AFANDE
Sele, mwanamuziki maarufu wa kizazi kipya nchini, aliwahi kuimba katika
wimbo wake fulani hivi akisema; ‘Aliwazalo mjinga ndilo
litakalomtokea.’
Leo, miaka kadhaa baada ya mstari ule, Yanga kimewatokea walichokuwa wanawaza kwa muda mrefu, lakini wakaonekana wajinga.
Tangu Emmanuel Okwi apate makali
katika miguu yake miaka minne iliyopita Mtaa wa Msimbazi, jijini Dar es
Salaam, Yanga walikuwa wanawaza kumpata, na kweli wamempata.
Maswali mengi kuliko majibu
Kabla Okwi hajavaa jezi za njano
na kijani, kuna maswali mengi yanayopaswa kujibiwa ingawa majibu yake
hayaonekani hewani. Tatizo si Yanga imempataje Okwi. Tunajua kuwa fitina
maridadi za usajili kwa sasa zimehamia Yanga baada ya kufifia kwa kundi
la Friends of Simba la klabu ya Simba ambao ndio walikuwa hodari zaidi
kwa fitina hizi kabla ya kuibuka kwa watu wanaoitwa akina Bin Kleb, Seif
Magari, Mussa Katabaro na wengineo pale Jangwani.
Lakini maswali yanakuja. Ni
kweli Simba haijalipwa pesa za Okwi? Kama wamelipwa, nani alipokea? Kwa
nini SC Villa wameruhusiwa kumuuza mchezaji ambaye alitajwa kuwa yupo
kwa mkopo tu klabuni kwao kwa ruhusa maalumu kutoka Shirikisho la Soka
la Kimataifa (Fifa)?
Nani hasa alikuwa anammiliki
Okwi kati ya SC Villa ya Uganda na Etoile du Sahel ya Tunisia? Lakini
pia kwa sasa kuna mfumo wa Transfer Matching System (TMS) ambapo jina la
mchezaji mwenye matatizo lisingeweza kukubali kuingia katika orodha ya
wachezaji wa Yanga. Mbona Yanga wamefanikiwa kuliingiza jina la Okwi?
Kwa nini wamepata ITC kama kweli Okwi alikuwa ana matatizo?
Kitanzi katika shingo ya Simba
Alfajiri ambayo kiungo Patrick
Mafisango alifariki, ilidaiwa kwamba dakika chache kabla hajakutana na
ajali alikuwa anakwepa kusaini mkataba mpya na klabu ya Simba huku
viongozi wao wakidaiwa kutembea na dola kadhaa za kumpa Mcongo huyo.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa
Mafisango alikuwa na mpango wa kwenda kucheza nje ya nchi, au kusaini
Yanga. Kama kweli angesaini Yanga, leo Yanga ingekuwa na wachezaji wanne
muhimu zaidi katika kikosi cha Simba kilichotamba miaka mitatu
iliyopita wakiunda ‘uti wa mgongo’ wa timu.
Ili timu iwe imara inahitaji
kuwa na wachezaji wanne ambao ukiwapanga uwanjani unapata ‘uti wa
mgongo’, yaani kipa, beki wa kati, kiungo na mshambuliaji.
Kikosi
hicho kiliundwa kwa msingi wa kipa, Juma Kaseja, katika ulinzi, nguzo
alikuwa Kelvin Yondani, katika kiungo msingi alikuwa Mafisango, katika
ushambuliaji nguzo alikuwa Okwi.
Ina
maana kasoro Mafisango, nguzo yote imekwenda Yanga. Hakuna ubishi kwamba
Yanga wanaibuka na kikosi imara zaidi kwa sasa hapa nchini kama
utawajumuisha Kaseja, Mrisho Ngassa, Haruna Niyonzima, Okwi, Yondani,
Mbuyu Twitte, Didier Kavumbagu, Frank Domayo na Hassan Dilunga. Nani
hataki kuwa na wachezaji hawa?
Kwa nini Simba wameondokana na
nguzo hizi kuimarisha nyumba ya wapinzani wao? Ukweli ni kwamba wakati
wenzao Yanga wakijadili soka la uwanjani, Simba wanaendeshwa na
mwanasiasa na wamekubali kwenda kisiasasiasa zaidi.
Timu ambayo Simba walikuwepo
nayo miaka mitatu iliyopita, wakitamba katika mechi za kimataifa dhidi
ya Kiyovu ya Rwanda na Setif ya Algeria huku wakitolewa kwa shida na
Shandy ya Sudan robo ya wachezaji leo wapo Yanga.
Kama nilivyosema, ujanja ujanja
ambao ulikuwepo Simba katika kundi la Friends of Simba kama vile kumpora
Victor Costa katika mikono ya Yanga na kumvalisha jezi iliyoandikwa
Jamal Malinzi, yote haya yamehamia Yanga.
Wajanja wote wa Simba wamesusa
na wamemuachia timu Mbunge kwa sababu wanaamini amekuwa na mdomo mwingi
kuliko vitendo. Wanataka maneno yake yafike mwisho na aadhirike mbele ya
wanachama. Nina uhakika wa asilimia 100 wengi kati yao wamefurahi
uhamisho wa Okwi kwenda Yanga kwa sababu wanajua huu ni wakati ambapo
Mbunge atawekwa pabaya na wanachama.
Yanga itabakia chui wa karatasi?
Nimesema hapo juu. Yanga
inaonekana kutimia katika maandishi. Wana Kaseja, Mrisho Ngassa, Haruna
Niyonzima, Okwi, Yondani, Mbuyu Twitte, Hamis Kiiza ‘Diego’, Didier
Kavumbagu, Frank Domayo na Hassan Dilunga. Nani hataki kuwa na wachezaji
hawa?
Bado siku 13 kengele za mwaka
mpya zigonge. Na zikigonga Yanga watakuwa wamekaribia kushiriki michuano
ya kimataifa. Wanaamini wana kikosi kabambe. Mioyoni wanaweza kuwa
wanasema ‘Huku Okwi, huku Ngassa, katikati Kiiza na Kavumbagu’. Lakini
watafanya kweli?
Kama wachezaji walionao sasa
wakicheza asilimia 80 ya uwezo wao, Yanga inaweza kushindana katika anga
za juu na kuwafurahisha mashabiki wao. Tatizo kubwa ni kwamba mastaa
hawa wanaweza kuwepo na bado Yanga wakabakia kuwa chui wa karatasi tu.
Chui asiyeuma.
Mpira wetu bado hauna nidhamu.
Utasikia Okwi kaenda kwao miezi miwili, Niyonzima kaenda kwao wiki sita,
na mastaa waliopo wanashindana kuingia klabu za usiku kuliko kwenda
mazoezini asubuhi.
Haijalishi ni kiasi gani cha
mastaa unao klabuni, kama hawajitumi kama wachezaji wa Mbeya City
wanavyofanya, basi hakuna unachoweza kufanya katika soka. Unaishia
kuogopwa kwa majina ya gazetini tu.
Matokeo
yake, licha ya usajili huu sioni kama Yanga wanaweza kukomesha ubabe wa
Waarabu na TP Mazembe. Labda kama wakiamua kufa uwanjani na kufanya
mazoezi ambayo wachezaji watakojoa damu.
Maisha yanataka nini Okwi?
Desemba kama hii mwaka jana,
Okwi alipokea kiasi cha zaidi ya dola 40,000 (Sh 64 milioni) katika
Hoteli ya Sheratoni jijini Kampala kutoka kwa matajiri wa Simba ili
asaini mkataba wa miaka miwili wakihofia kuwa Yanga na Azam
zingemchukua.
Siku chache baadaye Simba hao
hao walimuuza kwenda Tunisia ambapo alipewa dola 45,000 za utangulizi na
kisha akaambiwa adai nyingine. Hicho ndio kilikuwa chanzo cha ugomvi wa
klabu hiyo na Okwi mpaka staa huyo akaamua kurudi nyumbani Uganda kwani
alilalamika kuwa alikuwa hajalipwa mshahara wa miezi mitatu.
Lakini kweli pesa zinamfuata
Okwi. Juzi ametia tena kibindoni zaidi ya dola 60,000 kusaini Yanga kwa
miezi 30 ijayo. Hii inamaanisha amevuna Sh200 milioni za Kitanzania kwa
kipindi cha miezi 12 tu. Unataka nini zaidi? Nani anamlaumu?
Kilicho wazi ni kwamba anavunja
mizizi yote ya urafiki na watu wa Simba ambao walimlea nchini tangu mtu
anayeitwa Geofrey Nyange Kaburu amlete nchini akiwa na umri wa miaka 16.
Watu wachache ndani ya klabu
wanaweza wakafurahi kwa sababu uhamisho wa Okwi unamaanisha kuwa sasa
wanachama watakuwa wamemchoka mwanasiasa na wao watapata nafasi ya
kuheshimiwa tena klabuni. Hata Kaburu mwenyewe anaweza kuwa katika kundi
hili.
Lakini kwa vyovyote vile hii ni sinema, ndio
CHANZO: MWANASPOTI


Umeongea maneno Mazur lakin dhahir umeonekana kuegemea upande mmoja na kuuponda mwingne..mtu kama SI makin akisoma hawez elewa mapema lakin Ni dhahir hii makala imeandaliwa na shabik WA simbam..tuongelee maendeleo ya mpira na SI kuleta siasa kwenye mpira Baba....tuuache unazi usiojenga tufanye Yale ya msingi ambayo yatasukuma soka letu na SI kuleta makala zenye uchochoz WA mambo fulan...akhsantee...
ReplyDelete