Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, February 4, 2014

Msekwa: Wapinzani wakiungana wanaweza kuing’oa CCM



 
Kiongozi Mstaafu wa CCM, Pius Msekwa.PICHA|MAKTABADar es Salaam. Kiongozi Mstaafu wa CCM, Pius Msekwa amesema endapo vyama vya upinzani vikiungana na kuweka mikakati makini ya muda mrefu, vinaweza kuking’oa CCM madarakani.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na mwandishi wetu jana, Msekwa alisema kwa mtindo wa sasa wa vyama vya upinzani kila kimoja kusimama peke itakuwa ndoto kukishinda CCM.
“Kama vyama vya upinzani vinataka kuwe na upinzani wenye nguvu dhidi ya CCM ni lazima viungane vyote. Tena viweke mikakakati ya muda mrefu ya kujiimarisha,” alisema Msekwa kwenye mahojiano hayo.
Hata hivyo, alisema kuiondoa CCM madarakani siyo kazi rahisi kwa sababu mizizi yake imeenea kila kona ya nchi huku akisema wazo la upinzani kuungana halitakuwa rahisi kwa kuwa wengi wao ni walafi wa madaraka na hakuna atakayekuwa tayari kuvunja chama chake na kuunda kimoja kwa hofu ya kukosa uongozi.
Akijibu swali kuhusu nguvu ya Chadema kwa sasa Msekwa alisema: “Wanapambana na CCM kwenye majukwaa ya kisiasa lakini si kuwa na watu wengi wanaokiunga mkono.”
Alisema CCM kina mizizi hadi ngazi za chini kabisa nchi nzima tofauti na vyama vingine.
Alisema Chadema kiko katika baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara wakati Zanzibar hakina nafasi, tofauti na CUF ambacho alisema angalau kinaonyesha kuwa na nguvu visiwani huko.
Kuhusu Chadema kuwa na wabunge wengi Tanzania Bara, Msekwa alisema ni neema iliyokiangukia baada ya CCM kufanya makosa ya uteuzi kwa baadhi ya majimbo.
Msekwa ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge alisema pamoja na neema hiyo, Chadema hakiwezi kufikia asilimia 40 ya wabunge wote.
“Kweli Chadema kimejitahidi lakini ukichunguza utabaini ni neema iliyowaangukia kutokana na makosa ya CCM kuteua watu ambao wapigakura walikuwa hawawataki,” alisema Msekwa.
Alisema Chadema kimekuwa kikionekana kufanya vizuri kwenye siasa za majukwaani kwa sababu kina nafasi kubwa ya kukosoa na hata kutoa madai ya kutunga dhidi ya CCM ili mradi yawe yanawagusa wananchi.
Kuhusu uwezekano wa vyama vya upinzani kuchukua nchi kutokana na CCM kuwa na makundi mengi ambayo yanaweza kukisambaratisha katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 Msekwa alisema: “Hakuna mtu anayeweza kuondoka CCM na kuivunja nguvu. Hata akiwa ni kiongozi mwenye nguvu ya kisiasa kiasi gani ataondoka mwenyewe na CCM kubaki imara.”CHANZO MWANAINCHI

No comments:

Post a Comment