THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
Fax: 255-22-2113425 |
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
![]() |
| Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akikabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei, hundi ya shilingi milioni 100 kutoka benki hiyo kusaidia waathirika wa mafuriko yaliyozikumba wilaya tatu za Kilosa, Mvomero na Gairo. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Jumanne, Februari 4, 2014, amepokea hundi ya Sh. milioni 100 kutoka
Benki ya CRDB kusaidia wahanga wa mafuriko yaliyozikumba wilaya tatu za
Kilosa, Mvomero na Gairo katika Mkoa wa Morogoro, mwezi uliopita.
Rais
Kikwete amekabidhiwa hundi hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dkt.
Charles Kimei katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, na
kuhudhuriwa pia na Mhesimiwa William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia pia masuala ya maafa.
Akizungumza
kabla ya kukabidhi hundi hiyo kwa Rais Kikwete, Dkt. Kimei amesema kuwa
fedha hizo ni sehemu ya Sh. Milioni 850 ambayo ni asilimia moja ya
faida ya Benki hiyo ambayo hutengwa kila mwaka kwa ajili ya kuunga mkono
shughuli za jamii.
“Sote
tumeona madhara makubwa yaliyosababishwa na mafuriko haya. Watu wengine
wamepata hasara – akinamama, watoto, wajawazito na wazee. Hawa wote
wanahitaji misaada ya ziada ili kukabiliana na athari za mafuriko hayo,” amesema Dkt. Kimei.
Akizungumza
kabla ya kupokea hundi hiyo, Rais Kikwete ameelezea kwa ufupi mafuriko
hayo yaliyotokea alfajiri ya Januari 22, mwaka huu, 2014 na athari
ambazo zimetokana na mafuriko hiyo katika maeneo ya Magole, Dakawa na
Mateteni huko Dumila, Wilaya ya Mvomero, ambayo aliyatembelea mwishoni
mwa mwezi uliopita kujionea madhara.
“Waswahili
husema kuwa ajali haina kinga na ni kweli. Unajua mafuriko yaliyotokea
katika eneo la Dumila hayakutokana na wala na mvua ya pale. Mvua
ilinyesha kule Kiteto, Mkoa wa Manyara, lakini walioathirika kwa
mafuriko ni hawa jamaa zetu wa Dumila. Bahati tu ni kwamba mafuriko hayo
yalilikumba eneo hilo alfajiri wakati watu tayari wameamka na ndio
maana hakuna mtu aliyepoteza maisha yake katika eneo hilo,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Watu
wamepata hasara kubwa. Baadhi nyumba zao zimesombwa na kuzolewa na
maji, nyingine zimebomoka, watu wamepoteza mali zao nyingi kama vile
nguo na wengine hata chakula chao kimesombwa na maji. Wanahitaji msaada
na kwa kweli sisi katika Serikali tunaishukuru sana CRDB kwa kutoa
msaada huu kwa sabababu unachangia katika jitihada za Serikali
kukabiliana na tatizo hili.”
Akizungumza
katika shughuli hiyo, Mheshimiwa Lukuvi amesema kuwa tathmini mpya
imeonyesha kuwa watu walioathirika katika mafuriko hayo ni 9,268 na
kati ya watu hao kaya 522 hazina makazi kabisa baada ya nyumba zao
kubomolewa na maji, nyingi zaidi 466, zikiwa katika Wilaya ya Kilosa.
Amesema
kuwa nyumba 537 zimeharibika hata kama wenye nyumba hizo bado
wanaendelea kuishi ndani ya nyumba hizo na nyingine 1,036 ziliingiwa na
maji hata kama hazikuharibika.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
04 Februari, 2014


No comments:
Post a Comment