Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, December 22, 2013

MWALIMU SHULE YA MSINGI AMTIA MIMBA MWANAFUNZI WAKE

Ofisa Elimu Msingi, Wilaya ya Nkasi, Bw. Misana Kwangura akizungumza na Thehabari.
Na Thehabari.com, Namanyere-Nkasi
MWALIMU mmoja wa Shule ya Msingi Sintali (jina tunalo) anatuhumiwa kwa kuwatia mimba wanafunzi wawili mmoja akiwa wa shule anayofundisha yeye na mwingine wa Shule ya Sekondari Sintali hali iliowafanya wanafunzi hao kukatisha masomo.
Tukio hilo limetokea Katika Kijiji cha Sintali, Wilaya ya Nkasi na baada ya taarifa kuenea kijijini hapo mwalimu huyo alitoroka kituo chake cha kazi na kukimbilia pasipo julikana. Akizungumzia tukio hilo Ofisa Elimu Msingi, Wilaya ya Nkasi, Bw. Misana Kwangura alisema mwalimu huyo anadaiwa kufanya kosa hilo tangu mwezi Agosti, 2013 na baada ya kuanza kufuatiliwa alikimbia kituo chake cha kazi.
Alisema baada ya kutoroka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ulilazimika kusitisha mshahara wake jambo ambalo lilimlazimu ajilete mwenyewe ndipo alipokamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa kosa linalomkabili.
Hata hivyo Kwangura alisema wanafunzi hao mmoja wa darasa la saba na mwingine wa kidato cha pili wamekana mwalimu huyo kuwatia mimba na kudai wametiwa mimba na watu wasiojulikana ambao walikuja kijijini hapo kununua mazao. Mwalimu huyo amekana kuhusika na kitendo hicho.
Pamoja na hayo Jeshi la Polisi limemuachia mwalimu huyo baada ya kukosa ushahidi wa kumtia hatiani.
“…Uongozi wa Kijiji pamoja na wa shule wanaamini kuwa yeye (mwalimu huyo) ndiye aliyewatia mimba lakini wao wanakataa, sisi tunaamini wanamtetea ili asichukuliwe hatua za kisheria lakini sisi hatujakubali tunasubiri wanafunzi hao wajifungue kasha tutatumia DNA kupima tujue ukweli…tayari mmoja amejifungua tunamsubiri mwingine,” alisema Ofisa Elimu, Kwangura.
Alisema vipimo vitapelekwa kwa Mkemia wa Serikali ili hatuhakikishie bila utata. Alisema tayari wamemkamata mwalimu mwingine wa Shule ya Msingi Itindi ambaye naye amemtia mimba mwanafunzi wa darasa la saba wa shule anayofundisha tangu mwezi wa nane mwaka huu.
Huyu naye baada ya kumtia mimba alipotea lakini baada ya kusitisha mshahara amejileta mwenyewe na tayari anashikiliwa na Jeshi la Polisi Nkasi kwa kosa alilolifanya. tuajabu huyo alikutoroka. Akizungumzia kwa ujumla matukio ya wanafunzi wa Shule ya Msingi kutiwa ujauzito, Ofisa Elimu huyo alisema matukio ya mimba kwa wanafunzi shule za msingi yanapungua kwa sasa kwani tangu Januari hadi Novemba 2013 jumla ya wanafunzi 9 wametiwa ujauzito na kukatizwa masomo yao, idadi ambayo ni ndogo ukilinganisha na mwaka 2012 ambapo wanafunzi 11 walitiwa mimba.
Aidha aliongeza kuwa kwa mwaka 2011 jumla ya wanafunzi 16 wa shule za msingi walitiwa mimba na kukatizwa masomo yao. “…Kimsingi naweza kusema matukio haya kwa sasa yanapungua ukilinganisha na hapo nyuma, na hii inatokana na elimu ambayo tunaitoa kwa kuzunguka kwenye shule mbalimbali kwa kutumia ofisi ya Ofisa Elimu Sayansi Kimu,” alisema Kwangura.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TWMWA
 

No comments:

Post a Comment