Kiemba akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao la pili |
SIMBA
SC wamefuzu kuingia Fainali ya Kombe la Mapinduzi, baada ya usiku huu
kuilaza mabao 2-0 URA ya Uganda kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Shujaa
wa Simba SC leo alikuwa ni kiungo mwenye kipaji, Amri Ramadhani Kiemba
aliyesababisha bao la kwanza na kufunga mwenyewe la pili.
URA
ilipata pigo mapema dakika ya 32 baada ya mshambuliaji wake hatari,
Owen Kasuule kutolewa nje kwa nyekundu ya moja kwa moja kwa kumchezea
rafu winga msumbufu wa Simba SC, Ramadhani Singano ‘Messi’.
Dakika
45 za kipindi cha kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana na
kipindi cha pili ndipo Simba SC inayofundishwa na Mcroatia, Zdravko
Logarusic ilipofungua makucha yake.
Kona maridadi ya Kiemba
ilimkuta beki Donald Mosoti, aliyemsetia beki pacha wake wa kati, Joseph
Owino akafunga bao la kwanza dakika ya 49.
Wakati URA wanahaha kusaka bao
la kusawazisha, Simba SC walifanya shambulizi zuri na krosi maridadi ya
Haroun Chanongo ikaunganishwa nyavuni na Amri Kiemba dakika ya 52
kuipatia Simba SC bao la pili.
Bao hilo liliinyong’onyesha kabisa URA, ingawa iliendelea kupambana kupata japo bao la kufutia machozi.
Kwa ujumla, URA iliathiriwa mno
na kutolewa na mshambuliaji wake hatari, Owen Kasuule, kwani ndiye
tegemeo lake la mabao kwa pamoja na Feni Ali.
Baada ya mechi, Kiemba alipewa king’amuzi cha Azam TV kwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Simba SC sasa itapambana na KCC ya Uganda pia katika Fainali Jumatatu Saa 10:00 Uwanja wa Amaan.
No comments:
Post a Comment