SIKU zote
tumezoea kuona baadhi ya wanasiasa na viongozi wakiwa mstari wa mbele
kupinga ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na hata kupinga ajira kwa
watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
Hali hiyo
imekuwa ni tofauti kwa Kigogo mmoja wa Chama Tawala CCM wilayani
Mbarali mkoani Mbeya ambaye mbali na kumtumikisha mtoto aliyechini ya
miaka 18 bali pia amemfanyia unyama na ukatili uliopitiliza kwa
kummwagia maji ya moto kwa kile kinachodaiwa kuwa mtoto huyo anakula
sana.
Kigogo
huyo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Kitongoji cha Mahango kijiji cha Mageya
kata ya Rujewa wilayani Mbarali aliyefahamika kwa jina la Ziada Bakari
Mwihesi anadaiwa kummwagia maji ya moto mtoto Agustino Sanga(12) ambaye
alikuwa akimtumikisha kwa kufanya kazi za kuchunga mifugo yake kuanzia
alfajiri hadi usiku bila kumpatia chakula cha uhakika.
Mtoto
Agustino ambaye ni yatima anayelelewa na bibi yake baada ya kufiwa na
wazazi wake huko wilayani Makete mkoani Njombe alianza kuishi na
Mwenyekiti huyo wa chama mwaka 2011 akitokea wilayani Makete mkoani
Njombe ambapo Bibi yake kutokana na kutokuwa na uwezo alimkabidhi mama
huyo ili aishi naye huku akimsaidia kazi za kuchunga mifugo yake.
Akizungumza
mkasa huo mbele ya mwandishi wa habari hizi aliyefika kijijini hapo
kufuatilia taarifa za unyanyasaji dhidi yake, mtoto huyo alisema kuwa
aliletwa nyumbani kwa mama huyo mwaka 2011 na Bibi yake akitokea
Wilayani Makete Mkoani Njombe ili aweze kufanya kazi ya kuchunga ng’ombe
kwa mwenyekiti huyo.
Alisema
kuwa tukio la kuunguzwa moto lilimtokea mwezi Juni 2013 shambani kwa
Mwenyekiti huyo eneo la Jangulutu majira ya usiku ambapo Mwenyekiti huyo
alianza kumsimanga kwa madai kuwa amekuwa akila chakula kupita kiasi na
kusababisha watoto wake kutoshiba.
Mtoto
Agustino aliendelea kusema kuwa, mama huyo aliendelea kumsimanga na
ghafla alichukua maji yaliyoinjikwa jikoni yakiwa yamechemka kwa ajili
ya kupika ubwabwa usiku huo na kummwagia kifuani na baadaye kumfungia
ndani huku akilia kwa uchungu.
Agustino
aliendelea kufafanua mkasa huo kwa kusema kuwa akiwa amefungiwa ndani
mama huyo alikuwa akisaga mifupa ya ng’ombe na kumpaka katika jeraha la
kidonda alichounguzwa na kwamba kila alipokuwa akimpaka ndipo kidonda
kilipozidi kutoa usaha.
Alisema
akiwa ndani Bibi yake alianza kumtafuta ndipo siku hiyo alipofika
nyumbani kwa Mwenyekiti huyo na kumuuliza alipo ambapo alimweleza kuwa
mjukuu wake aliungua moto alipokuwa akicheza karibu na moto.
Agustino
aliendelea kubainisha kuwa tangu alipofika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo
mwaka 2011 hajawahi kupumzika na kwamba amekuwa akitumikishwa kama Punda
kuanzia alfajiri hadi usiku huku akipewa chakula kidogo.
Kwa
upande wake Babu wa Mtoto huyo Method Ndelwa(55) Mkazi wa Kitongoji cha
Mahango alisema mtoto huyo baada ya kufika nyumbani hapo alikuja mume wa
Mwenyekiti aitwaye Seleleka Twasanga na kumuomba mtoto huyo awe
anamchungia ng’ombe na mbuzi shambani kwake.
Alisema
tangu mjukuu wake alipoungua mwaka 2013 mwezi wa 6 hakuna msaada
wowote ambao unatolewa na familia ya Mwenyekiti na kwamba ameendelea
kuugulia na majereha yake bila kupatiwa matibabu ya uhakika.
Alisema
kuwa hakuwa anajua utaratibu wowote wa kutoa taarifa hizo kwenye vyombo
vya sheria ikiwemo Polisi na kwamba tangu alipounguzwa moto walikuwa
wakimuangalia tu mtoto huyo huku wakishindwa kujua hatima yake.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mahango ambaye ndiye anayedaiwa
kufanya unyama huo,Ziada Mwihesi alikana kumchoma moto mtoto huyo na
kudai kuwa siku ya tukio alipigiwa simu na mume wake aliyemtambulisha
kwa jina la Seleleka kuwa mtoto Agustino ameungua moto ndipo
alipoondoka na kwenda shambani na kumkuta mtoto huyo akiwa ameungua
kifuani.
Hata
hivyo Mwenyekiti huyo anadai kuwa chanzo cha mtoto huyo kuungua ni
kutokana na kuota moto asubuhi wakati akipasha kiporo cha wali katika
jiko la kuni na kusema kuwa mtoto huyo alishaungua moto akiwa kwa bibi
yake na kudai kuwa hapo amekuja kuungua kwa mara ya pili.
Pamoja na
kufanya unyama huo Mwenyekiti huyo alionekana kutohitaji kutoa
ushirikiano kwa mwandishi wa habari hizi kwa kutoa majibu ya mkato
wakati alipokuwa akiendelea kuulizwa maswali juu ya kuchomwa moto kwa
mtoto huyo ambapo pia alikanusha kummwagia maji ya moto mtoto huyo kwa
madai ya kumaliza chakula.
Naye
Mume wa Mama huyo Seleleka Twasanga alikiri kuungua kwa mtoto huyo na
kudai kuwa yeye alipata taarifa baada ya kupigiwa simu na jirani yake
ambaye wapo jirani shambani kwamba Mtoto Agustino ameungua moto ndipo
alipoondoka na kwenda shambani ili kujua chanzo cha tukio hilo.
Bw.Twasanga
alisema wakati anamchukua mtoto huyo kwa Bibi yake walifanya kama
kubadilishana na Bibi huyo ambaye alihitaji kila mwaka alimiwe shamba la
heka mbili kwa ng’ombe wakati mtoto Agustino akifanya kazi ya kulima na
kuchunga Ng’ombe na mbuzi shambani kwa Twasanga.
Akielezea
zaidi mume wa mama huyo alisema aliendelea kumlimia shamba bibi wa
mtoto Agustino na kukiri kutomlipa chochote zaidi ya bibi huyo kulimiwa
shamba.
Chama Cha
Waandishi wa Habari wanawake TAMWA kimekuwa katika harakati za kupinga
ukatili wa kijinsia ikiwemo unyanyasaji wa wanawake na Watoto.
Mkurugenzi
wa TAMWA Valerie Msokwa kupitia jarida lake linalotolewa na taasisi
hiyo alisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria ya Kimataifa ya haki
ya mtoto ya mwaka 2009 iliyowekwa katika tamko la Umoja wa Mataifa la
Haki za Mtoto linalotoa mwongozo wa kulinda na kutambua haki za mtoto
nchini.
Alisema
watoto wanakabiliwa na changamoto nyingi hivyo wanapaswa kulindwa dhidi
ya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wanaofanyiwa watoto katika
maeneo mengi ya mijini na vijijini.
Naye
Diwani wa Kata y Rujewa Bi.Gurzar Sabil alipotakiwa kuzungumzia tukio
hilo la kinyama la mwenyekiti huyo alisema kuwa hana taarifa hiyo
lakini aliahidi kuwasiliana na Ofisa Ustawi wa jamii wilaya ya Mbarali
ili waweze kwenda nyumbani kwa mtoto waweze kumsaidia ikiwa ni pamoja na
kumkamata mtuhumiwa.
Mara
baada ya Mwandishi wa habari hizii kuondoka wilayani humo Ofisa Ustawi
wa Jamii wilaya ya Mbarali Winifrida Mahali akiambatana na Mratibu wa
Dawati la Jinsia wilayani humo Christa Komba walifika nyumbani kwa
Mwenyekiti huyo na kumchukua hadi kituo cha Polisi.
Bi Mahali
alisema kuwa walimfuata mtuhumiwa pamoja na mumewe na kuwapeleka kituo
cha polisi ambako walilala hadi asubuhi na kufikishwa katika mahakama
ya wilaya ya Mbarali ambako wamesomewa mashtaka ya kujeruhi na
wamerudishwa rumande baada ya kukosa dhamana hadi Januari 29.
No comments:
Post a Comment