skip to main |
skip to sidebar
Katiba mpya mbadala yaandikwa mafichoni
Mwandishi WetuToleo la 337
5 Feb 2014
Maprofesa, majaji wachambua taarifa nyeti za Warioba
CCM sasa kuingia Bunge la Katiba na rasimu mbadala
WIKI takriban mbili kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba, mjadala wa
muundo wa serikali tatu uliopendekezwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba
mpya umeendelea kupasua vyama vya siasa, Raia Mwema ikielezwa kwamba
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeandaa rasimu mbadala ndani ya Bunge hilo
la Katiba.
Kwa mujibu wa habari za uhakika zilizolifikia gazeti
hili, CCM ni kama vile imetengeneza tume yake ya Katiba mpya
inayoshikirisha jopo la maprofesa, majaji na baadhi ya wanasiasa.
Kati ya taarifa wanazotumia kutengeneza rasimu hiyo mbadala ya Katiba
ni viambatanisho vya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inayoongozwa na Jaji
Joseph Warioba, viambatanisho ambayo pia walikabidhiwa Rais Jakaya
Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.
Mbali na hao
wengine waliokabidhiwa viambatanisho hivyo sambamba na Rasimu ya Pili
ya Katiba mpya ni viongozi wengine mbalimbali wa kitaifa, akiwamo Waziri
wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro.
Ndani ya ‘tume’
hiyo ya CCM aliyepata kuwa mwanasheria mkuu wa serikali (AG) Andrew
Chenge, anatajwa kuwamo na inaelezwa kwamba, ‘tume’ hiyo inalenga kuibua
mawazo mbadala na yale ya Tume ya Warioba, hususan muundo wa serikali
tatu ndani ya Muungano.
Tayari, Rais Jakaya Kikwete, katika
hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 37 ya CCM mkoani Mbeya
Jumapili iliyopita alisema msimamo wa CCM ni serikali mbili na
anayewapinga anapaswa kuibua hoja mbadala zenye ushawishi na si kutumia
mabavu, akisisitiza hoja hazifutwi kwa “kupigwa rungu” bali hufutwa kwa
kutumia hoja mbadala zenye mantiki.
“Kinachofanywa na CCM ni
kutengeneza mawazo au mapendekezo mbadala yenye mantiki zaidi. CCM
haing’ang’anii mwonekano wa sasa wa serikali mbili. Ndani ya mwonekano
wa sasa kuna imani kwamba yapo mabadiliko yanayoweza kufanywa ambayo pia
yanaweza kuungwa mkono na wapinzani, lakini ni mabadiliko ambayo si ya
moja kwa moja kwenda kwenye serikali tatu kama ilivyopendekeza Tume ya
Warioba,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Inaelezwa kwamba
huenda CCM ikaibua mawazo mbadala wa muundo wa serikali ambayo chanzo
chetu cha habari kimeelezea mawazo hayo mbadala kuwa ni “mawazo ya kati,
yasiyo na msimamo mkali kuhusu muundo wa Muungano.”
Lakini
wakati CCM ikiwa katika juhudi za kuingiza rasimu mbadala kwenye Bunge
la Katiba, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinashikilia
msimamo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.
Katika msimamo wake, CHADEMA hakina mapendekezo mbadala kuhusu serikali
tatu, bali kinaungana na yale ya Tume ya Warioba, kama ilivyo kwa vyama
vingine vya upinzani, hususan vyenye wabunge bungeni.
Hali
hiyo inajitokeza katika wakati ambao vyama hivyo vya siasa chini ya
Ofisi ya Msajili wa Vyama vikitaraji kukutana Februari kesho, kujadili
nafasi yao katika Bunge la Katiba.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Msajili wa Vyama, Jaji Francis Mutungi, vyama hivyo vitakutana kupitia
chombo chao maalumu, kinachoitwa Baraza la Vyama vya Siasa, kikiwa ni
chombo cha kisheria ambacho wajumbe wake ni viongozi wa kitaifa wa vyama
vya siasa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar walioteuliwa kuwakilisha
vyama vyao.
Katika hatua nyingine, duru za kisiasa kutoka
Zanzibar zinaarifu kwamba tafsiri ya mambo kuhusu serikali tatu au
serikali mbili imebadilika, baada ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa
uwakilishi katika Jimbo la Kiembesamaki, ambako Mahmoud Thabit Kombo wa
CCM ameshinda baada ya jimbo hilo kuachwa wazi kutokana na kufukuzwa
kwa mwakilishi wa awali, Mansoor Himid.
Vyanzo kadhaa vya habari vinabainisha kwamba uchaguzi huo ulibeba tafsiri kubwa kuhusu mijadala mizito ya kisiasa Zanzibar.
Wengi wanasema ushindi wa Kombo ambao msingi wake ni wapiga kura wa
ngazi ya chini na si safu ya viongozi wa juu pekee, tafsiri yake ni
ushindi wa serikali mbili, ikielezwa kwamba Kombo ni muumini wa serikali
mbili na alihojiwa na kuthibitisha hivyo katika Kamati Kuu ya CCM
iliyoketi Zanzibar mwezi uliopita kwa ajili ya uteuzi wa mgombea wa
jimbo hilo.
Mansoor Himid aliyefukuzwa, aliweka wazi msimamo
wake kwamba si tu serikali tatu, bali Zanzibar kuwa na mamlaka yake
kamili, akitajwa kuungwa mkono na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani
Abeid Karume.
“Matokeo ya uchaguzi huo mdogo maana yake ni
kwamba watu wa chini hawana tatizo na hoja za aina ya serikali, bali
hizi ni hoja za viongozi wa kitaifa tu. Uchaguzi huu ulikuwa na kambi
mbili tofauti na ulikuwa kipimo mbele ya wananchi kwamba kambi ipi
inakubalika.
“Kambi ya kwanza ni ile iliyokuwa ya Mansoor. Na
unapomwona Mansoor ni dhahiri Karume yupo. Lakini kambi ya pili ni Dk.
Shein (Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein) na CCM kwa ujumla,
ambamo wamo watu kama kina Seif Khatib na wengineo. Kambi hizi zilikuwa
zikipimwa kwa hoja ya serikali tatu, ndani yake madai ya mamlaka kamili
ya Zanzibar na nyingine ni hoja ya serikali mbili. Ushindi umekwenda kwa
kambi ya CCM,” kilieleza chanzo chetu cha habari.CHANZO GAZETI LA RAIA MWEMA
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/katiba-mpya-mbadala-yaandikwa-mafichoni#sthash.aOGnCHBH.dpuf
No comments:
Post a Comment