Mizengo Pinda. |
Watumishi
866 wa serikali wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa
ubadhirifu wa fedha katika halmashauri mbalimbali nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda
alipokuwa akisoma hotuba ya kuahirisha shughuli za Mkutano wa 14 wa
Bunge lililofanyika mjini hapa.
Pinda alisema watumishi waliohusika na ubadhirifu wa mali na fedha za
umma wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kusimamishwa kazi,
kushushwa vyeo na kufikishwa mahakamani.
Aidha, alisema kesi za watumishi hao ziko katika mahakama na vyombo
vya nidhamu vya Halmashauri na Tume ya Utumishi wa Umma kulingana na
makosa yao.
Alisema kutokana na hali hiyo, kati ya mwaka 2011/12 hadi Septemba,
mwaka huu jumla ya wakurugenzi 52, wakuu wa idara 65 na watumishi
wengine 746 wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa ubadhirifu
wa fedha katika halmashauri mbalimbali nchini.
“Waliofukuzwa kazi ni 232, waliosimamishwa 186, waliovuliwa madaraka
33, waliopunguziwa mshahara ni mmoja , walioshushwa cheo 32, waliopewa
onyo 113, waliofikishwa mahakamani 233 na waliofikishwa polisi na
TAKUKURU 36.
“Serikali itaendelea kuhimiza nidhamu katika matumizi ya kifedha na
vilevile itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watumishi wote watakaokuwa
wabadhirifu,” alisema.
Aidha, alisema pamoja na hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa
watumishi hao mmoja mmoja, serikali imeendelea kuchukua hatua nyingine
mbalimbali kukabiliana na tatizo la ubadhirifu wa mali za umma katika
halmashauri.
Pinda alizitaja hatua za kukabiliana na ubadhirifu huo kuwa ni
kuongeza uwezo kwa kuajiri wahasibu wa kutosha katika halmashauri,
kuanzisha kamati za mapato na matumizi katika ngazi zote za halmashauri,
kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa kamati za mapato na matumizi za
halmashauri zote na kufanya ukaguzi maalumu kubaini ufisadi na
ubadhirifu wowote uliojitokeza.
Alitoa mfano katika mwaka wa fedha 2011/12 ulifanyika ukaguzi maalumu
kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa 14 ambazo ni Kilindi, Kiteto,
Muheza, Ruangwa, Musoma, Kilwa, Temeke, Singida, Arusha, Mvomero,
Morogoro, Dodoma, Mbarali na Bunda.
Hali ya chakulaAkizungumzia hali ya chakula nchini alisema tathmini
ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba, mwaka huu
katika maeneo yenye matatizo ya usalama wa chakula na lishe inaonesha
watu 828,063 wanakabiliwa na upungufu wa chakula na watahitaji msaada
wa chakula wa Tani 23,312 hadi ifikapo mwezi Februari 2014.
Aidha, kati ya mwezi Julai na Novemba 2013, Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulitenga jumla ya tani 16,119 za chakula cha
mgawo kwa Halmashauri zenye mahitaji ya chakula cha msaada.
Waziri Mkuu alisema hadi kufikia Desemba 16 mwaka huu, tani 13,716
zilikwishachukuliwa na Halmashauri husika huku Tani 2,402 zilikuwa
hazijachukuliwa na Halmashauri za Mwanga, Babati, Igunga, Mpwapwa na
Manyoni.
“Ninawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ambazo hazijachukua
chakula hicho kufanya hivyo kabla ya Januari 15, mwakani na ambao
hawatatekeleza maagizo haya watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
Aliwahakikishia wananchi pia kuwa serikali itaendelea kusimamia
upatikanaji wa chakula katika Halmashauri zenye hali tete ya chakula kwa
lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula.
Pinda alieleza mwenendo wa bei za vyakula nchini kutokana na miezi
hii kuwa katika kipindi cha mwisho wa msimu wa ununuzi wa mazao, kiasi
cha mazao yanayoingia sokoni kimeanza kupungua.
“Hali hii imesababisha bei za wastani za vyakula hasa mahindi na
mchele katika soko hapa nchini kuanza kupanda ingawaje si kwa kiasi
kikubwa.
Kwa mfano, bei ya mahindi Kitaifa imepanda kutoka Sh 536.86 kwa kilo
mwezi Oktoba, mwaka huu hadi kufikia Sh 538.26 kwa kilo mwezi Novemba,
mwaka huu,” alisema.
Kwa upande wa mchele, bei ya wastani wa Kitaifa imepanda kutoka Sh
1,188.60 kwa kilo mwezi Oktoba, mwaka huu hadi Sh 1,191.10 kwa kilo
mwezi Novemba, mwaka huu na kuongeza kuwa pamoja na hali ya kupanda kwa
bei, bado bei za sasa kwa baadhi ya mazao mfano mahindi, mchele,
maharage na viazi ziko chini ikilinganishwa na zile za kipindi kama
hicho mwaka jana.
“Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa yenye mavuno mazuri kuendelea
kuwahamasisha wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya
Kaya zao na kuuza ziada katika Soko ili kusaidia kupunguza bei ya
vyakula katika miji yetu,” alisema.
Alisema halmashauri zihakikishe kuwa zinadhibiti ununuzi holela wa
chakula kutoka mashambani na majumbani mwa wakulima kwa lengo la
kujihakikishia upatikanaji wa chakula cha kutosha.
Operesheni TokomezaKuhusu Operesheni Tokomeza alisema matatizo
yaliyochunguzwa kuhusiana na operesheni hiyo ni pamoja na mateso dhidi
ya watuhumiwa, matumizi mabaya ya silaha, uchomaji wa nyumba za wananchi
na kuua mifugo kikatili.
Pinda alisema taarifa ya Kamati ilitoa mapendekezo mbalimbali,
waheshimwa wabunge walipata fursa ya kuchangia na kutoa ushauri kwa
serikali.
“Napenda kukubaliana na kamati na waheshimiwa wabunge kwa ujumla kuwa
pamoja na nia nzuri ya operesheni hiyo, utekelezaji na usimamizi wake
ulikuwa na kasoro kubwa,” alisema.
Alisema serikali imesikia na ndio maana mawaziri wanne wameona ni
vyema kujiuzulu ili kulinda heshima na imani ya wananchi kwa serikali
yao.
Mawaziri hao ni Shamsi Vuai Nohodha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Dk Emmanuel J. Nchimbi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk David Mathayo David, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na
Balozi Khamisi S. Kagasheki Waziri wa Maliasili na Utali ambapo Rais
ameridhia kujiuzulu kwao.
“Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru waheshimiwa
mawaziri hao kwa ujasiri wao na kwa kutambua dhamana yao, nawatakia kila
la heri katika shughuli zao za ubunge na nyingine kadri
watakavyojaliwa,” alisema.
Alisema serikali itaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo ya kamati na
ya bunge kwa ujumla kuhusiana na yaliyojitokeza katika Operesheni
Tokomeza.
Pinda aliahirisha Bunge hilo hadi Mei 6 mwakani, litakapokutana tena katika mkutano wa 15 wa bajeti.
TUNAOMBA BOFYA HAPA NA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI ZA KILA SIKU,(USIPITWEEEEEEEE)
No comments:
Post a Comment