Rais Jakaya Mrisho Kikwete akinyanyua juu kitabu baada ya kuzindua Sera
ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA) akiwa
na mwasisi wake Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa
Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati
za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini
Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakati wa kuzindua Sera
ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA)
iliyoasisiwa na Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa
Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati
za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini
Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014.Picha na IKULU

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na vijana baada ya kuzindua Sera
ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA)
iliyoasisiwa na Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa
Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati
za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini
Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014.

Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na msanii wa vichekesho ambaye pia ni
mhubiri na mwimbaji wa nyimbo za injili Emmanuel Mgaya maarufu kama
Masanja Mkandamizaji baada ya kuzindua Sera
ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA) akiwa
na mwasisi wake Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa
Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati
za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini
Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014
KUSOMA HOTUBA YA RAIS BOFYA HAPO CHINI
============= ==========
HOTUBA
YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, WAKATI WA UZINDUZI WA SERA YA MTANDAO WA VIKUNDI VYA MAADILI
NA UCHUMI TANZANIA (MVIMAUTA), KWENYE UKUMBI WA BCIC, MBEZI BEACH,
TAREHE 15 FEBRUARI, 2014
Baba
Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO
Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa
Kizazi Kipya;
Mheshimiwa Sadiq Meck Sadiq, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Askofu Michael Peter Imani, Mwangalizi wa Makanisa ya WAPO Mission International, Kanda ya Dar es Salaam na Pwani;
Maaskofu Waangalizi wa Wapo Mission;
Ndugu Waumini;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani kwa Mwaliko
Nakushukuru sana Baba Askofu Mkuu Sylverster Gamanywa na viongozi wenzako wa Wapo Mission International
kwa kunialika na kunishirikisha katika tukio hili la kihistoria la
kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania
(MVIMAUTA). Nakushukuru kwa Risala ambayo imeelezea kwa ufasaha malengo
na madhumuni ya MVIMAUTA na jinsi mlivyojipanga kuyatekeleza na nini
mnachotegemea Serikali ifanye kusaidia utekelezaji wake. Napenda
kuchukua nafasi hii kukupongeza kwa dhati kwa ubunifu wako na kwa kazi
kubwa na nzuri unayoifanya wewe na Kanisa lako la kulea vijana wawe raia
wema na wenye manufaa kwa familia zao, jamii na taifa kwa jumla.
Hii ni mara
ya pili kwangu kushuhudia matunda ya ubunifu wako na kazi njema
inayofanywa na WAPO Mission International. Mara ya kwanza ni mwaka 2010
mliponishirikisha katika uzinduzi wa Mpango wa Kizazi Kipya Tanzania.
Matokeo ya Mpango ule ni kuanzishwa kwa Mtandao wa Vikundi vya Maadili
na Uchumi Tanzania ambao sera yake ndiyo hii tunayoizindua leo. Nasema
hongera sana Baba Askofu Mkuu na hongereni sana viongozi na waumini wa
WAPO Mission International.
Sera ya MVIMAUTA
Ndugu Baba Askofu Mkuu;
Napata faraja ya
pekee kuona kuwa mpango huu sasa umewekewa mkakati madhubuti wa
utekelezaji ili malengo yake yaweze kufikiwa. Sote tumekusikia ukieleza
kwa ufasaha maudhui ya sera na mikakati ya utekelezaji wake. Ni ukweli
ulio wazi kuwa ni Sera nzuri na hakuna mpenda maendeleo wa kweli
anayeweza kubeza au kukataa kuwaunga mkono. Jambo mnalokusudia kufanya
ni jema kwa nchi yetu na la manufaa kwa vijana ambao ndiyo taifa la leo
na kesho. Mnalenga kusaidia kundi muhimu linategemewa sana na familia
zao, jamii na nchi yetu kwa jumla. Kundi ambalo bahati mbaya
linakabiliwa na changamoto nyingi za kimaadili na kimaisha. Lakini
changamoto ni fursa za aina yake pia kwani changamoto hupanua mawazo ya
watu. Changamoto huwafanya watu kuwa wabunifu katika kutafuta
majawabu. Baba Askofu na viongozi wenzako mmefanya kile kinachostahili
kufanywa. Hongereni sana.
Mmelitimiza vyema jukumu la wazazi, familia,
jamii na viongozi wa dini kuwapatia watoto na vijana malezi mema ili
waweze kuzikabili na kushinda changamoto za kimaadili. Najua ni kazi
ngumu hasa katika dunia ya leo ya utandawazi inayoongozwa na teknolojia
za kisasa za habari na mawasiliano. Hatuna budi kuifanya kazi hiyo,
tena tufanye kwa umahiri na kushinda. Tukishindwa tutakuwa tumepata
hasara kubwa kwani tutakuwa na vijana wasiokuwa waadilifu jambo ambalo
ni hatari kwa maendeleo na ustawi wa familia, jamii na taifa. Na sisi
lazima tuwe wabunifu tutumie utandawazi huo huo na teknolojia hizo hizo
kuwajenga vijana wetu wawe na maadili mema. Natoa pongezi nyingi kwa
WAPO Mission International
kwa jitihada mzifanyazo kufanikisha jambo hili muhimu na la msingi
sana. Siyo kazi rahisi lakini ni jambo linalowezekana. Penye nia pana
njia. Dumisheni msimamo wenu na endelezeni juhudi mzifanyazo
mtafanikiwa. Mungu ni mwema atawabariki na kuwashindia kwa kazi njema
muifanyayo.
Risala
Baba Askofu Mkuu Gamanywa;
Waheshimiwa Maaskofu na Ndugu Waumini;
Sote
tumekusikia Baba Askofu ukieleza kwa ufasaha kwenye risala shabaha za
Sera ya Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania na jinsi mnavyokusudia na
mlivyojipanga kuzitekeleza. Lazima nikiri kuwa nimetiwa moyo na mambo
mazuri mliyokusudia kufanya. Ikiwa mtandao mnaotaka kuunda utafanya
kazi kama inavyokusudiwa, nina imani baadhi ya changamoto kubwa
zinazowakabili vijana nchini zitakuwa zimepata muarobaini. Mambo mengi
yameelezwa vizuri na Baba Askofu Mkuu na mimi sina sababu ya kuyarudia.
Lakini naomba nigusie machache ambayo nadhani yanahitaji kusemewa
kidogo.
Kwanza
naomba niwapongeze kwa hatua mliyofikia ya kuanzisha mchakato wa
kusajili Chuo Kikuu cha Uongozi wa Kimaadili na Taasisi ya Kukuza
Vipaji. Naomba mkamilishe mapema usajili wa taasisi hizi za aina yake
ili vijana wetu waanze kunufaika nazo. Kuhusu umilikishwaji wa ardhi,
nawashauri mpeleke maombi yenu kwa mamlaka zinazohusika bila ya shaka
mtafanikiwa. Nchi yetu ina ardhi ya kutosha ya kuwawezesha kujenga
taasisi hizo. Lakini ardhi hiyo ina wenyewe wanaoimiliki. Ama ni
wananchi mmoja mmoja au familia zao au Serikali za Vijiji au
Halmashauri za Wilaya na Miji. Ni kweli Katiba inasema ardhi yote ya
nchi hii ni mali ya Rais. Lakini Rais ni mdhamini tu wa ardhi ya nchi
yetu kwa niaba ya wananchi wote. Inampa fursa ya kutwaa ardhi ya mtu ye
yote kwa manufaa ya taifa. Hapo tunazungumzia mambo ya kitaifa ya
kunufaisha wengi. Wenye ardhi hasa ni hao niliowataja hapo juu, hivyo
anaetaka ardhi hana budi kuwaona. Mnachotakiwa ni kutambua ardhi
mnayoitaka kisha mumjue mwenyewe nani muonane nae na kuzungumza nae.
Naamini mtaelewana na wala hakapakuwa na lazima ya Rais kusema neno.
Baba Askofu;
Nimefurahi
kusikia kuwa kilimo ni miongoni mwa shughuli za vikundi vitakavyoundwa
katika utekelezaji wa sera hii. Mmefikiria jambo la maana sana. Ni
ukweli ulio wazi kamba kilimo kinatoa fursa kubwa za ajira kuliko sekta
nyingine yo yote. Kilimo hakivutii watu wengi hasa vijana kwa sababu ya
matumizi madogo ya teknolojia za kisasa. Kilimo ni kazi ya shuruba kwa
sababu ya kutegemea jembe la mkono na plau ya kukokotwa na ng’ombe
badala ya trekta. Inakimbiza vijana wasomi. Kilimo kina tija ndogo kwa
sababu ya kutegemea mvua ya Mwenyezi Mungu na matumizi madogo ya
pembejeo za kisasa kama vile mbegu bora, mbolea, dawa za kuua wadudu na
za kukinga na kutibu magonjwa ya mimea. Hali kadhalika kutokutumia
maarifa ya kisasa katika utayarishaji wa mashamba, upandaji na
mengineyo. Juhudi tulizozianza mwaka 2006 chini ya ASDP zina lengo la
kukitoa kilimo na kukifanya kiwe cha kisasa. Tuna program za kutoa
ruzuku ya pembejeo kwa wakulima na tayari wengi wananufaika. Tunao
mpango wa kuingiza matrekta na kukopesha wakulima katika vikundi vyao.
Naamini vikundi hivi navyo vinaweza kunufaika. Pia tunao mpango wa
kuanzisha Benki ya Wakulima kutoa mikopo kwa wakulima waweze kupata zana
na pembejeo za kilimo. Vikundi hivi vitanufaika pia. Ninawatia moyo
likazanieni hili la vikundi vya kilimo kwani ni jambo lenye matumaini
makubwa. Sisi Serikalini tutaendelea kushirikiana nanyi kufanikisha
malengo yenu.
Tutasaidia
upande wa mafunzo kwa vijana wetu. Maafisa ugani watawaelimisha
masuala ya kilimo. Kwa wale watakaojihusisha na viwanda ni vyema
mkashirikiana kwa karibu na SIDO kwani wao wanao utaalamu wa kutosha
katika shughuli za namna hiyo. Kwa suala la mitaji siwezi kusema kwamba
Serikali inaweza kuwa na fedha zote zitakazohitajika. Lakini, jungu
kuu halikosi ukoko. Tutasaidiana pale tutakapoweza. Hivi sasa upo Mfuko
wa kusaidia wajasiriamali na hasa kupitia vikundi vya uzalishaji mali na
huduma. Bahati mbaya mahitaji ni makubwa kuliko uwezo wa Mfuko, hivyo
wanaopata si wengi. Katika hao wanaopata baadhi ya vikundi hivi
vinaweza kuwa miongoni mwa hao.
Napenda
kuchukua nafasi hii kutoa wito kwa taasisi za Serikali, Mashirika ya
Umma na sekta binafsi, kuangalia namna ya kuchangia katika juhudi hizi
za Serikali. Siyo lazima watoe fedha, lakini wanaweza kufungua fursa za
kuwasaidia vijana katika vikundi vyao kama hivi vilivyoanzishwa na WAPO
Mission International. Wanaweza kufanya kama wanavyofanya Shirika la
Nyumba la Taifa na VETA. Imani yangu ni kuwa hivi vikundi vikisaidiwa
vitakua na kuwezesha vijana wengi zaidi kujitegemea badala ya kusubiri
kuajiriwa Serikalini au kwenye makampuni binafsi.
Mwisho
Kabla
ya kumaliza narudia kuwapongeza kwa jambo hili jema mlifanyalo leo.
Lakini ni sifa yenu ya miaka mingi. Napenda kuwaahidi kuwa Serikali
itajitahidi kufanya yale inayotakiwa kufanya ili sera hii tunayoizindua
leo ifikie malengo yake. We will play our part. Mwisho nawashukuru
tena kwa kunialika, nawapongeza wale wote alioshiriki kuandaa na
kufanikisha shughuli hii ya leo. Wamefanya kazi nzuri iliyotukuka.
Nawapongeza waumini na hasa vijana kwa kufika kwa wingi. Ninyi ndiyo
walengwa. Bila ya nyie hakuna MVIMAUTA. Naomba sote tuendelee kumuunga
mkono Baba Askofu Mkuu Sylvester
Gamanywa na kumtia moyo azidi kufanya mambo mengi mengine mazuri katika
kuwatumikia ninyi waumini wa Kanisa lake na Watanzania kwa jumla.
Tunakupenda sana. Tunatambua na kuthamini sana kazi njema uifanyayo.
Nawaomba muendelee pia kuliombea taifa letu, liendelee kuwa na amani na
utulivu na tupate mafanikio zaidi.
Baada ya kusema hayo, sasa natamka kwamba Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania, imezinduliwa rasmi.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:
Post a Comment