Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na timu maalum
inayohakiki maeneo mapya ya utawala kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Pichani kulia na timu yake ya
Mkoa iliyokuwa ikiratibu maeneo hayo ofisini kwake leo tarehe 17 Januari
2014. Timu hiyo kutoka TAMISEMI inaongozwa na Mwanasheria wa TAMISEMI Ndugu Eustard Ngatale (watatu kulia).
Katika
kikao hicho kifupi Mkuu huyo wa Mkoa ameiomba mamlaka husika kupitia
timu hiyo kuangalia upya vigezo vinavyotumika katika kugawa maeneo mapya
ya utawala na upandishaji wa madaraja kutoka kijiji, kata, Tarafa,
Halmashauri, Miji na Manispaa.
Alisema
kuwa kuna maeneo mengine ambayo yakiangaliwa kwa kigezo kimoja cha
wingi wa watu bila kuangalia umbali wa huduma na giografia ya eneo
husika unakuta wananchi wanakosa huduma zao za msingi na kupata tabu
kubwa katika kuzipata.
Alitolea
mfano vijiji vikubwa vya mwambao ambavyo kupata huduma katika kata zao
ni lazma wavuke upande mmoja wa Ziwa kwenda upande mwingine jambo ambalo
ni hatarishi kama ilivyotokea kwa wananchi wa Kijiji cha Kipwa Mwambao
mwa Ziwa Tanganyika ambao hivi karibuni walipoteza watu 15 katika ajali
ya boti walipokwenda kupata huduma ya afya. Wengi ya waliofariki katika
ajali hiyo mbaya walikuwa ni watoto chini ya umri wa miaka 5.
Kikao kikiwa kinaendelea ambapo kwa upande wake Mwanasheria wa TAMISEMI Ndugu Eustard
Ngatale alisema kuwa kubariki na kuhalalisha uanzishwaji wa maeneo
mapya ya Utawala vipo vitu mbalimbali vya kuzingatia ambavyo ni pamoja
na kuwepo kwa makubaliano ya wananchi na viongozi wa maeneo husika
kupitia mihutasari ya vikao maalumu vya kisheria vya WDC, Halmashauri,
DCC na RCC katika ngazi ya Mkoa. (Na Hamza Temba - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa @Rukwareview.blogspot.com)
No comments:
Post a Comment