Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro
Mawaziri
na Naibu Mawaziri walioteuliwa, jana waliapishwa na Rais Jakaya Kikwete
Ikulu jijini Dar es Salaam, kushika rasmi nyadhifa hizo na kuahidi
kufanya kazi kwa kasi katika kuwahudumia wananchi.
Rais
aliwapisha jana jioni Ikulu jijini Dar es Salaam kufuatia mabadiliko
aliyoyafanya katika Baraza la Mawaziri juzi na kutangazwa na Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Waziri
mpya wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro, alisema atahakikisha
anajenga misingi kuhakikisha Katiba mpya inakuwa ya watu. Alisema
atafanya hivyo, kwa kuwa Katiba siyo ya mtu mmoja wala ya chama kimoja,
bali ni ya Watanzania na vyama vyote.
Hivyo,
alisema atafanya kazi kwa kujituma na kwa umakini mkubwa na kwamba,
atazingatia miongozo ya mabadiliko ya katiba kufikia malengo hayo.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema ameteuliwa na Rais
Kikwete kusimamia sera na siyo kuchota fedha katika wizara
anayoisimamia.
Alitoa
kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari
kufuatia taarifa zilizoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari jana
kuwa ameteuliwa ili achukue fedha kutoka Hazina kwa ajili ya uchaguzi
mkuu wa mwakani.
Nchemba,
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania
Bara, alisema ana wasiwasi na uelewa wa baadhi ya watu wanaozungumzia
mtu anayeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha au kufanya kazi Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) kwamba anakwenda kuchota fedha.
Alisema
licha ya kuwa ni mtendaji wa CCM, atafanya kazi za kitaifa na kwamba,
anakwenda kufanya kazi ya kitaalamu, ambalo ni eneo la taaluma yake na
anaamini kwa kushirikiana na wenzake watapiga hatua.
Kuhusu
utegemezi wa bajeti ya serikali, alisema tatizo hilo linatokana na
sheria ya manunuzi ya umma, ambayo inataka yafanyike kwa njia ya zabuni.
Alisema
sheria hiyo imekuwa ikiisababishia serikali mzigo mkubwa, hivyo akasema
dawa pekee ya kuondokana nalo ni kuongeza ukusanyaji wa mapato na kubana
matumizi.
Alisema atamshauri Rais kuhusu sheria hiyo ili ifanyiwe uchambuzi wa kitaalamu kabla ya kuipeleka bungeni kufanyiwa marekebisho.
Waziri wa
Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema watajielekeza zaidi katika
kuhakikisha wananchi wanalipa kodi ili kuondokana na utegemezi.
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama, alisema
atashirikiana na wadau kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu,
ikiwamo upungufu wa madawati, walimu na vitabu.
Naibu
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, alisema
atawapa ushirikiano waandishi wa habari wote bila ubaguzi na kuendeleza
uhuru mkubwa wa habari na vyombo vya habari uliopo.
Naibu Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi, alisema atahakikisha
ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo zinapelekwa kwa wakulima kwa
wakati.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk.
Binilith Mahenge, naibu wake, Ummy Mwalimu; Naibu Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Kaika Telele; Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene, hawakuwapo kwenye hafla hiyo.
No comments:
Post a Comment