Rais Jakaya Kikwete
Rais
Jakaya Kikwete hataweza kukamilisha uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu
la Katiba katika muda wa wiki mbili kama ilivyokuwa imekadiriwa awali,
kutokana na wingi wa majina yaliyopendekezwa kwa ajili ya uteuzi huo.
Ugumu wa
mchakato wa uteuzi wa wajumbe hao unatokana na Rais Kikwete kupokea
zaidi ya majina 5,000 yaliyopendekezwa na kuwasilishwa kwake kutoka
taasisi na asasi mbalimbali za kijamii, huku yeye akitakiwa kuteua
wabunge 201 tu, sawa na asilimia nne ya idadi ya majina
yaliyopendekezwa.
Wateule
hao wa Rais wataungana na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kuunda Bunge Maalumu la
Katiba, ambalo linatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi ujao mjini Dodoma.
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ameliambia gazeti hili kuwa ofisi
yake ina kazi ngumu ya kuchagua majina ya wajumbe watakaoingia kwenye
Bunge la Katiba na huenda kazi hiyo ikakamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Balozi Sefue alisema Januari 15 iliyotajwa na Rais Kikwete yalikuwa ni makadirio tu ya awali, lakini kazi bado ni ngumu.
“Makadirio
yangu ni mwisho wa mwezi huu (Januari). Ni kweli, Rais alitoa tarehe
hiyo, lakini yalikuwa ni mapendekezo ya awali tu,” alisema Balozi Sefue
na kuongeza:
“Hapa
kuna mapendekezo ya vikundi zaidi ya 600 na kila kikundi kimetoa majina
tisa; kwa hiyo kuna majina zaidi ya 5,400, kati yao tupate majina 200.
Tunahitaji muda mrefu ili tufanye kazi kwa ufanisi.”
Desemba
13 mwaka jana, Rais Kikwete alitoa tangazo kwa mujibu wa kifungu kidogo
cha (2A) cha kifungu cha 22 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya
83 akialika kila kundi kutoka pande zote za Muungano kuwasilisha kwake
majina kwa ajili ya kuzingatiwa kwenye uteuzi.
Mgawanyo wa wajumbe
Waziri wa
Katiba na Sheria, Mathias Chikawe hivi karibuni kuwa makundi ya kijamii
yalitakiwa kuwasilisha kwa Rais orodha ya majina ya watu wasiopungua
wanne na wasiozidi tisa kwa mujibu wa sheria.
Alibainisha
kuwa kila kundi linatakiwa kuzingatia umri, jinsia, uzoefu, sifa na
sehemu ya makazi ya mtu aliyependekezwa. Idadi ya wajumbe kutoka
Zanzibar haitapungua moja ya tatu ya wajumbe wote.
Chikawe
alisema wabunge hao 201 mchanganuo wao upo kwenye sheria na kwamba 20
watatoka kwenye taasisi zisizokuwa za kiserikali, ambapo nusu yao lazima
wawe wanawake na moja ya tatu kutoka Zanzibar.
Wengine ni wajumbe 20 kutoka taasisi zote za dini, wajumbe 42 kutoka vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu.
“Vipo
vyama 21 kwa maana hiyo, kila chama kitaleta wajumbe wawili, mgawanyiko
ni huohuo, kwa hiyo kwa vyama vya siasa hapa lazima mmoja atoke Zanzibar
na mwingine Bara na lazima mmoja awe mwanamke na mwingine mwanaume,”
alisema Chikawe.
Wajumbe
wengine na idadi yao kwenye mabano ni Taasisi za Elimu ya Juu (20),
makundi ya watu wenye ulemavu (20), vyama vya wafanyakazi (19), vyama
vinavyowawakilisha wafugaji (10), vyama vinavyowawakilisha wavuvi (10)
na vyama vya wakulima 20.
Mwakilishi wa Asasi
Mwakilishi
wa Asasi za kiraia, Marcosy Albanie alisema kuwa tatizo la kufurika kwa
majina linatokana na asasi nyingi kutokubali kuungana na kupeleka
majina machache.
“Kuna
jumla ya asasi za kiraia zaidi ya 66,000 nchini. Sisi katika muungano wa
asasi za kiraia tulikubaliana tukutane Dodoma ili tuchague watu
wachache. Lakini kuna taasisi zimejifungia ndani zikapeleka majina yao
wenyewe kwa ubinafsi wao,” alisema Albanie na kuongeza: “Kazi hapo kwa
Katibu Mkuu Kiongozi, achukue majina ya taasisi tuliokaa Dodoma na
kujadili kwa siku mbili, nyingine zikakaa zenyewe binafsi. Huo siyo
utaratibu wa kidemokrasia.”
Akizungumzia
utaratibu uliotumika kuwapata wajumbe hao, Albanie alisema kuwa
wamechagua watu 40 yaani wanawake 20 na wanaume 20 kwa kujali usawa wa
jinsia.
“Tumeangalia
sekta 11, kanda tisa, maana tunataka kila kanda iwakilishwe. Katika
kila kanda na sekta, majina ya watu wawili kwa aliyepata kura nyingi
zaidi. Jina la mwanamke na mwanaume kwa kujali usawa wa jinsia. Pale
tulipokosa mwanamke tumeweka wanaume wawili,” alisema Albanie.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema kuwa chama hicho kimezingatia sheria ilivyosema.
“Chadema
tumepeleka majina kwa mujibu wa sheria. Sheria ilisema majina
yasiyopungua manne na yasiyozidi tisa, tumefanya hivyo kwa kupeleka
majina manne. Ikulu waeleze ni chama kipi au taasisi ipi iliyokiuka
sheria na kivipi,” alisema Mnyika.
Aliongeza
kuwa chama hicho kilishatoa ushauri wa kurahisisha uteuzi ikiwa pamoja
na Serikali kutaja makundi na majina ya taasisi.
“Ndiyo
maana katika mapendekezo yao kwao juu ya muswada wa sheria, tulitaka
siyo tu sheria kutaja makundi kwa jumla, bali pia majina ya taasisi
zinazopaswa kufanya uteuzi na idadi ya wateule kwa kila taasisi,”
alisema.
Hivi
karibuni akitoa taarifa ya Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika
jijini Dar es Salaam, Mnyika aliwataja waliopendekezwa kuwa ni Profesa
Abdallah Safari, Mabere Marando, Nasra Juma Burhan na Method Kimomogoro.
“Marando
huyu ni msomi mwenye shahada ya Sheria na ni wakili wa Mahakama Kuu,
Kimomogoro ni msomi wa sheria na ni Wakili wa Mahakama Kuu, Profesa
Safari ni msomi mwenye Shahada ya Uzamivu aliyebobea kwenye mambo ya
sheria, vilevile ni Wakili wa Mahakama Kuu na mama Burhani ni mwalimu
kwa taaluma,” alisema Mnyika.
Chadema
kimekuwa kikikosoa mchakato huo, hali iliyofanya mwaka 2012 kwenda Ikulu
kukutana na Rais Jakaya Kikwete kikitaka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
kubadilishwa. Baada ya chama hicho, vyama vingine navyo vilialikwa
Ikulu na kuzungumza na Rais.
Naye
Naibu Natibu Mkuu wa Cham cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro amesema
kuwa chama hicho kimefuata sheria ilivyosema kuwa majina yasipungue
manne na yasizidi manne.
“Sisi
tumefuata sheria ambayo ilitutaka tupeleke majina manne hadi tisa.
Tumezingatia jinsi na ukanda kwa kuteua nafasi za wanaume sawa na
wanawake. Hata hivyo, siwezi kukwambia idadi wala kutaja majina kwa
sababu sera ya chama hairuhusu,” alisema Mtatiro.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment