![]() |
| Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba akiwaonyesha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu picha ya moja ya viatu vilivyokuwa na dawa za kulevya vilivyokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, jana. Viatu hivyo vilikuwa vikisafirishwa kwenda Liberia. |
Wasafirishaji
wa dawa za kulevya wamebuni mbinu mpya baada ya Kikosi cha Polisi cha
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kukamata kilo 3.5
za heroini zikiwa zimefungwa kwenye vifurushi zikipelekwa Monrovia,
Liberia.
Hatua
hiyo imekuja siku moja baada ya Kikosi cha Wanamaji cha Polisi kukamata
jahazi likiwa na kilo 201 za heroini wakati likisafiri kati ya Dar es
Salaam na Zanzibar.
Mkuu
wa Upelelezi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Hamad Hamad alisema jana
kuwa kifurushi hicho kilikamatwa Jumatatu saa tisa alasiri, kwenye
uwanja huo.
Hamad
alisema mmiliki wa kifurushi hicho kilichokuwa kinasafirishwa na
Kampuni ya Kusafirisha na Kupokea Mizigo (DHL) hajafahamika.
Kwa mujibu wa Hamad, mmiliki wa mzigo huo alikuwa ametumia jina la bandia pia maelezo ya mzigo ule yalikuwa ya uongo.
Hamad
alisema dawa hizo zilikuwa zimeingizwa ndani ya kandambili huku zikiwa
na vifurushi vingine kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Liberia.
“Kampuni ya DHL walipewa kazi ya kusafirisha mzigo huo na kujitetea kuwa hawakuelewa kulikuwa kitu ndani,” alieleza Hamad.
Hamad alisema kuwa polisi waliutilia shaka mzigo ule wakati ukipitishwa na kuamua kuukagua, ndipo wakakuta ni heroini.
Katika
hatua nyingine, Kamishna wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya,
Godfrey Nzowa alisema bado wanaendelea kuwahoji watu 12 raia wa nchi za
Iran na Pakistan waliokamatwa juzi na kilo 201 za heroini.
Alisema
pia wanaendelea kumchunguza raia wa Kenya, Abdulrahman Salim, ambaye
alikamatwa na kete 142 za dawa za kulevya aina ya cocaine kwenye Uwanja
wa JNIA.
Salim alikamatwa akitokea Brazil akiwa amepanda ndege ya Shirika la Ndege Ethiopia.
Mbinu zaidi
Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ameelezea mbinu mbalimbali
zilizobuniwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya, zilizobainika baada ya
watu saba walikamatwa katika matukio saba tofauti.
Dk
Tizeba alisema hata vitabu vimekuwa vikitumika ambapo wahusika wamekuwa
wakikata katikati ya vitabu hivyo na kuweka kete za dawa za kulevya
kabla hawajavisafirisha nje ya nchi. Hata hivyo jambo hilo sasa
wamelishtukia na udhibiti umeongezwa katika viwanja vya ndege.
“Hivi
karibuni tumekamata kitabu cha somo la baiolojia kikisafirishwa kwenda
Liberia na kilitiliwa shaka na kilipofunguliwa kilikutwa na kilo mbili
za dawa za kulevya,” alisema.
Alisema
wameamua kusafarisha kwa njia hiyo baada ya kuona mpango wa kumeza
umedhibitiwa na hadi sasa wahusika wa matukio hayo saba wamekamatwa, na
mmoja bado ila huenda akatiwa mbaroni wakati wowote.
“Saba tunao kwa mahojiano na mwingine ambaye anahusika na kitabu hicho cha baiologia anafuatiliwa,” alisema


No comments:
Post a Comment