Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akionyesha Kitabu cha Mpango Mkakati wa Haki za Watoto 2013-2017, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani na Maadili, uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (katikati) akikata utepe kuashiria kuzindua Kitabu cha Mpangokazi wa Taifa wa haki za Binadamu wa mwaka 2013-2017, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani na Maadili, uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo. Wa pili (kushoto) ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na Naibu wake, Angela Kairuki (kushoto) Mwenyekiti wa Tume ya Hakiza Binadamu na Utawala Bora, (wa pili kulia).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani na Maadili, katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi, Makamu wa Rais Dkt. Bilal, kuhutubia na kufungua rasmi, maadhimisho hayo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo.
Baadhi ya wafanyakazi wa Mashiriki, Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali, wakimsikiliza Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, alipokuwa akihutubia wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani na Maadili, uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo.
Baadhi ya wafanyakazi wa Mashiriki, Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali, wakimsikiliza Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, alipokuwa akihutubia wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani na Maadili, uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwangoza baadhi ya Viongozi meza kuu kusimama na kuomboleza kifo cha Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini, Nelson Mandera, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani na Maadili, uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo.
Maandamano yakipita mbele ya Jukwaa Kuu na mabango ikiwa ni sehemu ya ufunguzi Maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani na Maadili, uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo.
Maandamano yakipita mbele ya Jukwaa Kuu na mabango ikiwa ni sehemu ya ufunguzi Maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani na Maadili, uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimsikiliza Mrakibu Mwandamizi wa Mwandamizi wa Magereza, Isaack Kangura, wakati alipotembelea Banda la maonyesho la Magereza katika Viawanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani na Maadili, leo.
Maelezo yakiendelea......
Picha ya pamoja.....
*******************************************
HOTUBA:-
Nianze
kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na
kutuwezesha kukusanyika hapa leo, kushuhudia Maadhimisho haya ya Siku
ya Haki za Binadamu na Maadili ambayo husherehekewa Duniani kote Desemba
10 kila mwaka.
Nitumie
nafasi hii pia kuwakaribisha na kuwapongeza nyote mliofika mahali hapa.
Mmefanya hivi kutokana na sababu moja tu kubwa, nayo ni kwamba; Kila
mmoja wenu anatambua na kujali umuhimu wa Haki za Binadamu na Maadili
mema ndani ya jamii yetu.
Niwashukuru
pia wale wote waliofanikisha tukio hili kwa njia moja ama nyingine.
Kipekee niwashukuru Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Wizara ya
Katiba na Sheria, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Umoja
wa Mataifa -Tanzania, kwa jitihada zao kubwa za kuratibu na hatimaye
kufanikisha Maadhimisho haya. Hongereni sana.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Tanzania
imekuwa ikiadhimisha siku hii kutokana na ukweli kuwa sisi ni wanachama
wa Umoja wa Mataifa ambako ndiko chimbuko la Haki za Binadamu, na
kwamba kama Taifa, tunawajibika moja kwa moja kuzikuza, kuzilinda na
kuzitekeleza hapa nchini.
Serikali
ya Tanzania inao wajibu wa kulinda na kukuza Haki za Binadamu kama
ilivyoelezwa na kufafanuliwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977, Mikataba ya Kimataifa na Kikanda ya Haki za
Binadamu na sheria mbalimbali za nchi.
Kwa
kutimiza wajibu wa kulinda na kukuza Haki za Binadamu, Tanzania ni
miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizoridhia mikataba
mingi ya kimataifa inayohusu Haki za Binadamu. Baadhi ya mikataba hiyo
ni pamoja na; Tamko la Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu la 1948;
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa 1966; Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni 1966; Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Watoto 1989; Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa aina
zote za Ubaguzi wa mwaka 1965; Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Ubaguzi
wa aina yoyote dhidi ya Wanawake wa mwaka 1979; Mkataba wa Kimataifa wa
Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2008; Mkataba wa Afrika wa Haki za
Binadamu na Haki za Watu wa mwaka 1981 na Mkataba wa Afrika wa Haki na
Ustawi wa Watoto wa mwaka 1990.
Baadhi
ya mikataba hii tayari imeingizwa katika sheria zetu za nchi, ama kwa
kuunda sheria mpya au kurekebisha zile zilizopo, ili kuhakikisha kuwa
ulinzi wa Haki za Binadamu unaimarishwa.
Aidha,
pamoja na kuridhia mikataba hii, Serikali imekuwa ikiandaa ripoti
mbalimbali za utekelezaji wa Haki za Binadamu ambazo zimekuwa
zikiwasilishwa kwenye vyombo vya kimataifa kwa ajili ya kujadiliwa na
kutolewa mapendekezo ya utekelezaji.
Ndugu Wananchi;
Napenda
niwahakikishieni kuwa Serikali inaendelea kupitia mikataba ambayo bado
haijafanywa kuwa sehemu ya sheria za nchi, ili nayo iweze kuingizwa kwa
kadri inavyofaa kwa maslahi ya wananchi wetu na maendeleo ya nchi yetu.
Katika
kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kinara wa kujali Haki za Binadamu,
Serikali imeanzisha taasisi mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya
kulinda na kukuza haki nchini.
Taasisi
hizo ni pamoja na:- Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora;
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU); Bunge na Mahakama. Vyombo hivi vilianzishwa kwa
mujibu wa sheria na tutazidi kuvipa ushirikiano kadri inavyowezekana ili
viendelee kufanya kazi zake vizuri na kukidhi matarajio yake kwa umma.
Serikali
pia imejenga mazingira mazuri na kuruhusu taasisi zisizo za kiserikali
kuanzishwa kwa lengo la kusaidia juhudi zake za kuimarisha Haki za
Binadamu hapa nchini. Hadi sasa, Tanzania ina takribani mashirika 5,000
yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na utetezi wa Haki za Binadamu.
Mashirika haya yanatambuliwa kwa mujibu wa mikataba mbalimbali ya
kimataifa na sheria za nchi. Baadhi ya mashirika hayo ni pamoja na;
LHRC, NOLA, PINGOs, TPCF, TAWLA, ZLSC, WLAC, SIKIKA, SAHRINGON, TGNP,
HAKIELIMU na HAKI-ARDHI. Mashirika haya yamekuwa yakitoa mchango mkubwa
katika kutetea na kulinda Haki za Binadamu hapa nchini.
Serikali
pia imetengeneza Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Haki za Binadamu ambao
utazinduliwa leo kwa lengo la kuhakikisha kila sekta inajumuisha masuala
ya Haki za Binadamu kwenye mipango kazi yake na utekelezaji wake. Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Eneo
lingine muhimu ambalo Serikali inajivunia katika harakati zake za
kujenga misingi imara ya Haki za Binadamu hapa nchini, ni haki ya kupata
elimu ambapo hadi sasa, zaidi ya asilimia 98 ya watoto wenye umri wa
kwenda shule, wanaandikishwa na kupata elimu ya msingi inayotolewa
bure. Hivi sasa kila kata nchini ina shule ya msingi na sekondari, kata
zingine zina shule zaidi ya moja. Haya ni mafanikio makubwa katika
utekelezaji wa Haki za msingi za Binadamu.
Ndugu Wananchi;
Maadhimisho
haya yanatoa fursa nzuri kwetu sote kujiuliza; tumefanya nini katika
kipindi cha mwaka mzima na changamoto zinazokabili suala zima la Haki za
Binadamu. Tukumbuke kuwa utekelezaji wa Haki za Binadamu na Maadili ni
mchakato, hivyo siku zote ni lazima tuendelee kuboresha haki hizo, kama
vile ambavyo haki hizo pia huibuka na kuongezeka kila mara.
Napenda pia
kuwahakikishieni kwamba Serikali yenu inajitahidi kuhakikisha kuwa
wananchi wote hasa wale wa kawaida, wanapata msaada wa kisheria kwa
kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo:- Kuanzisha mchakato wa kuwa na
Sekretarieti ya Huduma za Kisheria; Kuboresha Mahakama za Mwanzo;
Kuanzisha Shule ya Taaluma ya Sheria na Kuongeza idadi ya majaji wa
Mahakama za Rufaa kutoka wanane mwaka 2005 hadi kufikia 14 mwaka 2012 ,
na wale wa Mahakama Kuu, kutoka 24 hadi 54.
Ndugu Wananchi;
Pamoja
na juhudi kubwa za Serikali kuboresha mazingira ya upatikanaji na
utoaji wa Haki za Binadamu nchini, matukio ya ukiukaji wa haki hizo
yameendelea kuongezeka. Taarifa za vyombo mbalimbali vya habari na
ripoti za kitafiti, zimeonesha na kuthibitisha uwepo wa matukio kadhaa
ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini. Baadhi ya matukio hayo ni kama
yale ya Ghasia zinazohusiana na vurugu za makundi; Mahabusu kuwekwa
rumande muda mrefu kabla ya kesi kusikilizwa; Unyanyasaji dhidi ya
wanawake na watu wenye ulemavu wa ngozi; Unyanyasaji wa watoto
(ikiwemo ukeketaji, ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni, mauaji kwa
wanaozaliwa na ulemavu, utekaji nyara, ajira mbaya nk.) Nawahakikishieni
kwamba Serikali imejipanga vema kukabiliana na kutokomeza uovu huo pasi
kumwonea huruma mtu yeyote anayejihusisha na maovu hayo.
Tukumbuke
kuwa watoto wanachukua nusu ya idadi ya Watanzania wote. Tunajua kwamba
mafanikio katika utekelezaji wa haki mbalimbali za mtoto, ni muhimu kwa
ukuaji na maendeleo ya nchi yetu hususan katika kufanikisha Malengo ya
Milenia. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha kwamba haki ya mtoto inalindwa
sio tu kutokana na kwamba tunaiwakilisha Serikali bali kama wazazi,
majirani na jamii kwa ujumla.
Leo
hii pia, tunajivunia kuzindua Mkakati wa Miaka Mitano wa Kuendeleza
Mageuzi ya Haki ya Mtoto 2013-2017. Tunazindua mkakati huu sambamba na
Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Haki za Binadamu kuonesha dhamira ya dhati ya Serikali kulinda, kuendeleza na kuhamasisha haki za watoto .
Mkakati
huu wa Haki ya Mtoto unaainisha hatua zinazopaswa kuchukuliwa na
mawizara idara, mawakala na CSOs kwa miaka mitano kuhakikisha watoto
wote ambao haki zao zimekiukwa, wanapata haki na kwamba mtoto yeyote
anayekwenda mbele ya vyombo vya sheria, aidha awe muhanga, shahidi au
aliyeonewa, anapata haki halali inayozingatia hadhi na utu wake kwa
wakati.
Ndugu Wananchi;
Nitumie
fursa hii pia kuwaasa Watanzania wenzangu kuanzisha kampeni maalum za
kukuza maadili katika ngazi mbalimbali zikiwemo zile za utumishi wa
umma, taasisi za dini, taasisi za elimu na katika nyanja zote za maisha
ya kila siku. Suala hili likifanyika vizuri, naamini sote kwa pamoja,
tutakuwa tumetimiza wajibu wetu wa malezi bora kwa watoto na vijana wetu
hali itakayosaidia kupunguza maovu mengi ndani ya jamii.
Ndugu Wananchi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kabla
sijahitimisha hotuba yangu, napenda kusisitiza kuwa usimamizi wa Haki
za Binadamu na ujenzi wa Maadili mema ndani ya jamii yetu, ni jukumu la
kila mmoja wetu. Kila mmoja wetu kwa namna moja au nyingine anawajibu wa
kulinda, kuheshimu na kudumisha Haki za Binadamu. Nawahakikishieni
kwamba Serikali ya Awamu ya Nne inatilia maanani sana suala la Haki za
Binadamu, Utawala Bora na Maadili. Tukishikamana katika hili naamini
tutashinda kwani “ Umoja ni nguvu”
Nawaasa
kujiepusha na mambo yote yanayochangia kwa njia moja ama nyingine,
kuvunja na kukiuka misingi ya Haki za Binadamu na Maadili mema. Kueni
raia wema na chukieni maovu.
Baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima natamka kuwa;Maadhimisho ya Sita ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Binadamu na Maadili, yamefunguliwa rasmi.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment