MCHUNGAJI
mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Usharika wa Mfarasi kata ya Madilu
wilayani Ludewa, mkoani Njombe, Petro Chambachamba (87) anashikiliwa
Polisi akihusishwa kwenye kesi ya mauaji. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Njombe, Fulgence Ngonyani, amesema jana kuwa Chambachamba pamoja na watu
wengine wanane, wamekamatwa wakihusishwa na mauaji yaliyotokea Februari
25, mwaka huu saa 8 mchana katika kijiji cha Mfarasi.Alisema watu hao
wanatuhumiwa kuchukua sheria mkononi kwa kumpiga hadi kumsababishia kifo
Boniface Mtweve (35), mkazi wa kijiji cha Ilininda kilichoko kata ya
Madilu wakimtuhumu kuiba simu tatu mali ya Nuru Ngairo.Kamanda alisema
kwa kupitia taarifa za siri kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho, Februari
28, watu hao walikamatwa na kufikishwa mikononi mwa dola. Wengine
waliokamatwa ni Linus Chaula, Stanley Katembo, Ery Mwapinga, Kedimoni
Mwapinga, Phillimon Mgimba, Richard Mvalla, Meshack Mgaya na Nuru
Ngairo.
“Ushahidi
wa awali unawahusisha watu hao tisa akiwemo mchungaji huyo, hata hivyo
wanaweza kuachiwa huru endapo baadaye wataonekana kutohusika na tuhuma
hiyo na uchunguzi unaendelea,” alisema Kamanda.
Hata
hivyo, waumini wa usharika huo wamedai vyanzo vya taarifa za Polisi
zinazomuhusisha mzee huyo katika kesi hiyo, ni vya uongo na wameomba
aachiwe huru.
Zaidi ya
wananchi 600 wa kijiji hicho, juzi walishiriki mkutano maalumu
wakishutumu kuchukuliwa kwa mchungaji pamoja na watuhumiwa wengine.
Katika
mkutano wa kijiji uliofanyika katika kijijini Mfarasi, Mwenyekiti wa
Kijiji hicho, Petro Mwapinga alisema, “ inasikitisha Polisi walivamia
kijijini hapa usiku wa manane na kuwakamata ndugu zetu bila kushirikisha
uongozi wa kijiji.”
Ofisa
Mtendaji wa Kijiji hicho, Samwel Mtewele alisema wote wanaotuhumiwa
kuhusika katika mauaji hayo, ni wale waliotoa taarifa katika kituo cha
Polisi cha Lugarawa wilayani Ludewa, kwamba nyumba zao zilivunjwa na
mali zao mbalimbali ziliibwa.
Msaidizi
wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kusini Magharibi,
Michael Lugome, alieleza kushangazwa na hatua ya Polisi kumkamata
mchungaji huyo na wenzake.
“Taarifa
tuliyopewa na Kijiji inaonesha kwamba kabla ya mauaji hayo, Mchungaji
wetu mstaafu na watuhumiwa wengine, walivunjiwa nyumba zao na mali zao
kuibwa; taarifa hizo zilipelekwa Polisi, na askari walipaswa kuzifanyia
kazi taarifa za wizi huo,” alisema Lugome.
“Hili ni
tukio la aina yake na yawezekana likawa la kwanza; lakini tuna maswali
ya kujiuliza ni wapi na katika mazingira gani tukio hilo lilitokea na
watu hawa akiwemo mzee huyo wa miaka 87 alishirikije katika tukio hilo,”
alisema Mwenyekiti wa Idara ya Uinjilisti ya Dayosisi hiyo, Nicholaus
Mgaya.
Mke wa
Mchungaji huyo, Lea Chambachamba, alisema mumewe alikuwa nyumbani wakati
watu wenye hasira kali kijijini hapo wakimpiga mtuhumiwa.
Alisema kabla ya tukio hilo, nyumba yake ilivunjwa na vitu kuibwa ambavyo inadaiwa mtuhumiwa huyo aliyeuawa, alikutwa navyo.
“Polisi
hawajatenda haki, mume wangu ana miaka 87, mimi nina miaka 70; mzee wa
umri huo anawezaje kwenda kwenye kundi lenye watu wengi na kushiriki
kumshambulia mtu?” alisema.
No comments:
Post a Comment