Polisi
wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya wakifungua dawa
zilizokamatwa jana kwenye jahazi liitwalo Kunarak-Iran lililokutwa
katika Bahari ya Hindi eneo la Tanzania likiwa na kilo 201 za heroini,
pamoja na raia wanane wa Iran na Wapakistan wanne. Picha na Michael
Jamson.
Kikosi
kazi cha Jeshi la Polisi cha Kudhibiti Uharamia Baharini kimekamata
kilo 201 za dawa za kulevya aina heroini zilizokuwa zikiingizwa nchini
kutoka Iran.
Kamishna
wa Polisi, Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa,
alisema jana kikosi hicho kikiwa kwenye doria ya kawaida kiliona boti
ambayo haikuwa na bendera wala kiashiria chochote ndipo walipoitilia
shaka na kuamua kuifuatilia.
Nzowa alisema kuwa mzigo huo ni mkubwa zaidi wa heroin kuwahi kukamatwa na vikosi vya doria vya Tanzania.
Alisema
mara ya mwisho kwa mzigo mkubwa zaidi wa heroin kuwahi kukamatwa
ilikuwa mwaka 2012 wakati zilipokamatwa kilo 70 za dawa hizo jijini Dar
es Salaam.
Nzowa alisema Kikosi cha Wanamaji kiliposhuku boti hiyo, kiliisimamisha na kugundua kuwa ilikuwa na watu 12.
Alisema baada ya uchunguzi wao waligundua kuwa kulikuwa na raia wanane wa Iran na wanne wa Pakistan.
“Boti
hiyo ilivutwa hadi ufukweni ambako leo (jana) ilifanyiwa uchunguzi na
ndipo zikakutwa na kilo 201 za heroin,” alisema Nzowa.
Nzowa alisema boti hiyo iliyosajiliwa Kunarak, Iran, ilikuwa inaongozwa na nahodha mwenye uraia wa nchi hiyo, Ayub Hot (50).
Nzowa
alisema kitakachofuata sasa ni kufanya upelelezi na kujua walikuwa
wanataka kupeleka wapi mzigo huo, kufahamu mtandao wao na walipanga
kufanya nini katika ufukwe wa Dar es Salaam.
Alisema baada ya upelelezi wao kukamilika watu hao watafikishwa mahakamani.
Naye
Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Polisi, ACP Mboje Kanga alisema watu
hao 12 hivi sasa wamewekwa mahabusu ya wanamaji na kikosi hicho kwa
kushirikiana na Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya wataendelea na
upelelezi.
Taarifa
ya mwaka 2011 ya Kitengo cha Dawa za Kulevya iliyochapishwa katika
ripoti ya Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Marekani inaeleza kuwa,
heroini huingia Tanzania kupitia Bahari ya Hindi ikitokea Afghanistan,
Iran, Pakistan na Falme za Kiarabu. MWANANCHi

No comments:
Post a Comment