
Watu
watatu, akiwamo askari polisi wamefariki dunia na wengine watatu
kujeruhiwa baada ya kuzuka mapambano kati ya polisi na raia katika
Kijiji cha Igwati, Tarafa ya Malinyi Wilaya ya Ulanga, Morogoro.
Diwani wa Kata ya Malinyi, Said Kila aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Leon Chikwita, Andrew Likomoka na Edson Kidunda.
Alisema
mmoja wa majeruhi Idelfonce Malenga (35), hali yake ni mbaya baada ya
kupigwa risasi shavuni. Majeruhi wawili majina yao hayakufahamika mara
moja.
Diwani
Kila alisema mauaji hayo yalitokea baada ya kundi la wakulima kuvamia
Kituo cha Polisi Malinyi kushinikiza kuachiwa kwa wenzao watatu
waliokuwa wanashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mfugaji mmoja wa kijiji
hicho hivi karibuni.
"Baada ya
kupata taarifa za kukamatwa kwa wenzao walifika kituo cha polisi
ambako, hawakuwakuta watuhumiwa hao kwani walikuwa wamehamishiwa kituo
kingine," alisema diwani huyo.
Alisema
katika jitihada za kulinda kituo, polisi walitoa tahadhari mbalimbali za
kuwataka wananchi hao kutawanyika ikiwamo kupiga mabomu ya machozi,
lakini waliendelea kukaidi amri hiyo na badala yake walizidi kujikusanya
na kukivamia na kisha kukichoma moto pamoja na gari la askari
lililokuwapo. Katika shambulizi hilo, ndipo mauaji hayo yalipotokea.
Chagonja eneo la tukio
Kutokana
na tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema ametuma timu
maalumu ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja
kwenda kuongeza nguvu katika operesheni ya kuwasaka na kuwakamata wote
waliohusika na tukio hilo.
Msemaji
wa Jeshi la Polisi, Advera Senso ilisema jana katika taarifa yake kwa
vyombo vya habari kuwa, IGP Mwema ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa
Morogoro hususan, Kata ya Malinyi kuwa watulivu na kuendelea kutoa
ushirikiano kwa Polisi wakati uchunguzi ukiendelea.
Chanzo cha mgogoro
Mgogoro
kati ya wafugaji na wakulima wa Igwati ulianza Desemba 13, mwaka huu
wakati kundi la wananchi lilipomkamata mfugaji huyo na kumpeleka katika
ofisi za kijiji.
Ilidaiwa
kuwa baada ya kumfikisha, mtendaji wa kijiji alimfungia mtuhumiwa huyo
ofisini kwake na kuanza kuhoji sababu za wananchi kumkamata jambo ambalo
linaelezwa kwamba liliwakera na kuanza kumshambulia hadi kuikimbia
ofisi na kumwacha mfugaji huyo ambaye alishambuliwa na kuuawa.
Kitendo
cha kukamatwa na kupigwa hadi kuuawa kwa mfugaji huyo kinadaiwa kuwa
kilikuwa cha kulipiza kisasi baada ya wafugaji kuvamia nyumbani kwa
Mjumbe wa Kamati ya Mazingira, Victoria Marietha na kumjeruhi vibaya
kisha kufariki dunia katika Hospitali ya Lugala, Malinyi alikokuwa
akipatiwa matibabu.


No comments:
Post a Comment