Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, January 19, 2014

VIONGOZI WA DINI WAMALIZIA ZIARA YAO SONGOSONGO

 Makamu Mkurugenzi Uzalishaji, Songas , Mhandisi Elias Mnunduma, akiwaeleza baadhi ya viongozi wa dini pichani, namna uzalishaji wa
gesi katika mitambo ya kuzalisha gesi ya Songas katika kisiwa cha Songosongo unavyofanyika
 Baadhi ya viongozi wa dini katika picha ya pamoja na mtaalamu wa uzalishaji Songas Mhandisi Elias Mnunduma baada ya kupata maelezo namna shughuli nzima ya uzalishaji inavyofanyika katika mtambo huo
ikiwemo pia masuala ya usalama wa wafanyakazi na wageni wanaotembelea mahali hapo.
 Mtaalamu wa Masuala ya Gesi  na Msimamizi Mkuu wa Mitambo ya Kusafisha Gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Sulatan Pwaga, akiwaeleza viongozi wa dini kuhusu mradi wa eneo linapojengwa mitambo ya kusafisha gesi.
 Viongozi wa dini wakiwasili katika ofisi za kijiji cha Songosongo. Wakiwa ofisini hapo, viongozi hao walipata taarifa kuhusu namna kijiji kinavyofaidika kwa kuwepo wa uwekezaji wa gesi kijijini hapo, ambapo kijiji hicho kimefaidika kwa  umeme na maji bure.
Pichani ni moto unaotoka wakati wote uzalishaji  wa gesi unapoondelea katika mitambo. Kwa mujibu wa wataalam wa mtambo huo, moto huo unaonesha kwamba gesi ipo inazalishwa na vilevile uwepo wake unaashiria usalama wa mitambo na watu wanaofanya shughuli katika mtambo huo.

========  ======= =======
VIONGOZI WA DINI WAMALIZIA ZIARA YAO SONGOSONGO
Na Asteria Muhozya, Songosongo, Kilwa.

Viongozi wa dini wamemaliza ziara yao ya kutembelea
shughuli mbalimbali katika sekta ya gesi na mafuta kwa kutembelea kisiwa cha Songosongo eneo la kwanza kuzalisha gesi asilia.

Wakiwa kisiwani humo walifanikiwa kukutana na uongozi wa kijiji cha Songosongo ambapo walipata taarifa mbalimbali za namna mradi wa
gesi ulivyokinufaisha kisiwa hicho ikiwemo pia mipango ya baadae ya kuendeleza eneo hilo.

Akieleza kuhusu manufaa yaliyoyopatikana kisiwani humo kutakana na kuwepo uwekezaji wa gesi, mjumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii
Kijijini hapo Bibi Chiku Abdalah alieleza kuwa, mbali ya kupata umeme na maji bure, kijiji kimefaidika na huduma nyingine za jamii ikiwemo wanafunzi kupata msaada wa elimu pamoja na afya.

“ Tunawashukuru Pan Afrika na Songas, wanatujali wanatusaidia elimu za watoto wanatupatia maji, tunashirikiana nao vizuri’,Alisema. Naye Mjumbe  kamati ya Mipango, Uchumi na fedha kijijini hapo Bw. Yussufu Faraki alieleza kuwa, tayari shule ya chekechekea imejengwa kijijini hapo na fursa za ajira kwa vijana zimepatikana.

“Tunakwenda vizuri na Songas na Pan Afrika, wamekarabati shule, wametuwekea watu wa mahusiano, walituletea mkunga, wanalipa ada. Tunakubali changamoto zipo lakini kila mmoja anamhitaji mwenzake alisema Faraki.

Akielezea kuhusu ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava alisema kuwa, wamefika kijijini hapo kuona shughuli za maendeleo zinazotokana na uwekezaji katika sekta ya gesi asilia na kujenga uelewa mpana kuhusu uwekezaji wa gesi na faida zake kwa maendeleo ya eneo la uwekezaji ikiwemo pia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Kikirsto Tanzania (CCT) na Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Kongamano la viongozi wa dini Bw. John Mapesa alisema kuwa, Elimu ya Songosongo imejulikana kwa viongozi wa dini na namna wananchi wa eneo hilo wanavyoizungumzia sekta  ya gesi na namna walivyonufaika nayo.

“Tumepata elimu ya kufaa, tunapoelekea katika kongamano letu, tutajua namna  nzuri ya kuishauri Serikali na Wizara katika sekta hizi  kwa
Maendeleo ya Taifa”. Alisema.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Jamii wa  Kampuni ya Songas Bw. Nicodemus Chipakapaka alieleza kuwa, Songas mbali na uchimbaji imejikita katika kutoa huduma za jamii kupitia elimu, afya ambapo shirika hilo limekuwa likigharamia wanafunzi wanafaulu kuendelea na masomo ya sekondari kijijini hapo. Mbali na hayo alieleza kuwa, Songas wamefanikiwa kuboresha zahanati ya kijiji,  ikiwemo pia kuwezesha uwepo wa wahudumu wa afya wanaohudumia wananchi kijijini hapo.

Akieleza namna shirika la Pan Africa linavyosaidia katika shughuli za maendeleo kijijini hapo , Afisa Maendeleo ya Jamii wa Shirika hilo Bibi. Tura David alieleza kuwa, pamoja na mambo mengine, kwa kuzingatia umuhimu wa elimu na namna utakavyowanufaisha wana Songosongo, Shirika hilo limeanzisha mpango wa kuwasaidia wanafunzi 10 kila mwaka wanafaulu vizuri zaidi na kuwaendeleza katika shule zilizopo nje ya Songosongo na nje ya Wilaya hiyo.

“Tunaamini mpango huu utasaidia na kuwa mfano mzuri wa uwepo wa gesi mahala hapa. Tunataka kujenga kizazi kilichoelimika.” Wenzetu wa Songas wameanzia chini zaidi kwa kuwaangalia wote wanaofaulu, sisi tunataka kupata walio wanafunzi bora zaidi.” Alisema.

Aidha, aliongeza kuwa, tayari Shirika hilo limejenga Bweni la wasichana kijijini hapo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 55.

Akielezea zaidi kuhusu mradi wa gesi na mahali panapojengwa mitambo ya gesi, Mtaalamu wa Masuala ya gesi na Msimamizi Mkuu wa Mitambo ya Kusafisha Gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)  Mhandisi Sultan Pwaga alieleza kuwa, mitambo mipya inayojengwa ya kuzalisha gesi kisiwani humo inatarajiwa kuzalisha futi za
ujazo milioni 140 kwa siku,  uzalishaji wa umeme wa zaidi ya megawati 10 , ambapo pia kutakuwa na mtambo wa kukandamiza gesi,  na mtambo wa kusafisha maji ya wastani wa lita 60,000 kwa siku ambapo wananchi wa Songosongo wanatarajiwa kufaidika na huduma za maji hayo.

Aidha, Makamu Mkurugenzi uzalishaji  Songas, Mhandisi Elias Mnunduma alieleza kuwa, kwa sasa eneo hilo la Songosongo linazalisha kiasi cha gesi cha futi za ujazo milioni 105 kwa siku ambapo asilimia 80 ya gesi inauzwa Tanesco kwa ajili ya kuzalisha umeme na asilimia 20 inapelekwa viwandani.

No comments:

Post a Comment