Viongozi wa Chadema walipokuwa Kigoma kwenye Operersheni Pamoja Daima
Wakazi wa Kigoma waliojitokeza kwenye mkutano wa Operesheni Pamoja Daima.
CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepasua ngome ya mbunge wake, Zitto
Kabwe na kuzidi kujiimarisha kisiasa katika jimbo la Kigoma Kaskazini.
Timu ya
viongozi wa CHADEMA wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho
Zanzibar, Said Issa Mohamed, Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema na
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano, John Mnyika iliwasili jana na
kuitikisa Kigoma kwa mikutano ya M4C Operesheni Pamoja Daima.
Hamasa ya
wananchi wa Kigoma hususan katika Kata ya Mikongolo iliyoko katika jimbo
la Kigoma Kaskazini, ilijionyesha wazi baada ya timu hiyo kupokewa na
umati mkubwa wa watu waliokuwa wakiimba nyimbo za kukisifu chama hicho
huku wakilazimika kutembea umbali wa kilometa 3 kwenda eneo la mkutano
kutokea mahali ilipotua helkopta.
Kutokana
na umati wa wananchi kuwa mkubwa, watumiaji wengine wa barabara wakiwemo
waliokuwa wakiendesha magari, walilazimika kusimama pembeni mwa
barabara kupisha msafara huo wa viongozi, huku nderemo, vifijo pamoja na
ishara za salamu za chama hicho, zikitawala.
Wakihutubia
katika maeneo mbalimbali ya mkoani hapa wakianzia wilayani Uvinza
(Nguruka), Kigoma Kaskazini (Mikongolo na Kagunga) na Kigoma mjini,
viongozi hao wameendelea kuzungumzia ajenda za operesheni hiyo ambayo ni
pamoja na masuala ya mchakato wa katiba mpya, umuhimu wa Watanzania
kudai kuboreshwa kwa daftari la wapiga kura, matumizi ya rasilimali za
nchi kwa faida ya wananchi na hali ya ugumu wa maisha ambayo wamekuwa
wakiihusisha na uongozi mbovu unaosimamia sera zilizoshindwa.
Akizungumza
katika mikutano iliyofanyika jana katika maeneo mbalimbali ya Kigoma
wakianzia wilayani Uvinza (Nguruka), Kigoma Kaskazini (Mikongolo na
Kagunga) na Kigoma mjini, Makamu Mwenyekiti Mohamed alisema kuwa lengo
la operesheni hiyo ya CHADEMA awamu hii ni kuwatembelea wananchi nchi
nzima ili kujadiliana nao masuala hayo muhimu kwa taifa.
Mbali ya
kuwashukuru wananchi na hususan wanachama wa CHADEMA mkoani Kigoma kwa
kuendelea kusimama na kukipenda chama chao, Makamu Mwenyekiti huyo
alisema kuwa wameamua kuwa sauti ya Watanzania wanyonge katika masuala
yanayohusu mustakabali wao, hivyo hawataruhusu mtu yeyote, awe
mwanachama au kiongozi, kukiyumbisha chama kwa maslahi binafsi.
“Chama
chenu kimetambua kuwepo kwa hila na njama za kutaka kukisambaratisha.
Kuna watu waliingia kwenye chama hiki kwa ajili ya malengo ya
kukisambaratisha, bahati nzuri kwetu na bahati mbaya kwao ni kwamba
mbinu hizo zimefeli kwa sababu zimebainika,” alisema Mohamed huku
akionekana kuungwa mkono na watu wa Mkongolo.
Kwa upande
wake Mjumbe wa Kamati Kuu, Lema, aliwaasa Watanzania kuwa ili nchi yao
ikombolewe kuondokana na watu aliodai ni wakoloni weusi wanaofanya kazi
kwa mwavuli wa CCM, kunahitajika chama kimoja chenye nguvu ambacho
kitasimama imara kwa ushirikiano na wananchi wenyewe.
Lema pia
alitumia fursa ya mikutano ya jana kukemea propaganda za udini ambazo
zimekuwa zikienezwa mkoani humo na nchi nzima kwa ujumla zikitumiwa na
baadhi ya wanasiasa wanaofilisika na kuishiwa hoja kama ngao ya
kujikinga kila wanapotuhumiwa usaliti na kukosa uadilifu katika masuala
ya uongozi.
“Ndugu
zangu wana wa Kigoma naomba msishiriki katika dhambi ya udini
inayopandwa na baadhi ya watu wachache wasioitakia mema nchi yetu. Hii
dhambi haitatibika kamwe, kaeni mbali na uovu huu. Wanaoupanda wana
malengo yao…achaneni nao. Tujadilini mambo ya msingi yanayotukabili sote
kama Watanzania,” alisema Lema.
Naye
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano, Mnyika, alisisitiza kwamba chama
hicho kitaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kinidhamu kwa wanachama
wake hususan kwa viongozi ambao watabainika kwenda kinyume na taratibu
za chama hicho.
No comments:
Post a Comment