TAMKO LA WENYEVITI WA CCM-MIKOA LA KUMPONGEZA KATIBU MKUU WA CCM NDG. ABRAHAMANI KINANA NA SEKRETARIETI YA CCM TAIFA.
LEO TAREHE 10/DESEMBA/2013
OFISI NDOGO YA CCM DAR- ES- SALAAM
Sisi
Wenyeviti wa CCM-Mikoa tuliokutana leo Tarehe 10/Desemba/2013 hapa Dar
es salaam, kwa kauli moja na kwa niaba ya wanaCCM wa mikoa yetu, tunatoa
kauli ya kumuunga mkono Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ndugu
Abrahamani Kinana na Sekretarieti yote kwa utekelezaji uliotukuka wa
majukumu yao ya kichama. Tangu alipopewa wadhifa wa Ukatibu Mkuu
ameonyesha uwajibikaji mkubwa, uliokiwezesha Chama kupata uhai mpya na
kuamsha Ari na matumaini zaidi ya Watanzania kwa Chama Cha Mapinduzi.
WanaCCM
nchini tuko katika mstari wa mbele kuisimamia Serikali yetu kwa mujibu
wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015 sura ya Tisa; Inayokitaka Chama
kuisimamia Serikali yake.
Kwa pamoja tunaungana na kupinga kwa nguvu zote mambo yafuatayo;
1. Ubadhirifu
unaofanywa katika Serikali za Mitaa nchini unaozifanya Halmashauri
nyingi kujirudiarudia kupata hati chafu na zenye mashaka, inayosababisha
hasara na manung’uniko kwa wananchi.
2. Utelezaji
duni wa baadhi ya miradi ya maendeleo unaopelekea kuwepo kwa huduma
duni na zisizokidhi thamani ya fedha na matakwa ya kitaalamu. Hii
inaashiria uwepo wa Rushwa na ubadhirifu wa fedha kwa baadhi ya miradi
ya maendeleo.
3. Ucheleweshaji
wa maslahi na stahiki za watumishi wa Umma kunakopelekea kuwa wavunja
moyo na ari watumishi, katika kutekeleza majukumu yao na hivyo
kusababisha kutokea kwa migomo ya mara kwa mara kufuatia uzembe katika
kuwapatia haki zao, kinyume na misingi ya utawala bora.
4. Gharama
kubwa ya uendeshaji wa shughuli za Serikali na Taasisi zake
ikilinganishwa na gharama zinazotumika kwenye miradi ya maendeleo na
uboreshwaji wa huduma za jamii kwa wananchi.
5. Usimamizi
mbovu wa Operation mbali mbali za Serikali zenye nia njema kwa Taifa.
Mfano Operasheni kuhamisha wafugaji na Operasheni Tokomeza; Zina nia
njema lakini usimamizi wake umekuwa mbovu hata kupelekea kuvuruga nia
yake njema kwa Taifa.
6. Kushindwa
na Kuchelewa kutatua baadhi ya Kero sugu kwa Wananchi kama malalmiko
mbali mbali ya wakulima (mfano mbolea za minjingu kutofanya vizuri kwa
asilimia kubwa, matatizo ya wakulima wa pamba na korosho nk.) na
wafugaji; Rushwa zilizokithiri katika sehemu mbali mbali za utoaji wa
huduma kwa wananchi na ucheleweshwaji wa fadha za miradi ya maendeleo
nk.
Katibu
Mkuu wa CCM daima amekuwa akikemea kwa nguvu zote madhaifu yote
tuliyoyataja hapo juu na sisi kama Wenyeviti wa CCM Mikoa yote Tanzania. Tunaitaka
Serikali ichukue hatua za haraka katika kurekebisha madhaifu hayo.
Viongozi na watendaji wengine wote wa Serikali, walioonesha udhaifu
mkubwa katika kutekeleza majukumu yao, na ambao walipewa wito na wengine
ambao wanatakiwa kupewa wito; wa kuhudhuria mbele ya Kamati Kuu ya CCM
wachukuliwe hatua zinazostahili. Tunawakumbusha viongozi wa Serikali
watambue kuwa Chama cha Mapinduzi kinaisimamia Serikali kwa mujibu wa
Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015 Sura ya Tisa.
_______________________________________________
Mgana Izumbe Msindai – Mwenyekiti wa Wenyeviti Mikoa
______________________________________________________
Haji Juma Haji – Makamu Mwenyekiti Wa Wenyeviti Mikoa
______________________________________________
Lucas Ole Mukusi – Katibu wa Wenyeviti Mikoa
No comments:
Post a Comment