Hivi
karibuni The Citizen liliandika habari ya kushtua katika ukurasa wa
mbele, likielezea wasiwasi wa wataalamu na mabingwa kadhaa wa masuala ya
uchumi kuwa, Tanzania inakabiliwa na janga kubwa la mzigo wa madeni
iwapo Serikali haitapunguza kasi ya mikopo isiyokuwa na tija katika
kuinua uchumi.
Onyo la
wataalamu hao linatukumbusha jinsi janga la Deni la Taifa
lilivyoligharimu Taifa kiuchumi katika miaka ya 90, ambapo karibu
rasilimali zote ambazo Serikali ingezitumia katika utekelezaji wa miradi
ya maendeleo na pia kuziwekeza katika huduma muhimu za kijamii
zilielekezwa katika kulipa madeni. Ni aibu na ukweli ulio mchungu kwamba
ilipofika mwaka 2006, Deni la Taifa lilikuwa asilimia 70 ya Pato la
Taifa, ingawa msamaha wa madeni ulipunguza kiwango hicho hadi asilimia
21 mwaka uliofuata.
Hata hivyo,
kilichoendelea baada ya pale ni uthibitisho kwamba Serikali haikupata
fundisho kutokana na janga hilo, kwani ilizidisha kasi ya kukopa kiasi
kwamba
Deni la Taifa hivi sasa linakadiriwa kuwa kati ya asilimia 40 na 50
ya Pato la Taifa, ambalo linakadiriwa kuwa Sh50 trilioni. Ni vigumu
kuamini kwamba Deni la Taifa limekua kwa kasi ya kutisha kutoka Sh10
trilioni mwaka 2005 hadi Sh27 trilioni mwishoni mwa mwaka uliopita.
Kama
baadhi ya wataalamu wa masuala ya uchumi wanavyohadharisha, suala hapa
siyo Serikali kukopa, bali ni kwamba mikopo hiyo inayokadiriwa kuwa Sh2
trilioni kila mwaka inachukuliwa kufanya kitu gani? Takwimu za Benki Kuu
ya Tanzania (BoT), zinaonyesha kwamba Deni la Taifa lilipaa kwa Tsh5
trilioni kati ya Januari na Oktoba mwaka uliopita.
Mtaalamu
mmoja wa uchumi ametukumbusha jinsi miaka ya 70 Serikali ilivyokopa Sh96
bilioni kuanzisha Kiwanda cha Viatu Morogoro, lengo likiwa kuuza viatu
nchini Italia. Kutokana na kufilisika kilibinafsishwa miaka ya 90 na
hivi sasa majengo yake yamegeuzwa kuwa ghala, huku deni la uanzishwaji
wa kiwanda hicho likiwa limelipwa kupitia kodi za wananchi. Mfano
mwingine ni bajeti ya Sh122.4 bilioni ya kusambaza pembejeo za ruzuku
kwa wakulima kwa mwaka 2011/12, ambapo Tsh89 bilioni zilikuwa ni mkopo
kutoka Benki ya Dunia.
Taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imefichua uvundo na
ufisadi mkubwa katika mfumo mzima wa pembejeo za ruzuku. Kwa hiyo,
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inakutana leo kupokea na
kujadili ripoti hiyo. Kwa mfano, katika Kijiji cha Lunyala
, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa asilimia 70 ya wananchi
walioorodheshwa kupata mbolea walikuwa bandia, huku Benki ya Dunia
ikikaririwa ikisema asilimia 60 ya Bajeti ya pembejeo za ruzuku ililiwa
na mafisadi.
Kinachosikitisha
ni kwamba Deni la Taifa litalipwa na wananchi wote ingawa waliofaidika
nalo ni mafisadi na viongozi wachache walio serikalini na mashirika ya
umma. Lakini kinachosikitisha zaidi ni tabia ya Serikali kuendelea
kukopa kwa lengo la kuendeleza matanuzi na matumizi makubwa yasiyo ya
lazima.
Mfano
mzuri ni ziara fupi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mkoani Mtwara mwishoni
mwa wiki, ambapo aliongozana na ujumbe mkubwa kupita kiasi na magari ya
kifahari ya Serikali yasiyopungua 30. Sisi tunadhani unahitajika
mjadala mpana wa kitaifa kuhusu Deni la Taifa.Chanzo: mwananachi
No comments:
Post a Comment