Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, February 11, 2014

KAMPENI UCHAGUZI MDOGO WA UBUNGE KALENGA KUANZA WIKI IJAYO...

 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepanga ratiba ya Uchaguzi mdogo katika jimbo la Kalenga katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ambapo siku ya kupiga kura itakuwa Jumapili ya Machi 16, mwaka huu na kampeni zitaanza wiki ijayo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Mallaba alisema kuwa uteuzi wa wagombea ubunge, utafanyika Februari 18, ambapo kampeni za uchaguzi zitaanza Februari 19 hadi Machi 15 mwaka huu.
"Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuiarifu uwepo wa nafasi wazi ya ubunge katika jimbo hilo, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, William Mgimwa aliyefariki dunia Januari mosi mwaka huu," alisema.
Alisema baada ya taarifa hiyo, Tume imepanga ratiba hiyo, ambapo wagombea wanatakiwa kuwasilisha fomu za uteuzi kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kalenga siku ya uteuzi kabla ya saa 10.00 alasiri.
"Tume inawataarifu wananchi wote pamoja na vyama vya siasa kufuata ratiba iliyotolewa pamoja na kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia siku ya uteuzi hadi siku ya kupiga kura ili watimize haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka," alisema.
Aidha, Tume hiyo imewasisitiza wananchi wote katika maeneo husika, kujitokeza kukagua taarifa zao wakati wa kuweka wazi Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kuona kama kuna marekebisho madogo yanahitajika kufanyika, kuwawezesha kupiga kura bila malalamiko yoyote. Mallaba alisisitiza kwamba hakutakuwa na uandikishaji mpya wa wapiga kura.
Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha rasmi Godfrey Mgimwa (32) kuwa mgombea wa uchaguzi katika Jimbo la Kalenga mkoani Iringa huku kikivitaka vyama vingine kutanguliza ustaarabu mara kampeni zitakapoanza.
Akimtambulisha mgombea huyo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema CCM imejipanga kuchukua jimbo hilo kwa kishindo, kama ilivyofanya katika uchaguzi mdogo wa madiwani, uliofanyika hivi karibuni, ambapo chama hicho kimeshinda viti 24 kati ya 27 vilivyokuwa vikigombaniwa.
Aidha Nape alisema pia CCM imemteua Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho upande wa Tanzania Bara,  Phillip Mangula kuwa Mratibu wa shughuli zote za kampeni za chama hicho katika jimbo hilo, lililoachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa.
Nape alisema wamepanga kamati ya siasa ya Wilaya ya Iringa Vijijini  na kamati ya siasa ya mkoa, kuwa ndizo zitakazosimamia kampeni za mgombea huyo, zinazotarajiwa kuanza Februari 19 na baadae uchaguzi utakaofanyika Mach 16 mwaka huu.
"CCM haitavumilia vurugu za aina yoyote,  kama ilivyojitokeza katika uchaguzi wa madiwani sehemu mbalimbali, matarajio wenzetu watakuja na ustaarabu wenye lengo la kufanikisha uchaguzi ufanyike salama," alisema Nape.
Aidha, alisema CCM itashinda uchaguzi huo kwa asilimia kubwa, kama ilivyofanya mwaka 2010 iliposhinda kwa asilimia 85 ya kura zote zilizopigwa.

No comments:

Post a Comment