Mhandisi
wa Ujenzi kutoka Shirika la Mafuta Tanzania (TPDC), Mhandisi Mwita
Yagela (Kulia) akiwaonesha michoro ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata
gesi Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume
ya Mipango ilipotembelea eneo la ujenzi huo, Madimba, mkoani Mtwara.
Wanaotazama ni wakaguzi hao, kutoka kushoto ni Prof. Longinus
Rutasitara, Bibi Salome Kingdom, Bibi Florence Mwanri na Bw. Jordan
Matonya.
Mmoja
wa viongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Katikati) akitaka ufafanuzi
juu ya maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo
Madimba, mkoani Mtwara. Wanaomsikiliza ni Mchumi Mwandamizi kutoka Ofisi
ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Salome Kingdom (Kushoto) na Mhandisi wa
Ujenzi kutoka Shirika la Mafuta Tanzania (TPDC), Mhandisi Mwita Yagela
(Kulia).
Timu ya Ukaguzi
wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais ikijionea maendeleo ya
ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Madimba, mkoani Mtwara.
Mhandisi
wa Ujenzi kutoka Shirika la Mafuta Tanzania (TPDC), Mhandisi Mwita
Yagela (Kulia) akiwaonesha mabomba ya kusafirishia gesi Timu ya Ukaguzi
wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
ilipotembelea baadhi ya maeneo yanakopita mabomba hayo. Mpaka sasa jumla
ya kilomita 350 kati ya kilomita 492 zimeshatandazwa.
Mmoja
wa wakaguzi kutoka Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi
ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Nancy Kitajo akistaajabu bomba za
kusafirishia gesi zinazoelekea kwenye kiwanda cha kuchakata gesi
kilichopo Madimba, mkoani Mtwara.
Vongozi
wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Prof. Longinus Rutasitara (Kushoto) na Bibi Florence Mwanri
(Kulia) wakiangalia moja ya bomba la kusafirishia gesi. Bomba moja lina
uzito wa tani tano na urefu wa mita 11. Mpaka sasa jumla ya kilomita 350
kati ya kilomita 492 zimeshatandazwa.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa makazi ya wafanyakazi katika kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Madimba, mkoani Mtwara.
Na Saidi Mkabakuli
Maendeleo
ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam unatarajiwa
kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu kufuatia kuendelea vyema
kasi ya kundaza bomba hilo.
Wakizungumza na wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Wahandisi wa Ujenzi kutoka Shirika la Mafuta Tanzania (TPDC), Mhandisi Mwita Yagela na Mhandisi Omary Kitiku wamesema
kuwa kasi ya sasa ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo
kijiji cha Madimba, mkoani Mtwara inatia moyo na hivyo kuashiria
kukamilika kwa mchakato huo kwa wakati.
“Mpaka sasa jumla ya kilomita 350 kati ya kilomita 492 za bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam zimeshatandazwa hali inayokwenda sambamba na mpangokazi wa ujenzi wa kiwanda hiki,” alisema Mhandisi Yagela.
Kwa
mujibu wa Mpangokazi wa ujenzi wa kiwanda hiko hadi kufikia mwisho wa
Julai kiwanda kinatakiwa kukamilika, na mpaka sasa, makazi ya
wafanyakazi imekamilika.
Akizungumza
wakati wa ukaguzi huo, Mmoja wa viongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi
ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri
alisema kwamba kukamilika kwa bomba hilo kunatoa mwanya wa kukamilika
kwa wakati uzalishaji wa umeme katika vituo vya Kinyerezi, jijini Dar es
Salaam.
“Kukamilika
kwa bomba hili kunatoa fursa ya kwa Mradi wa kuzalisha umeme kiasi cha
Megawati 150 na Megawati 240 kwa kutumia gesi asilia vilivyopo
Kinyerezi, jijini Dar es Salaam,” alisema Bibi Mwanri.
Kwa
mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 -
2015/16), Miundombinu ni kipaumbele cha kwanza, hasa uwekezaji mkubwa
katika miundombinu ya nishati ambapo nguvu kubwa imewekwa katika
uwekezaji wa miundombinu ya nishati ambapo utekelezaji wa ujenzi wa
bomba la gesi Mtwara hadi Dar es Salaam unafanywa sambamba na ujenzi wa
mitambo miwili ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi katika eneo la
Kinyerezi Dar es Salaam.
Serikali
imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 -2015/16) wa
kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo kuu la Mpango huu ni
kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi ya ukuaji
mpana wa uchumi na unaolenga watu walio masikini zaidi. Mpango wa Kwanza
wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja wa mipango
mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa utekelezaji na
kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi
ya maendeleo kitaifa.
No comments:
Post a Comment