Misululu
ya magari ilikuwa ni ya kawaida kuonekana nyakati za asubuhi na jioni
wakati watu wakielekea na kutoka kazini, lakini sasa foleni zimekuwa ni
za kawaida katikati ya jiji na maeneo mengine ambayo ukarabati wa
barabara unaendelea wakati wote.
Dar es
Salaam. Wakati kukiwa na ongezeko kubwa la ununuzi wa magari na
kusababisha idadi kubwa ya vyombo hivyo vya usafiri, foleni za magari
nchini, hasa jijini Dar es Salaam, imefikia hatua ya kutisha huku
ikisababisha madhara makubwa kiuchumi, kijamii na kiafya, ikiwamo
magonjwa ya akili.
Misululu ya magari ilikuwa ni ya kawaida kuonekana nyakati za asubuhi
na jioni wakati watu wakielekea na kutoka kazini, lakini sasa foleni
zimekuwa ni za kawaida katikati ya jiji na maeneo mengine ambayo
ukarabati wa barabara unaendelea wakati wote.
Wakati kukiwa na kasi ndogo ya ukarabati wa miundombinu ya usafiri,
kumekuwa na ongezeko kubwa la magari jijini Dar es Salaam. Pia
kumekuwapo na ongezeko kubwa la idadi ya watu hadi kufikia milioni 4.3
kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002 huku vyombo vya usafiri wa umma
(daladala) vikitumia njia zisizo sahihi (kutanua), kufanya foleni kuwa
kubwa hali inayosababisha jiji kuwa kero kwa muda wote.
Licha ya jitihada za Serikali kutumia treni kusafirisha abiria ili
kusaidia kupunguza msongamano wa magari nyakati za asubuhi na jioni,
bado tatizo hilo ni kubwa. Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi, Dk. John
Pombe Magufuri aliagiza Kampuni ya Strabag, inayojenga miundombinu ya
mabasi yaendayo kasi, kufungua barabara zilizokamilika ili kupunguza
msongamano.
Kutokana na tatizo hilo, wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine
yanayoathiriwa na foleni, wamekuwa wakilazimika ama kusitisha safari au
kuchelewa kazini na kwenye shughuli nyingine, huku vyombo vya usafiri
vikilazimisha kufanya safari chache na hivyo wamiliki kupata fedha
kidogo kuliko matarajio yao.
“Madereva wanapata magonjwa ya akili kutokana na kero za barabarani,”
alisema Dk. Innocent Godman, ambaye ni mmoja wa wataalamu wa nyanja
tofauti aliyeongea na gazeti hili kuhusu tatizo hilo.
“Kwanza ni msongo wa mawazo kuhusu uchumi kutokana na mafuta mengi
kupotea njiani; pili barabara mbovu; tatu hasira za kuchelewa
anakokwenda; na nne wanakumbana na askari wa usalama barabarani ambao
wanawakamua fedha,” alisema mtaalamu huyo wa magonjwa ya akili na
mshauri nasaha kuhusu utumiaji wa madawa ya kulevya.
Tanzania inaelezwa ni nchi inayoongoza kwa kuwa na msongamano mkubwa wa magari katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Zatafuna mabilioni ya shilingi
Katika utafiti wake, Wakala wa Mradi wa Mabasi ya Kasi (DART), Jumbe
Katala amebaini kuwa foleni husababisha ajali za barabarani, upotevu wa
nishati (mafuta) na muda wa kukaa barabarani mambo ambayo husababisha
hasara ya zaidi ya Sh655 bilioni kwa mwaka.
Katika utafiti huo, Katala alibaini kuwa foleni hizo husababisha
kudorora kwa uchumi, huku bei ya mafuta ipanda kutokana na mahitaji ya
nishati hiyo kuongezeka.
Alisema kuendesha na kuzima gari mara kwa mara kwa sababu ya foleni
huongeza matumizi makubwa ya gari na kuongeza kasi ya uchakavu wake,
hivyo kusababisha gharama kubwa za matengenezo ya mara kwa mara.
Madhara kiafya
Kiafya, foleni pia zinatajwa kusababisha maradhi lukuki yakiwamo
magonjwa ya akili, pumu, maradhi ya mfumo wa hewa, mzio utokanao na
mafuta na maradhi ya moyo.
Msongamano wa magari pia husababisha wasafiri hasa madereva kuvuta
hewa chafu itokanayo na mafuta ya magari na maradhi ya mfumo wa hewa
kutokana na kutovuta hewa safi. Dk. Godman alisema madereva wengi wa
Tanzania wana magonjwa ya akili kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni
pamoja na foleni.
“Madereva wanapata zaidi ya magonjwa ya akili hata mara mia moja
zaidi,” alisema Dk. Godman. Dk. Godman alisema msongo wa mawazo
unaotokana na adha za usafiri nchini umewaathiri watu wengi na
kusababisha wawe na lugha chafu, hasira za mara kwa mara na uongo.
“Foleni za magari kwa hapa nchini ni zaidi ya janga kwa sababu unaathiri
kila sekta ya maisha,” alifafanua.
Kutokana na utafiti huo, madereva wengi wanaofanya kazi katika maeneo
hayo, hasa katika mabasi ya mijini (daladala) kwa muda mrefu, wanatajwa
kuwa katika hatari ya kupata maradhi ya akili kutokana na kuwa na
msongo kwa kipindi kirefu.
“Wengi wao wanavuta bangi, halafu wakichanganya foleni ya barabarani
na ugumu wa maisha, huo ni ugonjwa wa akili,” alisema. Wanasayansi
wanautaja ugonjwa huo kwa kitaalamu kuwa ni ‘maradhi ya msongo wa
foleni’ (Traffic Stress Syndrome).
Kuvunja ndoa
Wataalamu wa masuala ya kijamii wanaeleza kuwa madereva na abiria
wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenye foleni na kusababisha kupoteza
muda ambao wangeutumia kwenye uzalishaji.
Kutokana na hali hiyo, bila takwimu wanasema abiria hao wengi
hulazimika kusema uongo kwa kuchelewa katika mikutano ya kikazi, elimu,
biashara na wakati mwingine watu kuadhibiwa kwa kuchelewa maofisini na
majumbani, jambo linalosababisha kuyumba kwa ndoa.
Hasara zaidi
Mhadhiri wa Uchumi, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji
Semboja anachanganua hasara ya msongamano katika mtazamo wa upotevu wa
muda na mafuta.
Anasema, iwapo magari yatachukua muda mrefu kufika eneo moja, basi
hata bidhaa zitapanda bei, kwa sababu mafuta mengi yanatumika njiani.
“Chombo cha moto kilichotumia dakika kumi, si sawa na kilichotumia saa
nzima, ukijumlisha hasara ya mafuta ni sawa na kujenga barabara zote
hapa nchini,” alisema.
Profesa Semboja alisema kuwa msongamano wa magari unachangia kuwapo
uzembe kazini na sasa imekuwa kawaida mtu kusingizia kachelewa kazini
kwa sababu ya foleni.
“Jambo la muhimu ni kutafuta kiini cha tatizo, mfumo wa barabara
ambao hauendani na mfumo wa maji, makazi, biashara, maisha na ofisi,”
alisema.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Greyson Lwenge alisema hakuna ubishi
kuwa foleni zinasababisha hasara, hasa ya utumiaji mkubwa wa mafuta na
muda unaopotezwa kwenye foleni barabarani.
“Kwa hali ya kawaida foleni ni hasara, mahali pa dakika 10 unatumia
nusu saa au wakati mwingine saa nzima. Ndiyo maana tumekuja na miradi
hiyo ili kupunguza msongamano,” alisema Waziri Lwenge.
Hata hivyo, Waziri Lwenge alisema Serikali imejipanga vyema na mradi
wa mabasi yaendayo kasi, Daraja la Kigamboni, barabara za juu na upanuzi
wa barabara kuu ili kupunguza msongamano wa magari.
No comments:
Post a Comment