ALLIANCE FOR CHANGE AND TRANSPARENCY
(ACT TANZANIA)
MABADILIKO NA UWAZI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jumatatu, 03 Machi 2014, Dar es Salaam
1. Utangulizi
Ndugu wana habari,
Naomba nichukue fursa hii
kuwashukuru kwa kuitikia wito wa kuhudhuria mkutano wetu, ambao ni wa
kwanza tangu chama chetu kianzishwe. Tunatambua na kuheshimu kazi yenu
kama mhimili wa nne wa dola, na leo tunaomba kuzungumza na watanzania
kupitia kwenu.
Lengo kuu la mkutano huu ni
kukitambulisha kwenu chama kipya cha siasa kinachoitwa Alliance for
Change Tanzania (ACT Tanzania) na kuwaombeni kukitambulisha chama hiki
kwa watanzania kupitia vyombo vyenu vya habari.
2. ACT Tanzania ni nini?
Ndugu Wanahabari,
ACT Tanzania ni kifupi cha
maneno: Alliance for Change and Transparency, yaaani Umoja wa Mabadiliko
na Uwazi. Ni chama kipya cha siasa kilichoanzishwa kwa lengo mahsusi la
kuwaleta pamoja watanzania wanaoamini kwamba nguvu ya pamoja
inahitajika katika kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi hii, na kwamba
uwazi na uadilifu ni tunu ambazo taifa hili linazihitaji sana kwa sasa
na baadaye.
3. Itikadi na Misingi ya ACT Tanzania
ACT Tanzania ni chama
kinachoaamini katika demokrasia jamii na chenye shabaha kuu ya kupigania
na kusimamia mabadiliko na uwazi nchini Tanzania. ACT-Tanzania inaamini
kuwa mabadiliko yoyote katika jamii lazima yainufaishe jamii husika, na
kwamba wananchi wenyewe ni lazima washiriki katika kuleta mabadiliko
hayo kwa uwazi na uzalendo. Mwongozo wa sera za ACT-Tanzania ni
maendeleo shirikishi na kuhakikisha uwepo wa uongozi adili katika ngazi
zote.
ACT Tanzania inaongozwa na misingi mikuu mitano ifuatayo:
i) Uzalendo
ACT-Tanzania inaamini kwamba
kila mwananchi ana wajibu wa msingi kabisa wa kutoa mchango wake katika
jamii na Taifa kwa ajili ya kuhifadhi ustawi wa nchi kwa ajili ya kizazi
cha leo na cha baadaye. Ili wananchi waweze kutoa mchango huu kwa dhati
na kwa moyo, ni muhimu mazingira yawepo ya kuhakikisha kwamba wananchi
wanaipenda nchi yao. Kwa msingi huu, ACT-Tanzania itajenga mazingira
mwafaka ya wananchi kuipenda nchi yao ili wajitoe kikamilifu katika
kuijenga na kuilinda. ACT-Tanzania itajenga mazingira yatakayoongeza
uzalendo wa wananchi kwa kuhakikisha uwepo wa uwazi, ulinzi na utumiaji
bora wa rasilimali za taifa na uadilifu wa viongozi.
ii) Usawa
ACT-Tanzania inaamini katika
usawa katika yyanja zote. Tunaamini kwamba mafanikio ya mtu mmoja mmoja
na jamii kwa ujumla yatatokana na bidii katika kazi. Kwahiyo, ACT
Tanzania kitapigania kuwepo usawa wa fursa na mazingira mazuri kwa wote
katika kuhakikisha kwamba kila mtu na kila kundi katika jamii linakuwa
na fursa sawa ya kufanya kazi za kujiajiri au kuajiriwa, na kwamba
kipato kitokanacho na kazi halali ndicho kitakuwa kipimo cha mchango
wake katika jamii na taifa.
iii) Uadilifu
Uadilifu katika maisha binafsi
na katika jamii utakuwa ndio msingi na mwongozo mkuu wa viongozi na
wanachama wa ACT-Tanzania. ACT-Tanzania inaamini kwamba uadilifu ndio
msingi na nguzo kuu ya mapambano dhidi ya rushwa na maovu mengine katika
jamii.
iv) Uwazi na uwajibikaji
ACT Tanzania inaamini katika
uwazi kwenye mambo yote ya kijamii na kitaifa. Hivyo basi viongozi na
wanachama wa ACT-Tanzania wana wajibu wa kupigania uwazi katika mambo
yote wanayofanya kwa ajili ya umma. Sambamba na uwazi, ACT- Tanzania
inaamini kwamba kila mwananchi na kiongozi mwenye dhamana katika umma
ana wajibu katika jamii na Taifa kwa ujumla na ni jukumu lake kutekeleza
wajibu huo bila kinyongo. Aidha, mwanachama na kiongozi atokanaye na
ACT Tanzania anapaswa kuwajibika kwa maneno na matendo yake katika
utumishi au nje ya utumishi wa chama au taasisi yeyote ya umma. ACT
Tanzania inaamini kwamba bidii katika kazi ndiyo njia pekee ya kujipatia
maendeleo.. Hivyo basi wajibu mkuu wa mwanachama wa ACT Tanzania
utakuwa ni: BIDII KATIKA KAZI.
v) Demokrasia ya Kweli
ACT-Tanzania inaamini
demokrasia ndiyo msingi wa kujenga fikra pevu na kueneza uhuru wa mtu,
jamii na Taifa kwa ujumla. Hivyo basi, viongozi na wanachama wa
ACT-Tanzania watapigania uwepo wa demokrasia ya kweli katika kila ngazi,
ndani na nje ya chama. Kila jambo lenye maslahi mapana katika chama na
katika umma litaamuliwa kwa njia ya kidemokrasia ya moja kwa moja au
kupitia kwa wawakilishi waliochaguliwa.
4. Taarifa ya Kazi na mipango ya mbele
� ACT Tanzania imekwisha kukamilisha rasimu ya awali ya Katiba ambaye iliwezesha kupata usajili wa muda
� Zoezi la kuandikisha
wanachama katika mikoa kwa ajili ya kuomba usajili wa kudumu kwa mujibu
wa sheria limekwishakamilika. Tumewapata wanachama katika mikoa yote ya
Tanzania Bara na Zanzibar. Hata hivyo, tumechagua mikoa kumi ambayo
tungependa msajili akahakiki kama sheria inavyotaka.
� Baada ya kukamilisha zoezi
la kuandikisha wanachama, wiki hii kabla ya Ijumaa tutapeleka fomu na
mahitaji mengine husika kwa Msajili wa vyama ili aweze kupanga ratiba ya
zoezi la uhakiki.
� Mara baada ya msajili kutoa usajili wa kudumu kwa muda atakaopanga, tutafanya uchaguzi wa kwanza mkuu
� Kama itampendeza msajili
akatupatia usajili wa kudumu mapema, tunatarajia kushiriki kwa nguvu
zote katika chaguzi zote ndogo zitakazojitokeza, uchaguzi wa serikali za
mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.
5. Shukrani
� Napenda kuchukua nafasi hii
kuwashukuru waratibu wote wa zoezi zima la uandikishaji wanachama
waliojitolea kwenye mikoa na wilaya mbalimbali katika kuhakikisha zoezi
hili linafanikiwa kwa wakati uliopangwa.
� Natoa wito kwa wanachama na
wapenzi wa chama popote walipo waendelee kukichangia chama kwa nguvu
zao, muda wao, taaluma zao na kwa kila hali kadri uwezo unavyomruhsu
kila moja wetu.
� Nawashukuru sana wataalam na
watafiti wetu mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea kutumia utaalam wao
kutushauri katika maeneo mbalimbali ya utafiti, uongozi, sera,
raslimali, usimamizi wa fedha, mawasiliano, sheria, sayansi ya siasa, na
kadhalika.
6. Wito kwa wanachama na watanzania
Tunatoa wito kwa kila mwanachama, mfuasi na mpenzi wa ACT-Tanzania popote walipo nchini kuhakikisha kwamba:
� wanazingatia misingi ya
chama iliyoanishwa hapo juu katika shughuli zao zote. Wakukumbuke kila
mara kwamba lengo kuu la chama hiki ni kupigania na kusimamia mabadiliko
na uwazi katika kila ngazi. Tungependa kila shughuli ya chama iwe
shirikishi na wazi kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
� anafanya kazi kwa bidii katika kukijenga chama na kushiriki maendeleo katika jamii aliyomo,
akizingatia kwamba chama hiki
kinaamini kwamba bidii katika kazi ndiyo njia pekee ya kujipatia
maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Hivyo, kila
mwanachama ahakikishe anatoa mchango wake katika kukijenga chama na
kuleta maendeleo katika jamii husika aliyomo.
� Tunawakaribisha watanzania
wote popote walipo na wanaoamini katika misingi tuliyoainisha hapo juu
kujiunga na ACT Tanzania. Kila mtanzania anayejiunga na chama hiki
akumbuke kuchukua wajibu wake katika kukijenga chama popote pale alipo.
Na akumbuke wajibu mkuu kwa mujibu wa chama hiki kuwa ni: BIDII KATIKA
KAZI.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki ACT-Tanzania, ahsanteni kwa kunisikiliza!
Kadawi Lucas Limbu,
Mwenyekiti wa Taifa
ACT Tanzania
No comments:
Post a Comment