Walikwenda kuwatoa wenzao waliokamatwa kwa mauaji
Wenzao wachoma kituo, gari la polisi, pikipiki, majadala ya kesi
Watu
watatu wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Polisi wa
Kituo cha Malinyi Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, na wengine
kujeruhiwa vibaya.
Tukio
hilo lilitokea jana asubuhi baada ya kundi la wakazi wa Kijiji cha
Igawa kuvamia kituo hicho wakitaka kuwatoa wenzao waliokamatwa kwa
tuhuma za mauaji.
Akizungumza
na NIPASHE kwa njia ya simu, Diwani wa Kata ya Malinyi, Said Tilla,
alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya asubuhi baada ya wakazi hao
wakiwamo waliouawa na kujeruhiwa kuvamia kituo hicho.
Tilla, alisema kundi la wakazi hao waliandamana hadi katika kituo
hicho wakiwa na matawi ya miti kushinikiza kutolewa kwa wenzao hao
walikamatwa siku mbili zilizopita kwa madai ya kumua mfugaji wa jamii ya
Kisukuma, Matanji Luhembe (16).
Alisema kitendo cha wakazi hao kuvamia kituo hicho kinatokana na
askari wake kuwakamata wakulima hao watatu peke yao na kuwaacha
wafugaji jamii ya Kisukuma wakati wao ndiyo chanzo cha mapigano hayo.
Wafugaji hao wanadaiwa kumuua mjumbe wa kamati ya mazingira ya kijiji hicho, Victory Maleka Desemba 12, mwaka huu.
Alisema
wakazi hao walipofika katika kituo hicho, waliwakuta askari saba
wakiendelea na kazi baada ya kuzidiwa waliamua kuwapiga risasi za moto
na kuua watatu na kujeruhi wengine wanne kisha kukimbilia
kusikojulikana.
“Wananchi
hawakuwa na siraha zozote bali walikuwa na matawi tu ya miti,
walipofika na kutaka wenzao watolewe ndipo askari wakaanza kupiga risasi
ovyo na kuwaua watu watatu papo hapo na wengine kujeruhiwa na kisha hao
askari wakakimbia na kutelekeza kituo hicho,” alisema Diwani Tilla
kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Aliwataja waliouawa kwa kupigwa risasi kuwa ni Leon Chikwale, Andrew Kikonoki na Edson Kidunde, wakazi wa kijiji hicho.
Alisema majeruhi hao walikimbizwa Hospitali ya Misheni ya Lugala kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Diwani
huyo, alisema baada ya mauaji, wakazi hao waliamua kuchoma moto kituo
hicho, na gari la polisi na pikipiki za kituo hicho huku baiskeli
zilizokamatwa katika matukio mbalimbali wakizichoma pia.
Hata
hivyo, alisema katika tukio hilo hakuna askari yoyote aliyejeruhiwa na
wakazi hao na kwamba Jeshi la Polisi limeamua kuongeza nguvu ya askari
kutoka sehemu mbalimbali ikiwamo wilaya ya Kilombero na mkoa wa Morogoro
ili kutuliza ghasia hizo.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Furaha Lilongeri, alithibitisha
kutokea kwa mauaji hayo yaliyosababishwa na askari hao kuwapiga raia
watatu waliokuwa miongoni mwa wananchi waliovamia kituo cha polisi.
Kamanda
wa polisi mkoani Morogoro, Faustine, Shilogile, alithibitisha kutokea
kwa mauaji ya watu hao papo hapo na wengine kujeruhiwa baada ya
kutokea mapambano baina yao.
Shilogile
alisema watu hao waliouawa ni kati ya zaidi ya wakazi 500 wa kijiji
waliovamia kituo hicho wakishinikiza kutolewa kwa wenzao wanne
waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili na kuchoma moto nyumba
saba.
Alisema polisi walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya wakazi hao waliovamia kituo kwa nia ya kutaka kukichoma moto.
Kamanda
huyo, alisema wakazi hao walichoma moto gari la askari aina ya Pick
up, pikipiki ya polisi, baiskeli tano za vielelezo na majalada ya kesi
yaliyokuwamo kituoni hapo .
Alisema
wakazi hao walivamia kituo hicho kwa nia ya kuwatoa watuhumiwa wanne
waliokamatwa usiku wa Desemba 14, mwaka huu kwa tuhuma za mauaji ya watu
hao wawili, lakini wakati tukio hilo likiendelea, walikuwa
wameshahamishiwa kituo kingine cha polisi.
Alisema
majeruhi wanne wa tukio hilo wamekimbizwa Hospitali ya Lugalo kwa
matibabu zaidi huku jeshi hili likiongeza nguvu kutuliza ghasia hizo.
Tukio
la kuuawa mfugaji huyo na kusababisha watu wannne kukamatwa lilitokea
Desemba 13, mwaka huu baada wafugaji wa jamii ya Kisumuma kumpiga na
kumjeruhi vibaya hadi kumuua Victory Maleka (55).
Chanzo
cha kifo cha Maleka ni wafugaji wa Kisukuma kumtuhumu marehemu
kuwaelekeza askari wa wanyamapori wa Shirika la Hifadhi za Taifa
(Tanapa) maeneo wanayoishi wafugaji hao kinyume cha sheria na ndipo
walipomvamia na kumpiga na kusababisha kifo chake.
Hata
hivyo, baada kifo hicho wakazi hao walishikwa na hasira na kuamua
kujikusanya na kulipiza kisasa kwa jamii ya wafugaji hao kwa kwa
kumuua mwenzao, Matanji Luhembe.
Luhembe alifariki baada ya kupigwa na wakazi hao waliomvamia ghafla akiwa na wenzake wakati wa harakati za kukimbia.
Luhembe alishindwa kujiokoa na kuanguka chini kutokana na tatizo la ugonjwa wa pumu na kupigwa hadi kufa.


No comments:
Post a Comment