Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto inawataarifu wananchi wote kuwa
tarehe 8 Machi ya kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine
wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Madhumuni ya maadhimisho haya ni kutoa fursa ya kupima utekelezaji wa
maazimio, matamko na mikataba ya Kimataifa, Kikanda na Kitaifa inayohusu
masuala ya maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia.
Madhumuni
mahususi ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii
juu ya umuhimu wa kutambua uwezo wa wanawake katika kuchangia kuleta
maendeleo yao endelevu; kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali
zilizofanywa na Serikali na wadau katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na
kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu kujiletea maendeleo yao,
familia zao na Taifa kwa ujumla.
Kauli
mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2014 ni:
”Chochea Mabadiliko Kuleta Usawa wa Kijinsia”. Ujumbe huu unasisitiza
kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya
jinsia katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo. Mwelekeo wa
maendeleo kijamii, kitaifa na kimataifa unasisitiza na kuhimiza kuandaa
na kutekeleza mipango inayozingatia ushirikishwaji na ushiriki stahiki
wa wanawake na wanaume katika kujiletea maendeleo yao.
Maadhimisho
haya kwa mwaka 2014 yatafanyika ngazi ya mkoa. Maadhimisho hutoa fursa
maalum kwa Taifa, mikoa, wilaya na wadau wengine kupima mafanikio
yaliyofikiwa katika kumwendeleza mwanamke na kubainisha changamoto
zinazowakwamisha kufikia azma ya ukombozi na maendeleo ya wanawake na
kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
Wizara
ya Maendeleleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inatoa wito kwa mikoa yote
kushirikisha wananchi na wadau wote katika kuadhimisha siku hii kwa
namna watakavyoona inafaa kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu. Kwa
pamoja tunaweza kushiriki kujiletea maendeleo ya familia na Taifa kwa
ujumla. Nimatumaini yangu kuwa kupitia maadhimisho haya jamii itachochea
mabadiliko ya kuwashirikisha wanawake na wasichana katika kupanga na
kutekeleza mipango mkakati na progamu za kiuchumi, kijamii na kisiasa
ili kufikia maendeleo endelevu ya nchi yetu.
Aidha,
nawaomba wanahabari wote nchini kushirikiana na wadau mbalimbali
ikiwemo Serikali na taasisi zisizo za kiserikali, asasi za kiraia na
wadau wamaendeleo kutangaza na kuelimisha jamii mifano bora inayoonyesha
jinsi mwanamke na msichana akipewa fursa na kuwezeshwa hutoa mchango
mkubwa sana kwa familia yake na taifa kwa ujumla. Hili ndilo lengo la
kuadhimisha siku hii. Tueleweke kuwa wanawake ni zaidi ya asilimia 50
(hamsini) ya watanzania wote.Wakishirikishwa ipasavyo katikia shughuli
za maendeleo mchango wao ni mkubwa sana.
Nawatakia mafanikio mema katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Anna T. Maembe
KATIBU MKUU
03/03/2014
No comments:
Post a Comment