Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, February 5, 2014

Raia wa China wakana kuhonga polisi mamilioni

POLISI_3affb.gif
Raia Watatu wa China, Huang Gin, Xu Fujie na Chen Jinzha wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, wamedaiwa kutoa hongo ya Sh30.2 milioni kwa Polisi ili wasiwakamate.
Hayo yalibainika jana wakati Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka akishirikiana na Wakili Faraja Nchimbi kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mfawidhi, Isaya Arufani.
Wakili Nchimbi akisoma maelezo ya awali, alidai Novemba 2, 2013 washtakiwa hao walikamatwa na polisi, ASP Joel Lugaye, D/SSGT Gerwin na Simon Saye wakiwa na nyara za serikali na kwamba walitoa hongo ya Sh30.2 milioni kwa askari hao ili wawaachie.
Alidai kuwa baada ya washtakiwa hao kutoa kiasi hicho cha fedha, askari hao waligoma kukipokea na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi na hatimaye kuwafungulia mashtaka hayo yanayowakabili.
Akiendelea kusoma maelezo hayo ya awali, Wakili huyo alidai kuwa washtakiwa hao walipekuliwa na kukutwa wakimiliki ganda la risasi iliyotumika kinyume cha sheria.
Siku hiyo ya tukio, washtakiwa hao wanadaiwa kukutwa wakiwa na nyara za serikali aina ya pembe za ndovu, shehena ya Pinde 706, vyenye uzito wa kilo 1880 zikiwa na thamani ya Sh5 bilioni.
Wakili huyo wa serikali alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao wakati wakihojiwa polisi wakiri kufanya makosa hayo, lakini walipokuwa wakisomewa maelezo hayo ya awali waliyakana yote.
Maelezo hayo yalisomwa huku mkalimani akiyatafsiri kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kichina kutokana na washtakiwa kutokujua lugha ya Kiswahili ama Kingereza ili waweze kuelewa kila kilichokuwa kikiendelea mahakamani hapo.
Baada ya maelezo hayo ya awali kusomwa, Hakimu Mfawidhi, Isaya Arufani aliwauliza washtakiwa hao ni maelezo yapi wanayoyakubali na yapi wanayakataa yanayohusiana na mashtaka hayo yanayowakabili.
Washtakiwa hao, kupitia mkalimani walikubali maelezo yao binafsi na kuyakataa mashtaka yote yanayowakabili. Upelelezi wa kesi hiyo ulikamilika Januari 28, 2014.
Washtakiwa hao, kupitia kwa mawakili wao, Edward Chuwa na Richard Rweyongeza waliwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakiomba wapewe dhamana, baada ya Mahakama ya Kisutu kuwanyima dhamana kutokana na kutokuwa na uwezo wa kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Katika maombi hayo ya dhamana namba 14 ya mwaka 2013, Wachina hao kupitia kwa mawakili wao, wanadai kuwa dhamana ni haki yao kwa mujibu wa Katiba ya Nchi. Yanasikilizwa na Jaji Rose Teemba.
CHANZO:MWANANCHI

No comments:

Post a Comment