![]() |
| Mke wa Rais Jacob Zuma, Nompumelelo Ntuli (MaNtuli).PICHA|MAKTABA |
Dar es Salaam. Mtanzania Stephen Ongolo anayekabiliwa na madai ya
kutishia kutoa siri za mke wa Rais Jacob Zuma, Nompumelelo Ntuli
(MaNtuli), huenda akarudishwa nchini na kuzuiwa kuitembelea Afrika
Kusini milele.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Tawi la Uchunguzi wa Kesi, katika Jimbo la Kwa
Zulu-Natal, Brigedia Clifford Marion, wakati kesi ya Ongolo ilipokuwa
ikisikilizwa katika Mahakama ya Camperdown, jijini Durban.
Ilielezwa kuwa, Ongolo si raia wa Afrika Kusini na kwamba alirudi nchini
humo Januari 19 mwaka huu baada ya kurejea kutoka katika mizunguko yake
katika nchi kadhaa za Afrika zikiwamo, Tanzania, Malawi, Msumbiji na
Ethiopia.
Ilielezwa kuwa visa yake inamalizika Februari 18 mwaka huu.
“Atarudi nchini mwake Tanzania na hatarudi tena Afrika Kusini,” alisema Marion.
Chanzo chetu cha habari kilichohudhuria kesi hiyo, kilisema Brigedia
Marion alihojiwa kuhusu taarifa za mashtaka dhidi ya Mtanzania huyo
ambapo alitoa ushahidi kuwa Ongolo amekuwa akituma ujumbe mfupi kwenye
simu ya MaNtuli, akimtishia kuwa atatoa siri kuhusu uhalali wa mtoto
wake (MaNtuli).
Inadaiwa kuwa Ongolo katika ujumbe wake alidai kuwa mtoto mmoja wa MaNtuli si wa Rais Zuma.
Kabla ya kukamatwa, Ongolo alikwenda katika vyombo vya habari kadhaa vya
nchini humo na kudai kuwa, anafahamu siri nzito kati ya MaNtuli na
Phinda Thomo, aliyekuwa mlinzi wa MaNtuli.
Thomo, alikutwa amejiua mwaka 2009 bafuni kwake, lakini Ongolo anadai
kuwa Thomo hakuuawa na badala yake, kifo chake kilipangwa kutokana na
uhusiano wa siri kati yake na MaNtuli.
Mashtaka ya kutishiwa kuvujisha siri zake, yalitolewa na MaNtuli ambaye
alidai kuwa Ongolo amekuwa akimlazimisha kumkutanisha kibiashara na Rais
Zuma.
Brigedia Marion alitoa ushuhuda mahakamani na kuiomba mahakama kukataa
kutoa dhamana kwa Ongolo ambaye alikamatwa mwishoni mwa Januari mwaka
huu.
“Tofauti na inavyoandikwa kwenye magazeti, Ongolo alikamatwa baada ya
kufika ofisini kwangu akija kulalamika kuwa kuna kesi ya wizi na uvamizi
kwenye nyumba ya dada yake ambayo inasimamiwa vibaya,” alisema Brigedia
huyo.
Alisema, Ongolo alipofika ofisini hapo alijitambulisha kama Stephen
Ongolo lakini baadaye alibainika kama Stephen John Masunga ndipo Marion
akalikumbuka jina kwani MaNtuli alikuwa ameshawasilisha mashtaka hayo
polisi.
“Kukamatwa kwake ilikuwa ni bahati. Nilipoona jina ni lilelile,
nikaangalia namba ya simu niliyopewa na MaNtuli na kuanza kuipiga na
simu ya Ongolo ikaita na hapohapo nikamweka chini ya ulinzi,” alisema
Marion.
Ilidaiwa kuwa baada ya Ongolo kukamatwa, simu yake na hati ya kusafiria
vilichukuliwa na alipotakiwa kumpigia simu wakili wake, hakufanya hivyo
na badala yake alimpigia simu mwandishi wa habari wa gazeti la Sunday
Independent, Nathi Olifant.
Marion alisema, alikusanya ujumbe mfupi kutoka kwenye simu za Ongolo na
MaNtuli na kubaini kuwa wawili hao waliwahi kukutana mwaka 2010.
Source: Mwananchi


No comments:
Post a Comment