwanza hadi Oktoba 2012, aliuawa na kundi la watu wenye hasira katika
kilima cha Kanyama, katika kata ya Kisesa, kiasi cha kilometa 10
Mashariki ya jiji la Mwanza.
Msemaji wa familia, Timothy
Gregory aliiambia Mwananchi jana kuwa, mipango ya mazishi imekamilika
kabla ya watu kutoa heshima zao za mwisho na mazishi yatafanyika kesho
(Alhamisi) mchana.
“Baadhi ya watu muhimu katika familia wamekwishawasili akiwamo binti yake mdogo aliyekuwa Ulaya,” alisema msemaji wa familia.
Alisema binti mkubwa wa marehemu
alikuwa akitarajiwa kufika Mwanza muda wowote jana tayari kwa mazishi
ambayo yatashirikisha pia viongozi wa chama na Serikali kutoka ndani na
nje ya Mkoa wa Mwanza.
Wakati huo huo, Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Mwanza, SACP Valentino Mulowola alisema, kulikuwa
hakuna mtuhumiwa aliyeongezeka jana baada ya saba waliokamatwa juzi
katika maeneo ya Kisesa na Kanyama.
Salaamu za rambirambi
Katika taarifa yake kupitia
Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Kikwete alisema: “Nimemtumia salamu
za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo kutokana na vifo
vya watu wawili vilivyotokea Desemba 15, mwaka huu katika Kitongoji cha
Kanyama Kata ya Kisesa Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza.”
Taarifa hiyo ilisema kuwa Rais
ametuma salamu hizo kutokana na vifo vya Mabina na Tenery Malimi
vilivyotokea baada vurugu zilizosababishwa na mabishano ya ardhi. Rais
amemuomba mkuu wa mkoa kuwatahadharisha wananchi kutokuchukua sheria
mikononi na pia kuwa waangalifu na matumizi ya silaha za moto.
“Nimesikitishwa na kufadhaishwa
na taarifa za vifo vya wananchi hao wawili vilivyosababishwa na mgogoro
wa ardhi ambao ungeweza kupata suluhu kwa njia za amani. Ni vyema
wananchi wakawa na subira na kuwa waangalifu katika kutatua migogoro
yao,”. Rais alisema na kuongeza kuwa ni “subira na busara ndiyo ziwe
muongozo wa kutatua migogoro yetu katika jamii badala ya hasira”.
Mabina
aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo Diwani na Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Magu mwaka 2000 – 2005, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
Mkoa wa Mwanza, mwaka 2007 – 2012. Rais ameziombea nyoyo za marehemu
wote Mungu azilaze mahali pema peponi Amen.
CHANZO: MWANANCHI


No comments:
Post a Comment